MAWAZIRI WAPEWA MWISHO LEO KUJAZA TAMKO LA MALI NA MADENI, HATI YA UADILIFU
Waziri
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majliwa Majaliwa (kulia) akitoa taarifa
mbele ya Waandishi wa Habari kuhusiana na misingi ya Fomu za Maadili ya
Utumishi wa Umma kwa Viongozi wa Umma pamoja na kujaza fomu za tamko za
rasilimali walizo nazo na za madeni waliyonayo sambamba na kutaja majina
ya baadhi ya Mawaziri na Manaibu Waziri ambao bado mpaka sasa
hawajarudisha fomu hizo kwa Kamishna. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah
Kairuki.
Baadhi
ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo pichani) wakati akitoa taarifa
kuhusiana na misingi ya Fomu za Maadili ya Utumishi wa Umma kwa Viongozi
wa Umma pamoja na kujaza fomu za tamko za rasilimali walizo nazo na za
madeni waliyonayo sambamba na kutaja majina ya baadhi ya Mawaziri na
Manaibu Waziri ambao bado mpaka sasa hawajarudisha fomu hizo kwa
Kamishna.(PICHA ZOTE NA EBENEDICT LIWENGA-MAELEZO)
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema
mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni wawe wamejaza
fomu hizo na kuzirejesha katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma Dar es Salaam ifikapo leo saa 12.00 jioni (Ijumaa,
Februari 26, 2016).
Agizo
hilo la Rais limetolewa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mbele ya
waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisini kwake, Magogoni
jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa
Rais ameelekeza mawaziri ambao hawajajaza tamko la rasilmali au hati ya
ahadi ya uadilifu wafanye hivyo na kuzirejesha kabla saa 12 jioni na
Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa
mwenyewe kwenye nafasi yake,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu amesema wakati akifungua mafunzo ya Mawaziri na Naibu Waziri
kuhusu Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Utekelezaji wa Ahadi
ya Uadilifu yaliyofanyika Ikulu jana (Alhamisi, Februari 25, 2016)
alikabidhiwa majina ya Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao hawajawasilisha
Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili.
Amewataja
mawaziri wanaotakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali pamoja na
hati ya ahadi ya uadilifu kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw.
Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi (OMR – Muungano na Mazingira), Bw.
January Makamba. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine
Mahiga ambaye anatakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi
wa umma na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce
Ndalichako ambaye anatakiwa kutoa tamko la rasilmali na madeni.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira), Bw. Luhaga Mpina
anatakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilmali na madeni pamoja na hati
ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.
Comments
Post a Comment