Mume amuua mke mjamzito!
Marehemu Clara Justin Munishi enzi za uhai wake.
Stori: Makongoro Oging’, UWAZI
DAR ES SALAAM:
Dunia katili! Clara Justin Munishi (30), mkazi wa Keko Mwanga, Temeke
jijini Dar amefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa na kujeruhiwa vibaya
na mumewe, Novatus Peter Kabero.
Tukio hilo la kikatili, lilitokea usiku
wa saa tano, Januari 13, 2016 nyumbani kwa wanandoa hao ambapo kwa
mujibu wa majirani, mwanamke huyo alisikika akilia na kuomba msaada kwa
muda mrefu kutokana na kushushiwa kipigo kikali na mumewe.
Mume wa marehemu Novatus Peter Kabero.
“Unajua hawa ilikuwa kama kawaida yao
kugombana, mara kwa mara mwanaume alikuwa akimpiga sana mkewe hasa
nyakati za usiku. Sasa siku hiyo hata tuliposikia Analia na kuomba
msaada, tulijua ni kama kawaida yao, kumbe mwenzetu alikuwa anauawa,”
alisema mwanamke mmoja anayeishi jirani na eneo la tukio, aliyekataa
kujitambulisha jina lake.
Habari zaidi kutoka kwa vyanzo vyetu,
zinaeleza kuwa baada ya kuzidiwa na kipigo, mwanamke huyo aliyekuwa na
ujauzito wa miezi mitatu, alidondoka na kupoteza fahamu, mumewe
akaendelea kumpiga kisha akamburuza na kumtoa nje ya uzio alikomtelekeza
na kutokomea kusikojulikana.
Waombolezaji wakiwa msibani.
“Ilibidi jirani mmoja apige simu polisi
kwa sababu siku hiyo alikuwa akilia sana tofauti na siku zote anazopigwa
na mumewe. Pia tulishindwa kwenda kuwaamulia kwa sababu mumewe ana
kawaida ya kuwatishia watu na bastola. Muda mfupi baadaye, polisi
walifika eneo la tukio, wakamchukua akiwa hajitambui na kumpeleka
Hospitali ya Temeke ambako alifariki dunia muda mfupi baadaye.
Ndugu wa marehemu aliyejitambulisha kwa
jina la Raymond Kavishe, aliliambia Uwazi kwamba wamesikitishwa sana na
kifo cha kinyama cha ndugu yao na kuliomba jeshi la polisi kumsaka
mtuhumiwa ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa Jumatano
ya wiki iliyopita kwenda kijijini kwao, Marumumlama, Wilaya ya Hai
mkoani Kilimanjaro alikozikwa Alhamisi ya Januari 21, mwaka huu.
Marehemu ameacha mtoto mmoja.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Andrew Satta alipoulizwa, alikiri kutokea
kwa tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha mauaji hayo, inadaiwa ni
mwanamke huyo kukaidi amri ya mumewe aliyemkataza kwenda kwa rafiki wa
marehemu kwa madai kwamba anamtafutia wanaume. Kamanda Satta aliongeza
kwamba mtuhumiwa anaendelea kusakwa na jeshi la polisi kwani alitoroka
baada ya kufanya mauaji hayo.
Comments
Post a Comment