Benki Kuu ya Tanzania yawaka moto!
Jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Najuwa wajuwa, Lakini mimi nakujuza zaidi
ASUBUHI ya Julai 5,
1984, wakazi wa Dar es Salaam waliamka kwa mshangao baada ya kusikia na
kuliona jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) likiwa linaungua kwa moto
uliokuwa umesambaza moshi mkubwa na mzito juu ya anga la mji huo ulio
ufukweni mwa Bahari ya Hindi.
Tukio hilo lilitokea kiasi cha miaka 32
iliyopita, wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo, kama
kawaida, Watanzania waliokuwa na kazi na ambao hawakuwa na kazi,
walifurika maeneo jirani ya jengo hilo ambalo ndilo ‘mama wa fedha’ za
nchi hii na kushuhudia likiwaka moto huku magari kibao ya zimamoto na
wafanyakazi wake wakihangaika kuudhibiti.
Kama kawaida pia, majeshi ya usalama
yalikuwa yamefurika eneo hilo ili kuhakikisha hapatokei purukushani
yoyote wakati wa kupambana na janga hilo.
Kwa ufahamisho tu ni kwamba jengo
lililoungua ni lile ‘orijino’, yaani jengo la mwanzo kabisa la benki
hiyo lililofunguliwa Julai, 1969 na Mwalimu Julius Nyerere. Ujenzi wa
jengo hilo lenye ghorofa zipatazo sita – wakati huo – uligharimu Sh.
milioni 11, ambazo zilikuwa ni sawa na Dola za Marekani milioni 1.6.
Kwa mahesabu ya sasa, si rahisi kuamini
kwamba jengo kubwa kama hilo liligharimu kiasi kidogo cha pesa kama
hicho! Hata hivyo, ikumbukwe kwamba jengo hilo lilifunguliwa miaka
ipatayo 47 iliyopita.
Hata hivyo, jengo hilo ambalo liliungua
sehemu zote ‘laini’ na kubaki likiwa zima katika sehemu zote ‘ngumu’
kama vile kuta, zege na vyuma na kadhalika, lilikarabatiwa na kuanza
kutumika, japokuwa lilifanyiwa mabadiliko kadhaa kwa ndani na nje.
Habari kamili au za wazi kuhusu chanzo
cha moto huo na hasara zake, hazikutolewa wazi sana licha ya wapelelezi
kutoka Uingereza ambao walikuja kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kutoa
ripoti kwa mamlaka husika. Hata hivyo, ni dhahiri hati na kumbukumbu
mbalimbali ziliteketea katika moto huo ambapo shughuli nyingi zilikuwa
zinafanyika kwenye ‘makaratasi’.
Tofauti na taswira ya wakati huo, makao
makuu ya benki hiyo hivi sasa yamebadilika sana, kwani jengo hilo
lililoungua hivi sasa liko katikati ya majengo pacha marefu, kila moja
likiwa na ghorofa 20, ambayo yalikamilika kujengwa mwaka 2006. Matokeo
yake, majengo hayo mawili, kaskazini na kusini mwa jengo orijino,
yamelifanya kuonekana kama ‘kambilikimo’ kenye kuchekesha.
source:GPL
source:GPL
Comments
Post a Comment