Mrembo afanyiwa kitu mbaya
Mrembo huyo akiongea na simu kuomba msaada.
Dar es Salaam: Hatari! Mrembo aliyetambulika kwa jina moja la Saida, amefanyiwa kitu mbaya kweupe baada ya kukombwa vitu vyote na mwanaume aliyedaiwa kutoka naye baa aliyemsukuma kutoka ndani ya Bajaj waliyopanda na kumsababishia majereha.
Tukio hilo likiwa ni mfululizo wa mengi yanayotokea maeneo ya Sinza, Afrika Sana jijini Dar, hasa nyakati za alfajiri, hivi karibuni wapita njia wa eneo hilo walisema kuwa walimuona Saida akitokea kwenye baa moja maarufu eneo hilo akiwa na mwanaume huyo asiyejulikana.
Ilidaiwa kwamba, wawili hao walionekana wakiyumba kutokana na kukesha wakipata kinywaji, walipanda Bajaj kisha ikaanza kuondoka lakini kabla hawajafika mbali ndipo wakamuona mrembo huyo akidondoka huku Bajaj ikitokomea kusikojulikana.
“Alipoinuka, alikuwa amechafuka sana na ameumia begani, damu zilikuwa zikimtoka ndipo akarudi tena hapa baa lakini wahudumu waligoma kumpokea, wakamweka nje,” alisema shuhuda mmoja.
Akizungumza kwa tabu, Saida alidai alisukumwa na mwanaume huyo aliyekuwa naye kwenye Bajaj ambaye alimpora vitu vyote, ikiwemo fedha zilizokuwa kwenye mkoba alizozipata kwenye biashara zake.
Watu mbalimbali waliopita maeneo hayo, walilaani kitendo hicho na kuitaka serikali kufuatilia baadhi ya baa zinazodaiwa kuhifadhi wahalifu na biashara za ngono kwa kuwa zinachochea vitendo kama hivyo vya wizi wa waziwazi.
“Huyu dada atakuwa ametoka kwenye hizi biashara zao, ona sasa wamemuibia kila kitu na wamemuumiza.
“Serikali ya mtaa inaonekana imeshindwa kupambana na hizi baa zinazohifadhi wahalifu na dadapoa, sasa kama inawezekana serikali kuu ilitazame hili kwa sababu uhalifu hauishi hapa,” alisema mmoja wa wapita njia aliyejitambulisha kwa jina la Saimon Lukas huku mrembo huyo akisaidiwa nauli na wenzake na kuondoka eneo hilo.
Comments
Post a Comment