CHADEMA Wacharuka Baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda Kumweka Ndani Mbunge wao Saidi Kubenea..Watoa Tamko
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kama ambavyo imeripotiwa kwenye vyombo vya habari na njia zingine za upashanaji habari tangu jana kuwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CHADEMA, Ndugu Saed Kubenea aliwekwa chini ya ulinzi na kuamriwa kwenda kituo cha polisi kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye inadaiwa hakutaka mbunge huyo azungumze na wananchi ambao ni Wafanyakazi wa Kiwanda cha Tanzania Took Garment, waliokuwa wamemuita mbunge huyo kwa ajili ya kumweleza matatizo wanayokumbana nayo kazini hapo, ikiwa ni pamoja na ujira kidogo na mazingira magumu ya kazi.Aidha akitambua kuwa alichofanya matumizi mabaya ya dhamana ya uongozi, hivyo akakusudia kuficha umma usijue uovu huo, katika tukio hilo Makonda aliwaagiza polisi wakamate kamera za waandishi wa habari waliokuwa katika eneo hilo wakitimiza wajibu wao wa kikazi na kitaaluma kwa jamii.
Katika hatua ya sasa, tunaomba kusema ifuatavyo;
1. Tukitambua kuwa mamlaka ya DC kuamuru watu kukamatwa yamefafanuliwa kisheria na kuwekewa mipaka yake ambayo Makonda amedhihirisha kuivuka katika nyakati tofauti sasa, Mkuu huyo wa wilaya hana mamlaka ya kisheria wala ya kisiasa kuhalalisha amri aliyoitoa ya kumkamata mbunge, tena aliyekuwa anatekeleza wajibu wake, tunamtaka DC Makonda amwachie Ndugu Kubenea mara moja huku tukitoa wito kwa mamlaka zilizomteua kumwangalia kwa makini kama bado anazo sifa za kuwa kiongozi wa ngazi hiyo.
2. Kwa kuwa amri hiyo si halali kwa sababu haina msingi wowote wa kisheria, tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kumuachia Ndugu Kubenea ili aendelee na uhuru wake huku akitekeleza wajibu wake wa kuwawakilisha wananchi wa Ubungo badala ya kumsumbua kwa mambo yasiyokuwa ya msingi.
3. Halikadhalika, Jeshi hilo liwarudishie waandishi wa habari vifaa vyao vya kazi vikiwa katika hali salama na bila athari yoyote ama ya vifaa vyenyewe au materials yaliyoko ndani yake.
4. Tunalitaka Jeshi la Polisi kutoa kauli ya kuwahakikishia usalama waandishi wa habari na vifaa vyao kila wanapotimiza wajibu wao kwenye matukio yanayomhusisha Makonda kwa sababu tayari ushahidi unaonesha anaweza kuwa tishio kwao binafsi na vitendea kazi vyao hususan pia wanapokuwepo polisi.
5. Kwa kitendo cha DC Makonda kuamuru kiongozi wa wananchi akamatwe bila kuwepo kosa lolote la kisheria, CHADEMA tutachukua hatua za kisheria dhidi ya DC huyo ili liwe fundisho kwake mwenyewe, wakuu wa wilaya wengine na utawala mzima wa Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli, ili watambue kuwa suala la kuongoza nchi kwa kuzingatia Haki, Katiba, Sheria na taratibu si suala la kupenda bali ni lazima kuzingatiwa kwa ajili ya amani na utulivu wa kweli.
Tutachukua hatua hizo huku tayari kukiwa na kumbukumbu za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBU) ambayo hivi karibuni ilimuonya DC Makonda na wakuu wa wilaya wengine na wakuu wa mikoa ambao wameanza tabia ya kuendesha nchi kwa amri ambazo hazina uhalali wowote zikiwa nje ya mamlaka yao ya kisheria kufanya hivyo.
Tuliamini angalizo hilo la THUB ambacho ni chombo huru cha serikali, lingeweza kuwa mwongozo sahihi kwa viongozi wa serikali na kwamba kosa la awali la Makonda kuwaweka mahabusu watumishi wa Wilaya ya Kinondoni walioko chini yake lingechukuliwa kama fundisho kwake, lakini bahati mbaya watawala wanaweka nta masikioni linapofika suala la haki za binadamu na uongozi bora.
Imetolewa leo Jumanne, Nov. 15, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
Comments
Post a Comment