MAMBO YAWA MAGUMU KWA WAZIRI WA ZAMANI WA CCM MAIGE NAE ATAJWA UFISADI NGORONGORO
Waziri wa zamani wa
Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu ya nne, Ezekiel Maige, jana
alitajwa katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro, Bernard Murunya ambaye ameshitakiwa kwa
matumizi mabaya ya ofisi.
Katika kesi hiyo, Maige
anadaiwa kulipiwa nauli ya safari ya nje na mamlaka hiyo kwa idhini ya
Murunya, ambaye sasa ni Mbunge wa Afrika Mashariki.
Shahidi wa kwanza katika
kesi hiyo, Sezari Semfukwe, alidai kuwa Murunya na aliyekuwa Mkurugenzi
wa Fedha na Utawala wa Mamlaka hiyo, Shad Kiambile, waliidhinisha
malipo ya dola 66,890. Alidai kuwa fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya
safari ya Maige na msaidizi wake aliyetajwa kwa jina la E. Muyungi na
Murunya mwenyewe.
Semfukwe, ambaye ni
Kaimu Mhasibu Mkuu wa mamlaka hiyo, alidai kuwa Murunya na Kiambile,
ndio walioidhinisha madokezo kwa ajili ya malipo hayo.
Akiongozwa na Wakili wa
Serikali Hamidu Sembano, akisaidiana na Rehema Mteta, mbele ya Hakimu wa
Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda, Semfukwe alidai kuwa
utaratibu wa maombi ya safari, unatokana na maelekezo ya mkuu wa idara
na kujaza fomu inayoonyesha anakwenda wapi na kwa muda gani.
Sambamba na hilo, alidai
kuwa aina zingine za safari zinahusisha watu wa nje ambao, si waajiriwa
wa NCAA kwa dokezo la mkuu wa idara au shirika.
Alidai kuwa alitoa hundi
ya malipo namba 309/0238 ya Septemba 9/2011, ambayo ilikuwa na dokezo
la safari kutoka kwa Murunya kwenda kwa Mkuu wa Kitengo cha Fedha. Pia
alitoa hundi ya malipo nyingine iliyokuwa ikionyesha imelipwa dola
zaMarekani 66,890 kwa kampuni ya Wakala wa Usafirishaji ya Cosmas.
Aliendelea kudai kuwa
hundi za malipo namba 310/0379 ya Oktoba 29, 2011 na ankara namba 5609
ya Septemba 7, 2011 zililipwa kwa Antelope Tours & Traveling kwa
ajili ya tiketi za Murunya, Muyungi na Maige kwa malipo ya dola za
Marekani 66,890 (zaidi ya Sh. milioni 133).
Shahidi hiyo alidai kuwa
kumbukumbu ya kitabu cha malipo ya hundi inaonyesha hundi namba 002758
na 002755 za Septemba 9, 2011 zililipwa kwa kampuni ya Cosmas
Travelling Agent na zilitiwa saini na Kiambile na Murunya.
Hata hivyo, wakati
shahidi huyo akitoa vielelezo hivyo mahakamani hapo ili vitumike kama
ushahidi, malumbano ya kisheria yaliibuka baina ya mawakili wa pande
zote.
Malumbano hayo yaliibuka
baada ya upande wa washtakiwa, ukiongozwa na wakili Amani Mirambo,
kutaka kujua ni vielelezo vingapi au vya aina gani ambavyo upande wa
mashtaka unavileta.
Hatua hiyo ilisababisha
malumbano ya kisheria hivyo kumfanya hakimu kuahirisha kesi kwa dakika
10. Baada ya muda huo, alirejea mahakamani baada ya dakika hizo na
kuwahoji.
Baada ya kuhoji pande
zote mbili, kutokana na malumbano ya kisheria, Hakimu alikatizwa na
Wakili wa Serikali Hamidu Simbano, aliyemwomba kuahirisha kesi hiyo na
kutaja tarehe nyingine ya washtakiwa kusomewa maelezo yao ya awali.
Awali, Mwendesha
Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Rehema
Mteta, aliwasomea maelezo ya awali juu ya tuhuma za matumizi mabaya ya
madaraka yaliyosababisha mamlaka hiyo kupoteza dola 66,890 (Sh.
133,780,000).
Mteta aliwataja
washitakiwa, mbali na Murunya na Kiambile, kuwa ni Meneja Utalii wa
mamlaka hiyo, Veronica Funguo na Salha Issa ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Cosmas Travelling Agentsource.thechoice
Comments
Post a Comment