Yanga Jeuri, Simba Kiburi
Wachezaji wa Yanga, Ngoma (kushoto) na Kamusoko (kulia).
Waandishi Wetu,Dar es Salaam
DAWA ya Jeuri ni Kiburi, Yanga na Simba leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa zinapambana katika mechi ya Ligi Kuu Bara huku nyuma yake kukiwa na vita kubwa.
Awali, Simba ilionekana haitafanya lolote katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini muda mfupi baada ya Jackson Mayanja kupewa kazi ya kocha msaidizi akiichukua timu kutoka kwa Dylan Kerr, raia wa Uingereza, mambo yamebadilika.
Chini ya Mayanja raia wa Uganda aliyewahi kuinoa Bunamwaya ya nchini kwake, Simba imefanikiwa kushinda mechi sita mfululizo za ligi kuu na moja ya Kombe la FA dhidi ya Burkina Faso ya Morogoro.
Wachezaji wa Ibrahimu Ajibu na Juuko Murshid (kulia) wakishangilia.
YANGA JEURIJeuri ya Yanga ipo zaidi katika fedha, kwanza ilikodi ndege kutoka Dar es Salaam hadi Cuepipe, Mauritius kucheza na Cercle de Joachim katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilishinda bao 1-0.
Ndege hiyohiyo ikaipeleka Yanga Zanzibar Jumapili iliyopita ambako iliweka kambi ya siku sita na jioni ikarejea Dar es Salaam kwa ndege maalum huku mabosi wake wakionyesha jeuri ya fedha wakati Simba iliyoweka kambi Morogoro, ikitumia usafiri wa basi kurejea Dar es Salaam.
Tofauti na Simba ambayo kidogo imelegeza masharti ambapo kocha wake Mayanja amekuwa akizungumzia mchezo huo katika hali ya kawaida, ndani ya kambi ya Yanga hali ni tofauti na kila mtu yupo kimya.
Wachezaji wa Simba,(kutoka kushoto), Hassan Isihaka,(wa pili kushoto) Haji Ugando,Mwinyi Kazimoto,Ibrahimu Ajib wakimpongeza,Hamis Kiiza(kushoto) baada ya kufunga moja ya mabao dhidi ya timu ya Mgambo Shooting mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana. Simba ilishinda mabao 5-1.(Picha na Yusuf Badi)
Yanga ilitarajiwa kurejea Dar es Salaam jana Ijumaa jioni kutoka kambini Pemba ilipokwenda tangu Jumapili iliyopita ikitokea Mauritius ilipocheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim.
Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ameweka kiburi cha kutozungumzia lolote kuhusu mechi hiyo lakini gazeti hili lilishuhudia mazoezi yote ya timu hiyo kwa siku zote kambini.
Kazi kubwa aliyofanya Pluijm, raia wa Uholanzi, ni kuhakikisha anausuka vizuri ukuta wake hasa mabeki wa kati Vincent Bossou na Mbuyu Twite ili wacheze kwa uelewano katikati.
Wachezaji wa Yanga Niyonzima na Tambwe wakishangilia.
Hatua hiyo imekuja kutokana na kutokuwepo kwa Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani. Cannavaro ametoka katika majeraha na
Yondani anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mechi ya
Yanga na Coastal Union.“Ni mechi ya kawaida tu hii, sizungumzi chochote kuhusu timu yangu ila nitaongea baada ya mechi hii tafadhali,” alisema kwa kifupi Pluijm.
Inaonekana wazi jeuri ya Pluijm inatokana na uwezo wa washambuliaji wake Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao kwa pamoja wamefunga mabao 24 kati ya 42 yaliyofungwa na Yanga hadi sasa.
Pia Pluijm ana kikosi kipana kwani hata kama Ngoma na Tambwe watapata matatizo, benchi wapo Paul Nonga na Malimi Busungu wenye uwezo mkubwa katika kushambulia.
Tofauti na Simba, katika mechi sita za mwisho za ligi kuu, Yanga imeshinda nne tu, imetoka sare moja na kufungwa moja. Katika mechi hizo, Yanga imefunga mabao 15 na kufungwa matatu.
Licha ya Yanga kuonyesha jeuri ya fedha kwa kutumia usafiri wa ndege kutoka Pemba hadi Dar es Salaam jana jioni, Simba wala haikuweka makeke kwani ilitumia usafiri wa basi lake kutoka kambini Morogoro hadi Dar es Salaam jana tayari kwa mechi.
Simba imeonyesha kiburi zaidi kwa kushinda mechi saba mfululizo huku ikifunga mabao 18 na kufungwa mawili tu. Kati ya mechi hizo, sita ni za ligi kuu ambapo ushindi wake umeifanya ifikishe pointi 45 na kukaa kileleni mwa ligi hiyo.
Chini ya Mayanja Simba imezifunga Mtibwa Sugar bao 1-0, JKT Ruvu (2-0), Burkina Faso (3-0), African Sports (4-0), Mgambo JKT (5-1), Kagera Sugar (1-0) na Stand United mabao 2-1.
Simba iliyoweka kambi Morogoro kwa wiki nzima, ilitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana usiku tayari kwa mchezo huo wa leo.
Akizungumza na Championi Jumamosi kutoka Morogoro, Mayanja alisema: “Hii ni mechi ngumu kwani Yanga wana kikosi imara, mimi nilichofanya ni kuiandaa timu icheze soka safi lenye manufaa, siwezi kukuhakikishia kitu kwani mimi siyo Mungu.
“Wengi wanadhani (Amissi) Tambwe ndiye mtu hatari Yanga, hapana kabisa kwani katika mechi kama hizi unaweza kumdharau mchezaji halafu akaja kuwahukumu msivyotegemea.”
Nguvu kubwa ya Simba leo itabaki kwa straika wake Hamis Kiiza anayeongoza kwa ufungaji katika ligi akiwa na mabao 16 ambaye atashirikiana na Ibrahim Ajib wakati katikati watakuwepo Jonas Mkude na Justice Majabvi.
USIENDE KUFANYA FUJO TAIFA
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na vikosi vingine vya usalama, limeimarisha usalama Uwanja wa Taifa na hakuna mtu au kundi la watu litakaloweza kuvunja amani.
Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, milango ya Uwanja wa Taifa itafunguliwa kuanzia saa 5 kamili asubuhi, huku barabara ya Chang’ombe ikifungwa kuanzia asubuhi.
Ni magari maalum tu yenye stika maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia eneo la uwanjani kupitia Barabara ya Mandela na Uwanja wa Uhuru.
“Vitu kama silaha, vilevi, mabegi na vitu vyenye ncha havitaruhusiwa kuingia ndani ya uwanja,” alisema Kizuguto.
Kizuguto alisema mwamuzi Jonesia Rukyaa wa Kagera yupo tayari kwa pambano hilo akisaidiwa na Josephat Bulali (Tanga), Samwel Mpenzu (Arusha) huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Elly Sasii (Dar) na Kamisaa Khalid Bitebo wa Mwanza.
Stori: Suleiman Hassan, Zanzibar na Nicodemus Jonas, Dar
Comments
Post a Comment