JAJI MKUU WA KENYA AFURAHIA UTENDAJI WA MAHAKAMA YA TANZANIA.
Jaji
Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Willy Mutunga (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utendaji wake wa
kusikiliza na kuamua mashauri mengi yanayopelekwa mahakamani. Kushoto
ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman na Kulia ni Jaji
Kiongozi Mhe. Shaan Lila.
……………………………………………………
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Jaji
Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Willy Mutunga ameipongeza Mahakama ya Tanzania
kwa utendaji wake wa kusikiliza na kuamua mashauri mengi yaliyopelekwa
mahakamani kwa mwaka wa sheria uliopita wa 2015 na kutoa wito kwa
watendaji wa Mahakama ya Tanzania kuendelea kufanya vizuri licha ya
changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Jaji
Mkuu wa Kenya ametoa pongezi hizo mbele ya waandishi wa habari leo
jijini Dar es salaam mara baada ya kukutana na kuongea na Majaji wa
Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani Tanzania kufuatia mwaliko alioupata
wa kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yatakayofanyika
Februari 4 mwaka huu.
Mhe.
Dkt. Mutunga amesema kuwa nchi ya Kenya mpaka sasa ina mashauri
yapatayo 300,000 ambayo bado hayajaamuliwa na kuongeza kuwa asilimia 5
ya wananchi wa Kenya ndio hupeleka mashauri yao Mahakamani huku asilimia
95 iliyobaki wakitafuta ufumbuzi wa kesi zao nje ya Mahakama.
“Ni
kweli Tanzania mnafanya vizuri katika katika kusikiliza mashauri kwa
haraka, asilimia 95 ya Wakenya hutafuta ufumbuzi wa kesi zao kwa
viongozi wa kidini na Kimila kutokana na baadhi yao kukosa fedha za
kutosha za kufuatilia na kugharamia kesi zao” Amesema.
Ameongeza
kuwa Mahakama ya Kenya kwa mwaka huu 2016 imejipangia malengo ya
kuhakikisha kuwa inasuluhisha mashauri yote ndani ya mwaka mmoja ili
kuongeza ufanisi na imani kwa wananchi.
Ameeleza
kuwa Tanzania ina jambo la kujifunza kutoka Kenya kufuatia mageuzi ya
Katiba iliyoyafanya mwaka 2010 hususan kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo
na nafasi ya Mahakama kwenye Katiba Mpya ambayo Tanzania inaendelea na
mchakato wake.
Akizungumzia
mageuzi hayo ambayo tayari Kenya imeyafanya kufuatia kuwepo kwa Katiba
mpya Mhe. Mutunga amesema kuwa ni pamoja kupungua kwa madaraka ya Rais
katika kuteua Majaji, na nafasi za Majaji kutangazwa na watu kupeleka
maombi na sifa zao kujadiliwa ambapo wananchi huruhusiwa kutoa maoni kwa
Tume ya Mahakama ya Kenya kuhusu majaji hao kabla ya kuapishwa.
Aidha,
ameeleza kuwa Watanzania wana kila sababu ya kujivunia umoja na
mshikamano uliopo ambao umesababishwa na waasisi wa taifa hilo huku
akibainisha kuwa majadiliano na upatikanaji wa Katiba Mpya utafanywa na
Watanzania wenyewe kwa kuwa Watanzania ni walimu na mfano wa kuigwa
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa
upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman
akizungumzia ujio wa Jaji Mkuu wa Kenya amesema kuwa Mahakama ya
Tanzania imenufaika na ujio wake kwa kuwa iko kwenye maadhimisho ya Wiki
ya Sheria ambayo huwakutanisha wadau mbalimbali wa sharia kujadili
changamoto na mafanikio ya Sekta ya Sheria nchini.
Amesema
kuwa kufuatia ziara ya Jaji Mkuu wa Kenya Mahakama ya Tanzania
imejifunza masuala mbalimbali ambayo ni muhimu katika ufanisi wa
shughuli zake ikiwemo Maslahi ya Watumishi wa Mahakama, Jukumu la
Mahakama kutafsiri Katiba kwa kuangalia historian a uchumi pia kuazima
baadhi ya hukumu zilizotolewa nchini Kenya kama ushauri.
Aidha,
amebainisha kuwa Mahakama ya Tanzania inao wajibu wa kuendelea kuongeza
uwazi katika upatikanaji wa watendaji wake wenye nia ya kuwatumikia
wananchi na kuboresha njia za kuwapata majaji.
Comments
Post a Comment