Kiwanda Bubu Cha Kutengeneza Pafyumu Feki Chakamatwa Dar es Salaam
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
wamekamata kiwanda bubu kinachotengeneza pafyumu bandia kilichopo eneo
Tuangoma, mtaa wa Goroka Wilala ya Temeke.
Kukamatwa kwa kiwanda hicho
kinachotengeneza pafyumu aina ya SAME, kunatokana na TFDA kupata
taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kuna shehena kubwa ya pafumu hizo
katika duka moja la vipodozi lililopo Sinza kwa Remmy wilaya ya
Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hiiti Sillo alisema TFDA kanda ya
mashariki baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa kiwanda hicho kutoka kwa
wasamaria wema, walifanya ukaguzi katika duka hilo la vipodozi na
kukamata chupa 5,350 za pafyumu aina ya SAME zenye thamani ya Sh 107
milioni.
“Februari 23,mwaka huu tulifanya ukaguzi
katika duka hilo lililopo Sinza kwa Remmy na kukuta pafyumu 5,350
ambazo zinauzwa Sh 20,000 kwa chupa moja ya pafyumu na pia tuligundua
kuwa duka na pafyumu hizo zilikuwa hazijasajiliwa wala hazina kibali
kutoka TFDA”Alisema Sillo.
Alisema, awali maelezo aliyowasilisha
na mmiliki wa duka hilo katika ofisi za TFDA kanda ya mashariki
yalionyesha kuwa shehena hiyo ya pafyume iliingizwa nchini Desemba 27,
mwaka jana kutoka nchi ya Uturuki kupitia uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere, lakini tulivyofanya uchunguzi tulibaini kuwa
zinatengeneza hapa nchini.
“Kufuatia kukamatwa kwa shehena hii ya
pafyumu ambayo ni sawa na katoni 83, tuliendelea kufanya uchunguzi
ambapo tuliambiwa kuwa zinatengenezwa hapa nchini na sio
Uturuki”aliongeza.
Comments
Post a Comment