Hirizi ya Jambazi Yazua Balaa
Hirizi ya jambazi huyo ikiwa shingoni.
WAANDISHI WETU, AMANI
Uvamizi wa majambazi kwenye
Benki ya Access, Tawi la Mbagala Rangi Tatu wilayani Temeke jijini Dar,
Ijumaa iliyopita umeibua mapya baada ya jambazi mmoja kukutwa na hirizi
shingoni, Amani lina mlolongo wa mambo yote.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja kutoka ndani
ya Jeshi la Polisi, Mkoa wa Temeke, jambazi huyo aliyekutwa na hirizi
ni yule aliyesimama na bunduki mbili barabarani akifyatua risasi juu ili
kuzuia magari yanayotoka Posta na Kariakoo yasipite eneo hilo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, Kamishna Simon Siro.
SIKIA SIMULIZI HII
“Hii kazi ngumu sana! Yule jambazi
aliyeshika bunduki mbili na kusimama barabarani, tulipompiga risasi
tulimkuta ana hirizi shingoni!
Lakini mbaya zaidi ni kwamba, ile hirizi ilikuwa kama inahema.
“Lakini cha ajabu sasa, baada ya
kuonekana imetulia, yule jambazi naye akatulia, akawa ameshakata roho.
Huu ujambazi wa kupewa ujasiri na hirizi naona unashika kasi. Majambazi
wengi tukiwaua au kuwakamata tunawakuta na hirizi. Hirizi si kitu mbele
ya risasi bwana,” alisema mtoa habari huyo.
Alisema hirizi hiyo nyeusi ilikuwa
imeshonwa kwa uzi mnene na askari walipoiona, waliduwaa kwa vile jambazi
huyo alionekana kujiamini sana alipokuwa ameshika bunduki barabarani
kiasi cha kuonekana tishio.
“Huenda hirizi ilimsaidia kwa namna moja
au nyingine maana lazima alishanusurika wakati fulani nyuma kwa hiyo
alijua ni ile hirizi.
Lakini pia yule bwana baada ya kupigwa risasi alionekana kubadilika rangi na kuwa mweusi sana,” alisema mnyetishaji huyo.
MAJAMBAZI WOTE WALIKUWA NA HIRIZI?
Simulizi nyingine kutoka kwa shuhuda
mmoja wa tukio hilo ilisema kuwa, wakati majambazi hao wakianza kutimka
kwa kutumia pikipiki zao, mmoja alisikika akiwasisitiza wenzake
kuhakikisha hakuna anayevua hirizi wala kuruhusu ikatike.
“Nahisi wale majambazi wote walikuwa
wana hirizi. Walipokuwa wakiondoka, mmoja alikuwa akiongea kama mchezaji
uwanjani, akiwaambia wenzake kwamba wahakikishe hirizi zao hazikatiki
wala hazidondoki,” kilisema chanzo hicho.
MADAI YA KISHIRIKINA
Kumekuwa na madai mbalimbali kutoka kwa
polisi kwamba sehemu kubwa ya majambazi huenda kwa waganga wa kienyeji
‘sangoma’ kwa lengo la kujiganga kabla hawajaenda eneo la tukio kufanya
ujambazi. Inasemekana kwamba waganga hao huwapa hirizi na kuwachanja
chale kwa madai kwamba hawatauawa au risasi hazitaingia miilini mwao
licha ya kwamba inapotokea hali ya kujibishana kwa risasi, polisi
wamekuwa washindi mara zote.
RPC ATOA ONYO
Akizungumza na Amani juzi, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Andrew Satta aliwaonya watu kuachana na
shughuli za ujambazi na kwenda kwa waganga kupewa hirizi kwani risasi
haina cha hirizi.
Pia alisema jeshi lake limejiimarisha
zaidi ili kupambana na uhalifu hivyo akawataka wahalifu wote
kujisalimisha wenyewe polisi kabla hawajakutwa na mkono wa polisi ambao
bado upo kuwasaka.
“Hayo mambo ya hirizi sijui nini! Mimi
naona wanapoteza muda bure. Jeshi limejipanga vizuri, litawamaliza wote,
kwani tuko mitaani kila kukicha,” alisema Kamanda Satta.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga
WAZIRI ANENA MAZITO
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles
Kitwanga aliwataka majambazi wote kujisalimisha kwani kwa oparesheni
iliyoanza kwa nchi nzima toka Ijumaa iliyopita, hakuna atakayesalimika.
VIGOGO WATAJWA KUHUSIKA
Wakati hali iko hivyo kwa jambazi huyo,
kuna madai kwamba, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa nchini ‘vigogo’
ndiyo wamekuwa wakifadhili kwa pesa makundi ya kigaidi ili kusababisha
mauaji katika jamii.
Hilo
limekuja baada ya tukio la Jumatatu iliyopita jijini Arusha ambapo,
askari waliwaua watu watatu waliokutwa na silaha nzito za kivita ndani
kama vile AK-47 (angalia picha ukurasa wa mbele) ambayo hutumika hata
vitani.
Baadhi ya watu walioshuhudia mapigano ya
askari polisi wa Arusha na watu hao, walishangaa kuona raia wanamiliki
silaha za kivita mitaani.
“Haiwezekani watu wamiliki silaha za
vitani hivihivi tu. Lazima baadhi ya matajiri wanatoa pesa nyingi kwa
ajili ya kuviimarisha hivi vikundi nchini, iko siku moja huko mbele
watafanya balaa zito,” alisema Fadhili Moreno, mkazi wa Njiro jijini
Arusha.
Comments
Post a Comment