Rais Magufuli Aapa Kuwatumbua MAJIPU Viongozi wa Sekretarieti ya EAC.......Asema Pesa Walizotumia Kuandaa Mkutano ni Nyingi Sana



WAKUU wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameazimia Rais John Magufuli awe Mwenyekiti wa jumuiya, kwa maana kwamba Tanzania iendelee mwaka mwingine kuongoza kipindi ambacho Burundi ndiyo ilipaswa kushika wadhifa.
Dk Magufuli ambaye anaongoza jumuiya hiyo ambayo imepata mwanachama mwingine, Sudan Kusini, ameanza kwa kasi kubwa huku akipenyeza msimamo na falsafa yake ya ‘kutumbua majipu’ kuhakikisha nchi wanachama wanakwenda pamoja na kuleta maendeleo ya wananchi.
Hayo yalifanyika katika mkutano wa kawaida wa 17 wa Jumuiya, ambapo wakuu hao wa nchi pia walikubaliana kwa pamoja Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kushirikiana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kutatua mgogoro wa Burundi.
Magufuli aliahidi atafuatilia Sekretarieti ya EAC, kuhakikisha inafanya kazi kwa maslahi ya wananchi wa nchi wanachama na si kuwanyonya.
Rais Magufuli alihimiza viongozi wakuu wa umoja huo, kutoa kipaumbele katika ujenzi wa viwanda. Alisisitiza msimamo wake kupitia Sekretarieti ya jumuiya hiyo, kubana matumizi kuhakikisha malengo ya kuleta maendeleo katika nchi wanachama yanatimia.
Akizungumzia gharama za ukumbi waliotumia kwa ajili ya mkutano huo wa 17 kwenye Hoteli ya Ngurdoto, Magufuli alisema dola 45 kwa kichwa zilizotumika ni nyingi ambazo kama zingebanwa, zingeokoa fedha ambazo zingenunua madawati na kwenda kusaidia mahali pengine.
“Mwito wangu kwa sekretarieti, muwe cost conscious (macho na gharama),” alisema.
“Tubane sana matumizi iwezekanavyo, tukahudumie watu masikini na si kuwa na Sekretarieti inayokuwa parasite (nyonyaji),” aliendelea kusema.
Sekretarieti hiyo inaongozwa na Liberal Mfumukeko kutoka Burundi, aliyeteuliwa na wakuu hao wa nchi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano baada ya Dk Richard Ssezibera wa Rwanda, muda wake kumalizika.
Magufuli katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, alisema amepiga hesabu ukumbi huo ni ghali. Alitoa mwito kwa sekretarieti na watumishi wote kwamba ni lazima wafahamu kwamba wako kwa watu masikini na wanahudumia watu masikini katika nchi wanachama.
“Nataka niiambie Sekretarieti, Marais wamefanya kosa sana kunichagua mimi kuwa mwenyekiti. Nitahakikisha nawafuatilia kweli. Kwa hiyo mjipange vizuri na kama patakuwapo mmoja wa wafanyakazi anakwenda sehemu isiyotakiwa, nitaripoti kwa nchi anakotoka ili atumbuliwe jipu,” alisema.
Alisisitiza ifanye kazi kwa niaba ya nchi zao kwa kutengeneza sheria na mambo yatakayozisaidia. Alihimiza sekretarieti isiwe sehemu ya walalamikaji, bali wawe watatuzi wa matatizo ya jumuiya.
Alisema nchi wanachama wanapaswa kubadilika, kuwa na mtazamo wa kuhakikisha wananchi wake wananufaika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tunapaswa kutembea pamoja kwa maslahi ya jumuiya,” alisema. Rais Magufuli anaongoza jumuiya hiyo kwa mwaka mmoja, nafasi ambayo ilipaswa sasa ichukuliwe na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.
Hali hiyo inatokana na nchi hiyo kuomba kuachia nafasi hiyo ili kuelekeza nguvu zake katika kushughulikia matatizo yake ya ndani, lakini ilipewa nafasi ya kutoa Katibu.
Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi huku Sudan Kusini ikiwa imekidhi vigezo na kukubaliwa kuwa mwanachama mpya wa jumuiya hiyo katika mkutano huo wa 17.

Comments

Popular posts from this blog