BREAKING NEEWWSS:RAIS MAGUFULI ATUMBUA JIPU TANESCO
Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Rais
wa awamu ya tano, Dk. John Pombe Magufuli anayesifika kwa utumbuaji wa
majipu, safari hii ameifanya kazi hiyo kimyakimya, baada ya kuivunja
Bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) iliyokuwa
ikiongozwa na Dk. Mighanda Manyahi, Risasi Mchanganyiko linathibitisha.
Kwa
mujibu wa chanzo cha kuaminika, bodi hiyo iliyokuwa na wajumbe wanane,
ilivunjwa Machi 3, mwaka huu katika barua zilizosainiwa na Kaimu Katibu
Mkuu Kiongozi Mhandishi Mussa Ibrahim Iyombe na kusababisha kuongezeka
kwa idadi ya bodi za mashirika mbalimbali ya serikali zilizovunjwa.
Bodi
hiyo ya wakurugenzi iliyovunjwa, licha ya mwenyekiti wake Dk. Manyahi
ilikuwa na wajumbe ambao ni Dk. Haji Semboja (Makamu Mwenyekiti), Kissa
Kilindu, Juma Mkobya, Shaaban Kayungilo, Dk. Mutesigwa Maingu, Boniface
Muhegi, Felix Kibodya na Nyamajeje Weggoro.
Mmoja
wa wajumbe wa bodi hiyo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la
kutotajwa jina lake, alisema ni kweli wamepewa barua za kutenguliwa kwa
uteuzi wao, lakini anaamini Rais Magufuli hakupewa taarifa sahihi
zilizosababisha kuchukua uamuzi huo.
“Rais
anafanya kazi kwa kupewa information (maelezo), lakini nina wasiwasi
baadhi ya wanaomsaidia huwa hawampi taarifa sahihi, bodi yetu haikuwa na
sababu zozote za kuvunjwa, lakini hatuna cha kusema kwa sababu
ameshachukua uamuzi na hakuna wa kuutengua,” alisema mjumbe huyo.
Gazeti
hili liliwasiliana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ili kujua sababu
za kuvunjwa kwa bodi hiyo na endapo yapo maagizo ya kuchukuliwa kwa
hatua zaidi dhidi ya wajumbe wa bodi hiyo.
Grayson
Msigwa ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu,
alikiri kuchukuliwa kwa hatua hiyo, lakini akalitaka gazeti hili
kuwasiliana na Tanesco kwa maelezo mengine yoyote ya ziada.
Risasi
Mchanganyiko liliwasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme
(Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba kuhusu suala hilo, ambaye alikiri
kuvunjwa kwa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo.
“Ni kweli bodi imevunjwa na jambo hili mbona limezungumzwa hata na
Waziri (wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo), limetokea siku
kadhaa zilizopita,” alijibu kwa kifupi mtendaji huyo.
Baadhi
ya mashirika ya umma ambayo bodi zake zimevunjwa na rais wa awamu ya
tano tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana ni Mamlaka ya Bandari
(TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
Comments
Post a Comment