PROF. MUHONGO AAGIZA MALIPO YA USHURU WA HUDUMA YAFANYIKE HADHARANI
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kulia)
akikata utepe kuashiria ufunguzi wa mgodi. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Musoma, Zelothe Stephen
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiwasili
katika mgodi wa dhahabu wa Cata Mining. Kulia ni Mkurugenzi wa mgodi
huo, Mahuza Nyakirang’ani.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akikagua
shughuli zinazoendelea mgodini hapo. Kushoto kwake ni Meneja wa mgodi
huo, Peter Bourhill na kulia kwake ni Mkurugenzi wa mgodi, Mahuza
Nyakirang’ani.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akisalimiana na baadhi
ya wananchi kutoka vijiji vya jirani na mgodi wa Cata Mining
waliohudhuria mkutano wake wa hadhara ili kujadili masuala mbalimbali.
Meneja
wa mgodi wa Cata Mining, Peter Bourhill akimweleza jambo Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokua akikagua mgodi huo.
Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa mgodi, Mahuza Nyakirang’ani.
Prof. Muhongo aagiza Malipo ya Ushuru wa Huduma yafanyike hadharani
Serikali
imeagiza ulipaji wa ushuru wa huduma unayofanywa na migodi mbalimbali
nchini ufanyike hadharani ili kila mwananchi aelewe kiasi kilicholipwa.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa agizo hilo hivi
karibuni alipofanya ziara kwenye mgodi wa dhahabu wa Cata Mining uliopo
katika kijiji cha Kataryo, mkoani Mara ambapo vilevile alikagua shughuli
za mgodi huo na kuweka jiwe la msingi.Profesa Muhongo alisema ili
kuondoa hali ya sintofahamu pamoja na kuongeza uwazi na utekelezaji
sahihi wa miradi kutokana na fedha zitokanazo na malipo ya ushuru wa
huduma, ni lazima ulipaji huo wa ushuru husika ukashuhudiwa na kila
mwananchi.
Aliongeza
kwamba wananchi wanapaswa kushirikishwa katika kuibua miradi
itakayotekelezwa kwa kutumia fedha hizo za ushuru wa huduma.“Wananchi
wanapaswa kuelewa ni kiasi gani kimelipwa; na hiyo haitoshi inatakiwa
washirikishwe kwenye matumizi ya fedha hiyo.”
Waziri
Muhongo alimuagiza Kamishna wa Madini kuandika barua kuikumbusha migodi
yote nchini pamoja na Halmashauri ambazo kuna migodi kufuata utaratibu
uliowekwa. “Migodi itaandaa mfano wa hundi ya malipo husika na italipa
hadharani kwenye mikutano ya hadhara ili kila mwananchi wa eneo husika
ashuhudie, na aelewe kiasi halisi kilicholipwa”.
Alisema
baada ya kupokea malipo hayo, wananchi wapewe fursa ya kueleza wanataka
fedha hiyo iliyolipwa itumike vipi, ndipo madiwani wajadili utekelezaji
wake. “Asilimia 0.3 inayolipwa kama ushuru wa huduma ni lazima iende
kwenye miradi ya maendeleo ya maeneo husika na sio vinginevyo”
alisisitiza.
Akiuzungumzia
mgodi wa Cata Mining, Mahuza Nyakirang’ani ambaye ni mmoja wa
wakurugenzi wa mgodi huo alisema unamilikiwa na wamiliki watatu ambapo
wawili ni kutoka nchini Tanzania na mmoja kutoka nchini Canada.Alisema
gharama zilizotumika katika uwekezaji huo ni kiasi cha Dola za Marekani
milioni 54 ambapo baadhi ya fedha ni mikopo kutoka Benki ya CRDB na TIB
na fedha zingine zimetolewa na mbia wao wa Canada.
Nyakirang’ani
alieleza kuwa mgodi huo ni wa kati na utaanza uzalishaji kwa kutumia
marudio ya mchanga wa dhahabu uliochimbwa kipindi cha nyuma na
wachimbaji waliokuwepo hapo kipindi cha nyuma na kwa baadaye ndipo
wataanza kuchimba rasmi.
Akizungumzia
suala la uwajibikaji kwa jamii (CSR), Nyakirang’ani alisema mbali na
kwamba mgodi huo haujaanza uzalishaji, lakini umeanza taratibu za
kuboresha ujirani mwema kwa kuhakikisha wanachangia katika shughuli za
kimaendeleo kwa jamii zinazozunguka mgodi huo.Alisema mgodi huo umejenga
madaraja ya kudumu matatu, umeshiriki katika ujenzi wa barabara, shule
na zahanati. “Hapo awali ilikuwa mvua zikinyesha watoto wanashindwa
kuvuka kuja upande ilipo shule maana hakukuwa na daraja na hivyo maji
yalikuwa yakijaa lakini sasa watoto wanakwenda shule bila wasiwasi,”
alisema.
Aidha,
Profesa Muhongo alifanya mkutano wa hadhara na kuzungumza na wananchi
wa vijiji vya maeneo ya jirani na mgodi huo ambapo aliagiza wamiliki wa
mgodi huo kutoa ajira bila upendeleo kwa wananchi wanaozunguka maeneo
hayo hususan zile ambazo hazihitaji utaalamu.Katika hatua nyingine,
waziri Muhongo alipongeza uanzishwaji wa mgodi huo na kuahidi kwamba
Serikali itatoa ushirikiano katika hatua mbalimbali na vilevile aliwaasa
wamiliki wa mgodi huo pamoja na wananchi wanaoishi maeneo hayo kujenga
mahusiano mazuri.
Comments
Post a Comment