Hoteli ya kigogo NSSF yazua gumzo
Meneja wa Miradi Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Injinia John Msemo.
Stori: Makongoro Oging’ na Issa Mnally, UWAZIDAR ES SALAAM: Meneja wa Miradi Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Injinia John Msemo anadaiwa kujenga hoteli ya kisasa yenye ghorofa tano, Makumbusho jijini Dar huku baadhi ya watu wakisema kuwa, kama mtumishi wa serikali hatakiwi kumiliki mali hiyo, Uwazi limechimba.
Baadhi ya wananchi, wakiwemo majirani wa hoteli hiyo waliliambia gazeti hili kwamba, maadili ya watumishi wa serikali hayataki mtumishi wa umma kumiliki mali zenye thamani kubwa kama hoteli hiyo ambayo wao wanaikadiria kujengwa kwa mabilioni ya shilingi.
SHUHUDA
“Hii ni hoteli ya Msemo. Inaitwa Safina. Ina ghorofa tano. Huyu jamaa ni bosi pale NSSF, mimi sijui ni bosi wa nini lakini kwa mali kubwa kama hii sidhani kama ni halali yeye kumiliki.
Muonekano wa hoteli hiyo inayomilikiwa na Injinia John Msemo.
“Hebu nyie Gazeti la Uwazi jaribuni kuchimbua ukweli au uhalali wa
jamaa kumiliki mjengo huu. Najua mnaweza sana kwani ndiyo kazi yenu,”
alisema mkazi mmoja wa eneo hilo huku akiomba kusitiriwa jina.Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamesema kwamba, wao shaka yao kubwa ni kwamba isijekuwa Msemo ameweza kujenga hoteli hiyo kwa kutumia pesa ambazo si halali kwake kuwa nazo hivyo kutaka mamlaka husika kuchunguza kama si jipu.
UWAZI KWA MWENYEKITI WA MTAA
Kufuatia madai hayo, Uwazi lilifunga safari hadi kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makumbusho, Philip Komanya ambaye alikiri kuwa, hoteli hiyo ni ya Msemo lakini hajui alivyoijenga mpaka kufikia hatua hiyo.
“Ni kweli hilo jengo ni la Msemo. Lakini mimi kama mwenyekiti nimelijua hilo tu. Sasa amejenga kwa kutumia pesa aliyoitoa wapi si jukumu langu kujua na wala sina sababu ya kujua,” alisema Komanya.
UWAZI LAPIGA HODI NSSF
Baada ya kumalizana na mwenyekiti huyo, Uwazi lilimuibukia Msemo osifini kwake ambako ni Makao Makuu ya NSSF Tanzania yaliyopo Jengo la Benjamin Mkapa, Posta Dar na kuonana naye.
LENGO LA KUMTAFUTA MSEMO
Uwazi lilimfuata Msemo kwa lengo la kutaka kujua kama gazeti, hoteli hiyo ni yake kweli na uhalali wake ili aweze kuwatoa hofu wananchi.
HUYU HAPA
“Kweli ile hoteli ni yangu, mjengo ni wangu. Unajua ndugu waandishi, wananchi wanakuwa na hofu ya bure. Mimi nilichukua mkopo benki na utaalamu wangu. Ndiyo maana niliweza kujenga ile hoteli.
“Kwa kawaida benki kuna mikopo mikubwa na mikopo midogo na katika jengo lile pia kuna utaalamu wangu, Isitoshe baba yangu pia ni mfanyabiashara na hajawahi kufanya ulanguzi. Kwa ujumla ujenzi wa ghorofa lile ni halali na wala siyo jipu nitumbuliwe, hivyo kama kuna watu wana hofu kuwa kuna fedha zilizochotwa NSSF, niwaambie haiwezekani, utazichotaje?
“Mtu anaweza kufanya kitu kizuri baadaye kikazalisha maswali mengi lakini akipata ufafanuzi kwamba inawezekana mtu huyu ana ubia au utaalamu wa kufanya kitu hicho akapata jibu zuri pale brain (akili) yangu imetumika na ile mali ni kama ya familia.
“Mimi mchango wangu mkubwa katika jengo lile nina asilimia 25 na mchango wangu mkubwa ni wa ufundi na usimamizi na ukijumlisha pengine ingeweza kuzidi hiyo na asilimia 70 ni mkopo (hakuutaja ni kiasi gani), uliokamilisha mradi ule wa jengo.
Rais John Magufuli.
“Sasa mtu mwingine ambaye hajui hilo anaweza kusema atakavyo kama hao
waliowaambia hayo; ukweli siwezi kubandika tangazo kwamba jamani
asilimia 70 ya jengo hili ni mkopo.“Hata hivyo, sioni kama ni kosa au dhambi kwa mfanyakazi wa umma kuwa na mali ama kuwa tajiri bali inategemeana na jinsi ulivyoipata.
“Mimi lile jengo lina vielelezo vyote vya mkopo na kama ningejua kuwa mnakuja kuniuliza kuhusu ghorofa lile ningekuja na vielelezo vyote ili mhakikishe. Kila kitu kiko wazi na hakuna wizi uliotumika wa kitu chochote katika kujenga,” alisema Msemo.
Aidha, Msemo aliwataka waandishi kuwatoa hofu wananchi hao ambao wanadhani kuwa jengo hilo ni jipu kwa hiyo anahitajika kutumbuliwa.
Akijibu madai kuwa huwenda vifaa vya ujenzi wa jengo hilo vimepatikana kwa njia ambazo si halali, Msemo alisema anayesema hivyo ni mwendawazimu kwa sababu vifaa vyote alivyotumia ni halali na vimepatikana kihalali.
Comments
Post a Comment