Madaktari 2 na Wauguzi 4 Wasimamishwa kazi Jijini Mwanza Kwa Kukataa Kumzalisha Mjamzito Ambaye Alijifungua Mapacha Wawili Chooni Wakafariki
Mkuu
wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Baraka Konisaga, amemwamuru
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Adam Mgoyi kuwasimamisha kazi madaktari
wawili na wauguzi wanne katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana iliyopo
Kata ya Butimba kwa kushindwa kumuhudumia mama mjamzito aliyefikishwa
hospitalini hapo na kusababisha kujifungua watoto mapacha na baadaye
kufariki.
Hatua
hiyo imesababishwa na tukio la mgonjwa Suzana John (27) mkazi wa Kata
ya Mkolani kufikishwa na ndugu zake katika Hospitali hiyo, aliyekuwa
mjamzito na kupokelewa na Dk Norin Magesa na Muuguzi, Janet Foya
waliokuwa zamu ya usiku siku ya Machi Mosi, mwaka huu majira ya saa 4:00
usiku na kushindwa kumuhudumia zaidi ya kutoa lugha isiyoridhisha,
pamoja na uzembe.
Akielezea tukio hilo, mwanamke huyo (
Suzan John ) alidai kuwa alianza kusikia uchungu
na kuomba msaada kutoka kwa madaktari na wahudumu wa afya waliokuwa
hospitalini hapo bila mafanikio.
“Nilifika nikiwa hoi, nikawaambia muda wangu tayari lakini hawakunisaidia zaidi ya kunitolea maneno machafu.
"Wakati muda ukizidi kwenda huku nikiwa sipewi huduma yoyote, nilihisi kubanwa haja ndogo hivyo nikaamua kwenda chooni .
Kule chooni mambo yakabadilika ghafla, mtoto wa kwanza akawa keshaanza kutoka.Bahati nzuri mle chooni kulikuwa na beseni
"Nililichukua
lile beseni kwa ajili ya kuwaweka watoto huku niwakaita manesi.Manesi
hao walikuja wakanichungulia halafu wakarudi. Akaja Nesi mmoja
mwanafunzi, akakata kitovu
akawaweka kwenye nguo, wakawa wamefariki,” Bi. Suzan alieleza kwa
uchungu huku akilia.
Baada
ya mapacha hao kufariki, ndugu wa mwanamke huyo pamoja na wagonjwa
wengine walioshuhudia mkasa huo walipandwa na hasira huku wakitaka
kuwapiga wauguzi hao.
Taarifa
za vurugu hizo zilimfikia DC Konisaga ambaye alifika hospitalini hapo
na kukutana kwa dharula na Mkurugenzi wa Jiji, Adamu Mgoyi, baadhi ya
wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Nyamagana, Kaimu Mganga
Mkuu Mkoa, Uongozi wa Hospitali na baadhi ya ndugu wa mgonjwa Suzana
John aliyejifungua watoto mapach.
Katika
kikao hicho cha dharura, walipokea maelezo ya pande mbili, kutoka kwa
wauguzi na familia ya mgonjwa Suzana, na kupitia taarifa zilizokuwa
zimeandikwa na Madaktari wawili waliomuona mgonjwa huyo, ndipo DC
Konisaga akamuagiza Mkurugenzi Mgoyi na Kaimu Mganga Mkuu kuwasimamisha
kazi madaktari wawili na wauguzi wanne ili kupisha uchunguzi wa
kitaalamu juu ya tukio hilo.
Konisaga
aliwataja wanaotakiwa kusimamishwa kazi kuwa ni Dk Magesa na muuguzi
Foya waliompokea mgonjwa wakiwa zamu ya usiku wa Machi Mosi, mwaka huu
na kushindwa kumpatia huduma zaidi ya kumtolea lugha chafu na uzembe
huku wakishindwa kutoa maelezo wakati wa kukabidhi majukumu kwa
madaktari na wauguzi walioingia zamu ya asubuhi ya Machi 2, mwaka huu.
DC
Konisaga pia alieleza kuwa pamoja na kuingia kwa madaktari na wauguzi
wa zamu ya asubuhi ya Machi 2, bado hawakumjali na kumhudumia mgonjwa
huyo huku baadhi wakitoa lugha zisizo za faraja kwa ndugu wa mgonjwa.
Hata
alipozidiwa na kupewa taarifa na ndugu wa mgonjwa huyo, hawakufika na
mara kadhaa walikuwa wakifika na kutoka bila kumudumia pamoja na
kumsikiliza akilalamika.
Aliwataja
wengine wanaotakiwa kusimamishwa kazi mara moja ni Dk Emiliana Mvungi,
wauguzi ni Maria Mkankule, Suzana Sindano na Bibiana Moshi ambao
walikuwa zamu na kutomhudumia mgonjwa ambaye alijifungua katika
mazingira hatarishi akiwa Hospitalini hapo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo amemwagiza Kaimu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Rweyendela Onesmo ambaye ni Mganga
Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Sekou -Toure kupewa maelezo ya
kina kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Nangi William na
Mganga Mkuu wa Jiji, Dk John Andrew juu ya kushindwa kuchukua hatua
pamoja na kupewa taarifa hizo.
Comments
Post a Comment