Balaa Jipya Makalio ya Kichina
Stori: Hamida Hassan na Boniface Ngumije
Dar es Salaam:
Tabia ya baadhi ya wasichana hasa wa mjini kuwa na tamaa ya kuwa na
makalio makubwa na hivyo kulazimika kutumia dawa mbalimbali, imekuwa
ikishamiri kila siku licha ya serikali kupiga marufuku uingizwaji wa
dawa hizo.
Jayjay
Gazeti hili matoleo yaliyopita liliwahi
kuandika jinsi mastaa wengi Bongo wanavyotumia dawa hizo lakini
uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, kasi ya matumizi ya
dawa hizo yamekuwa yakishamiri huku waathirika wengi wakijiuguza kwa
siri baada ya kupata madhara.
Gilla.
Katika tukio jipya la hivi karibuni,
mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hamisa ambaye alidai ni mke
wa mtu alisema kuwa, alishawishiwa na rafiki yake kutumia dawa hizo ili
naye awe na ‘zigo’ lakini ameanza kuona zinamletea matatizo.
“Nimekuwa nikisikia kuwa dawa hizi zina
madhara lakini kuna rafiki yangu mmoja ambaye aliwahi kutumia na yuko
poa ndiye aliyenipeleka kwenye duka moja lililopo Kijitonyama na
kununua. Awali sikuona tatizo lakini kadiri siku zinavyokwenda nahisi
maumivu f’lani, najuta kuzitumia dawa hizi kwa kweli,” alisema mwanamke
huyo.
Kidoa.
OFM mtaani
Baada ya kupata malalamiko hayo,
waandishi wetu walifanya uchunguzi na kubaini kuwa dawa hizo zinauzwa
kwa siri sana tangu serikali icharuke na kutoa tamko la kuwashughulikia
wale wanaoziuza.
Katika uchunguzi huo, yamegundulika
maduka kibao mitaa ya Kariakoo, Kinondoni na Mwenge jijini Dar ambapo
wauzaji huziuza dawa hizo ‘kimagutu’ kana kwamba wanauza madawa ya
kulevya au bangi.
Mwandishi wetu alifika kwenye duka moja
lililopo Msimbazi baada ya kulengeshwa kuwa dawa hizo zinauzwa hapo,
muuzaji alipoulizwa uwepo wa dawa hizo, kwanza alikataa lakini baadaye
alikubali huku akionekana ni mwenye wasiwasi.
Afisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania, Gaudensia Simwanza.
Dukani kwa Maimartha
Ilidaiwa kuwa, asilimia kubwa ya mastaa
wanaotumia dawa hizo wanazinunua kwenye duka la Mtangazaji wa Azam TV,
Maimartha Jesse na ili kujiridhisha OFM walitinga kwake na kumkuta dada
ambaye jina lake halikufahamika ambaye alisema dawa hizo hawana dukani
hapo ila mwandishi akitaka anaweza kutafutiwa.
Baada ya mwandishi kujifanya anazihitaji
kwa udi na uvumba, mdada huyo alimpigia simu mtu ambaye haikujulikana
ni nani na ndani ya muda mfupi akawa amezileta dawa hizo ambazo zipo
kwenye mfumo wa losheni.
Alipopigiwa simu Maimartha na kabanwa
juu ya kudaiwa kuwaharibu wanawake wenzake kwa kuwauzia dawa hizo,
aliruka kimanga na kusema:
“Mimi sitaki kuzungumzia kuwa nauza au
siuzi kwa sababu naiheshimu sana serikali na nafuata maelekezo
wanayotoa, lakini ninavyojua dawa hizo zinauzwa kwa siri sana na
wanaotaka kuuziwa ni wengi.”
Aidha, wasanii wengi hawa wa kike
wamekuwa wakidaiwa kutumia dawa hizo huku mastaa wa kizazi cha sasa kama
vile Gift Stanford Gigy, Glasnost Kalinga ‘Gilla’, Asha Salumu ‘Kidoa’,
Janet Jackson ‘Jayjay’ na wengine wakidaiwa kuwa maumbile waliyonayo
siyo ‘orijino’.
Ijumaa lilipata fursa
ya kuzungumza na wadada hao ambao sasa ni habari ya mjini kutokana na
maumbo yao ambapo kila mmoja alifunguka kivyake:
Gigy: Kusema ukweli sijawahi kutumia dawa hizo, nazisikia tu. Umbo langu ni orijino na wala hayo masponji zivai, hata nikivua sasa.
Kidoa: Shepu yangu ni ya kuzaliwa nayo, najua dawa za Kichina ni shida hivyo siwezi kuthubutu kuzitumia.
Gilla: Mh! Wapo wanaoniambia natumia dawa hizo, kiukweli nimezaliwa hivyo na hivi sasa nimepungua hapo mwanzo si ndo mgenishangaa.
TFDA wanasemaje?
Baada ya OFM kufanya uchunguzi wake,
waandishi wetu walizungumza na Afisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na
Dawa Tanzania, Gaudensia Simwanza ambaye alisema wanapambana kuhakikisha
dawa hizo haziingii nchini na atakayekamatwa cha moto atakiona.
“Lakini kwa kuongeza tu ni kwamba kuhusu
watumiaji wanaopata madhara kwa matumizi ya dawa hizo wengi unakuta
hatuna taarifa nao kwa sababu huwa hawaji kwetu moja kwa moja,
wanakwenda mahospitali na sehemu nyingine kupata tiba, ila tunapopata
taarifa kama hizi tunafuatilia na kuzitendea kazi,” alisema Simwanza.
Aidha, dokta mmoja anayefanya kazi
katika wizara ya afya ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini
alisema kuwa, sasa hivi wako makini kuhakikisha uuzwaji holela wa dawa
zenye madhara kwa watumiaji unakoma.
“Unajua hiki siyo kipindi cha mchezo,
TFDA wanafanya kazi yao lakini wizara ya afya nayo inapambana, kikubwa
ni tahadhari kwa watumiaji wa dawa hizo, wajue kwamba kuna madhara
makubwa ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yao hivyo waache,” alisema
dokta huyo.
Comments
Post a Comment