DKT. KIGWANGALLA AUNDA KIKOSI KAZI KUBORESHA HUDUMA ZA MFUKO WA AFYA YA JAMII (CHF)

IMG_0652
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla.
Na Rabi Hume, Modewjiblog
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameanzisha kikosi kazi cha watu 24 ambacho kitakuwa na kazi ya kutengeneza mpango mkakati wa kuwezesha kuboresha Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).Katika taarifa ambayo imetolewa na Dkt. Kigwangala imeeleza kuwa kazi ya kuanzisha kikosi kazi hicho ni agizo kutoka kwa Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ambaye alimtaka aanzishe kikosi hicho ili washirikiane kuanzisha mpango mkakati wa kuwezesha kuboresha Mfuko wa Afya ya Jamii.“Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Ally Mwalimu alinipa kazi ya kuunda kikosi kazi maalum na kushirikiana nacho kutengeneza mpango mkakati wa kuboresha Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF),” alisema Dkt. Kigwangalla.

Dkt. Kigwangalla amewataja wajumbe wa kikosi kazi hicho kuwa ni Prof. Angwara Kiwara, Prof. Phares Mujinja, Dkt. Francis Frederick, Dkt. Heri Marwa, Dkt. Deogratius Pisa, Dkt. Amos Kahwa, Irenei Kiria, Semkae Kilonzo, Gemini Mtei, Dkt. Jehovaness Aikaeli na Obey Assey.
Wengine ni Mathias Kabunduguru, Dkt. Dereck Chitama, Prof. Flora Kessy, Florence Mwanri, Athuman Rehani, Maximillian Mapunda, Bedason Shallanda, Daniel Ngowi, Beng’ Issa, Edwin Mikongoti, Hussein Sengu, Dkt. Beatus Leon na Dkt. Pastory Sekule.
Aidha Dkt. Kigwangalla amewashukuru wajumbe hao kwa kukubali kufanya kazi na Wizara ya Afya kupitia mpango mkakati wa kuwezesha kuboresha Mfuko wa Afya ya Jamii bila malipo yoyote.
Hata hivyo mara baada ya kuwachagua wajumbe wa kikosi kazi hicho tayari kimependekeza mapendekezo yao jinsi ya kuboresha Mfuko wa Afya ya Jamii ambayo ni kuipa nguvu kadi ya CHF ili itumike kwenye mfumo wa Afya mpaka ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na vituo vya Jirani na kupandisha kiwango cha kuchangia CHF mpaka 30,000.
Mapendekezo mengine ni kuweka bei za kukatisha tamaa watumiaji wa huduma za Afya bila kadi ya Bima ya Afya ama ya CHF na kuwahamasisha waamue kujiunga kuliko kulipa gharama za kila huduma watakayotumia, kuhamisha Mfuko wa fedha za CHF kutoka Halmashauri na kuupeleka NHIF ngazi ya mkoa  lengo likiwa kumtenganisha mtoa huduma na mteja na kuweka 10,000 kuwa kiwango cha chini kwa bei za huduma za afya sehemu yoyote nchini kwa mtu asiye na kadi.
Aidha mapendekezo yao yatatumika kama serikali itayaridhia na wao wametoa mapendekezo hayo kutokana na kutambua kuwa Watanzania wapo tayari kulipia huduma za afya kwa bima ilimradi wawe wanapatiwa huduma bora ambazo zitawaridhisha.

Comments

Popular posts from this blog