SABABU ZA UKAWA KUSUSIA KAMATI ZA BUNGE NA KUMGOMEA SPIKA NDUGAI



Wakati vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vikitarajiwa kuanza leo kwa uteuzi wa wajumbe, wabunge wa upinzani tayari wameanza kwa kumtikisa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, baada ya kususia uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo.
Dalili za mgawanyiko kwenye kamati hizo zilianza kuonekana juzi, baada ya wabunge hao wa Kambi ya Upinzani kufanya kikao na kuweka msimamo wa kutaka kushirikishwa kwenye uteuzi wa wajumbe.
Kambi ya Upinzani ilisema inataka kushirikishwa katika hatua hiyo ikidai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), imekuwa ikiwapangia watu wa kuongoza kamati zinazosimamia mapato ya serikali ambazo kikanuni zipo chini yao.
Aidha, jana hali ilikuwa ngumu ndani ya kambi ya CCM ambao walifanya vikao tangu asubuhi mpaka jioni kujadili kamati hizo.
SABABU ZA UPINZANI KUSUSA
Viongozi hao wa kambi ya upinzani walidai kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakipangiwa watu wa kuongoza Kamati ya Hesabu za Serikali za (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambazo kikanuni zinatakiwa kuongozwa na upinzani.
Taarifa ambazo gazeti hili ilizipata jana kutoka ndani ya ofisi ya upinzani, zilidai kuwa ofisi hiyo ilimwandikia barua Spika wa Bunge, Ndugai kutaka washirikishwe kwenye uteuzi wa wajumbe wa kamati hizo.
Hata hivyo, ombi la viongozi hao liligonga mwamba, hatua iliyosababisha wagomee uchaguzi wa wenyeviti wa kamati.
Baada ya Ofisi ya Bunge kutangaza majina ya wajumbe wa kamati, Kambi ya Upinzani Bungeni ilikutana na waandishi wa habari, lakini wakaahirisha kwa madai kuwa wamegundua kwamba orodha ya majina yaliyotoka, yana matatizo mengi zaidi.
“Tumegundua kwamba matatizo hayapo kwenye kamati ya PAC na LAAC tu, kwenye kamati nyingi kuna matatizo kwa hiyo kwa sasa viongozi wa kambi wanakutana kujadili na kuchambua taarifa iliyotolewa baadaye tutakutana na wabunge wote kisha kesho tutatoa msimamo wetu,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Mnyika.
Baada ya kauli hiyo, Mnyika aliulizwa inakuwaje wao wanaendelea na vikao wakati wenzao wa CCM wakiwa kwenye uchaguzi:
“Siwezi kujibu chochote, neno lolote nitakalosema, nitaingilia hicho kinachojadiliwa na viongozi. Wewe subiri kwanza tumalize kikao, tutoke na msimamo wa pamoja na kesho tutawaeleza msimamo wetu,” alisema Mnyika.
Awali, kabla ya kutolewa kwa majina hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, alisema kwa muda sasa wamekuwa wakichaguliwa watu wa kuongoza kamati hizo na CCM.
“Ni sawa na mtu anakupa kitu kwa mkono wa kushoto na kukunyang'anya kwa mkono wa kulia. Ndiyo maana tukataka tushirikishwe kuanzia wajumbe watakaokuwa kwenye kamati hizo,” alisema Sakaya ambaye ni Mbunge wa Kaliua mkoani Tabora.
Taarifa ambazo Nipashe ilizipata jana jioni, Kambi hiyo ilimuandikia barua nyingine Spika ikieleza juu ya msimamo wao.
Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Aprili 2013, inasema: “Wenyeviti wa Kamati za Bunge zinazosimamia matumizi ya fedha za Umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati hizo ambao wanatoka katika Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.”
Nipashe ilipomtafuta Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel, ili kutolea ufafanuzi suala hilo, alihoji: “Kanuni unazo?, Nenda kasome kanuni zinasemaje kuhusu suala la uteuzi wa wajumbe kamati. Ukishalifahamu hilo, ndiyo uniulize una tatizo gani."
Alipoulizwa hatma ya Kamati za PAC na LAAC ambazo upinzani umegoma kushiriki vikao vya uchaguzi, alisema:
“Nitalijibu kweli hilo mimi? Kama mtu amesusia kitu kula, mimi nitasema kwa nini kasusa kula? Mimi sina jibu dada yangu, sina jibu kuhusu hilo.”
Alipotakiwa kuthibitisha kama kweli upinzani wameandika barua alijibu: “Nadhani watakuwa waliandika, kama itakuwa ni kutaka kushirikishwa kupanga wajumbe, itakuwa ni kinyume cha kanuni kwa sababu mwenye mamlaka ni Spika, hakuna mtu mwingine.”
Taarifa iliyotolewa na Bunge jana ilisema vigezo vilivyotumika kuchagua wajumbe wa kamati hizo ni pamoja na idadi ya wabunge inayolingana kwa kila kamati, aina zote za wabunge na kigezo cha asilimia ya kila aina ya wabunge waliopo bungeni kwa kuzingatia pande za Muungano, jinsia na uwakilishi wa vyama.
Ilisema kigezo kingine ni matakwa ya wabunge wenyewe kwa kujaza fomu za maombi, uzoefu au ujuzi wa wabunge kuzingatia kazi na majukumu ya kamati na uzoefu wa awali kielimu na kikazi.
Wajumbe wa upinzani kamati zilizoleta mpasuko
Wabunge wa upinzani kwenye kamati ya PAC ni Naghenjwa Kaboyoka, Yosemba Komba, Tunza Malapo (Chadema) na Ali Salim Khamis (CUF).
Kwa upande wa LAAC, wabunge wa upinzani ni Rose Kamili, Conchesta Rwamlaza, Grace Kiwelu, Joseph Mkundi (Chadema) na Vedasto Ngombale, Dk Suleiman Ally Yussuf (CUF).
Wabunge `matata' wapangwa Maendeleo ya Jamii
Majina yaliyotangazwa jana yameonyesha kuwa wabunge wengi machachari, wamepangwa katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Wabunge hao ni Hussein Bashe, Dk. Charles Tizeba, Magret Sitta, Peter Serukamba, Stephen Masele, Mussa Zungu, Juma Nkamia na Lazaro Nyalandu (wote CCM). Wengine ni Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) Joseph Mbilinyi, Suzan Lyimo na Saed Kubenea (Chadema).

Comments

Popular posts from this blog