Wakurugenzi watendaji Manispaa za Kigoma, Mpanda wasimamishwa

Simbachawene 2
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mhe. George B. Simbachawene.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mhe. George B. Simbachawene amewasimamisha kazi wakurugenzi watendaji wa manispaa za Kigoma, mkoa wa Kigoma na manispaa ya Mpanda, mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kuridhia na kutekeleza maamuzi ambayo yamesababishia serikali hasara na upotevu wa fedha.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma, Mhandisi Boniface Nyambele anakabiliwa na tuhuma ya uuzaji wa nyumba za halmashauri bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo na bila kibali cha waziri mwenye dhamana kama sheria inavyoelekeza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Ndugu Suleiman Lukanga anakabiliwa na tuhuma za ununuzi hewa wa gari la kusomba taka kwa kiasi cha shilingi milioni tisini na mbili, laki saba na elfu hamsini (92,750,000/=) na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Kakese kiasi cha shilingi milioni mia mbili, tisini na nne (294,000,000/=).
Aidha, Waziri Simbachawene ameagiza nafasi ya mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma ikaimiwe na Mhandisi Sultan Imari Ndilowa ambaye ni mkuu wa idara ya maji, manispaa ya Kigoma, nafasi ya mkurugenzi wa manispaa ya Mpanda ikaimiwe na ndugu Lauteri John Kanoni ambaye ni katibu tawala msaidizi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Katavi.

Comments

Popular posts from this blog