WAZIRI MKUU MPYA WA SERIKALI YA WAMU YA TANO NI HUYU


Fumbo kuhusiana na mtu mwenye sifa za kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli limeanza kufumbuliwa.
Hali hiyo inatokana na kile alichokidhihirisha Magufuli siku moja baada ya kuapishwa kwake na pia baada ya hapo wakati alipochukua maamuzi kadhaa ya vitendo, ikiwamo kutoa maelekezo muhimu yaliyodhihirisha aina ya Waziri Mkuu atakayemteua.Kwa mujibu wa muundo wa serikali, Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, ambaye mbali ya kuwa kinara wa mawaziri wengine, ndiye anayetakiwa pia kutoa maamuzi mazito linapojitokeza jambo linalomlazimu kufanya hivyo.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa na uongozi nchini wamesema hatua alizochukua Magufuli kuanzia siku ya kwanza ya kuapishwa kwake zinatoa picha ya wazi aina ya watu atakaotaka kuwa nao katika serikali yake.
Baada ya kuapishwa Novemba 5, 2015, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Dk. Magufuli alianza kazi siku hiyo hiyo kwa kutoa hotuba iliyosisitiza juu ya kauli mbiu yake ya ‘hapa kazi tu’ katika kutumikia wananchi, kuwafariji waliokuwa wapinzani wake katika urais huku akiwasihi waungane naye kuijenga Tanzania imara na pia alimteua Mwanasheria Mkuu, George Masaju, huku pia akitangaza siku ya kuanza Bunge kuwa ni Novemba 17.
“Ratiba yake katika siku ya kwanza aliyoapishwa ilikuwa ngumu kutokana na wageni wengi waliomtembelea lakini bado hakutaka kuchelewa katika kuteua Mwanasheria Mkuu. Na siku iliyofuata (Ijumaa) akaonyesha yeye ni Rais wa aina gani kwa kufanya ziara ya ghafla kwenye Wizara ya Fedha na kujionea aina ya watendaji waliopo. Yote haya yanatosha kufichua sifa za mawaziri atakaowateua,” alisema John Jacob, mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam ambaye ni mmoja wa wafuatiliaji wa siasa.
“Hivi sasa siyo kazi tena kubashiri aina ya Waziri Mkuu tutakayekuwa naye. Magufuli ameonyesha wazi kwamba yeye ni mchapakazi na hivyo hawezi kukubali wababaishaji au kuchagua mtu kwa sababu yoyote isiyohusiana na kazi,” alisema Latifa Abdallah, mfuatiliaji pia wa masuala ya siasa mwenye maskani yake jijini Arusha.
DALILI YA SIFA MUHIMU ZA WAZIRI MKUU MPYA
Baada ya uteuzi wa Mwanasheria Mkuu alioufanya siku ya kuapishwa kwake (Alhamisi), Magufuli alisubiri saa chache tu kabla ya kutembea kwa miguu kutoka ofisini kwake hadi katika jingo la Wizara ya Fedha ambako alifanya ziara ya kustukiza, akiingia kila ofisi kuona shughuli za ujenzi wa taifa zinavyoendelea.
Huko, baada ya kukuta watendaji wake wakiwa hawapo ofisini huku akipewa majibu kuwa wameenda kunywa chai, Magufuli alikuja juu na kutoa maagizo muhimu juu ya dhana ya kuchapa kazi.
Ni wazi kwamba kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha kuwa Waziri Mkuu wake atapaswa kuwa mtu wa vitendo zaidi na siyo maneno mengi.
Kadhalika, utoaji wa maamuzi kuanzia siku ya kwanza ni sifa muhimu ya kile alichokuwa akikisisitiza wakati wa kampeni kuwa kamwe, hatavumilia mawaziri wanaopenda majibu ya ‘tuko mbioni’, ‘tuko kwenye mchakato’, ‘tuko kwenye hatua nzuri’ wala ‘tuko kwenye hatua za mwisho’. Ni kazi tu.
Aidha, Magufuli ameonyesha vilevile kuwa Waziri Mkuu wake atakuwa ni mtu wa kutoa maamuzi kwa kasi. Sifa hii inatokana na muda alioutumia katika kutangaza jina la Mwanasheria Mkuu na pia siku ya kuanza kwa Bunge la 11.
Tofauti na ilivyozoeleka, juzi Jumamosi haikuwa siku iliyopita burebure kwa Magufuli. Alifanya kikao kizito na makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, gavana wa Benki Kuu (BoT) na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Katika kikao hicho, Magufuli alitoa maelekezo kadhaa yaliyofichua sifa nyingine muhimu atakazokuwa nazo Waziri Mkuu wake na pia mawaziri wengine.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu kuhusiana na kile kilichoijiri kwenye kikao hicho, ni kwamba Rais Magufuli aliagiza kufutwa mara moja kwa safari za nje za mawaziri na viongozi wengine wa juu serikalini na kwenye taasisi za umma.
Aliagiza kuwa masuala yote ya nje ya nchi yatekelezwe na mabalozi waliopo huko na kwamba, kukiwa na ulazima, basi safari hizo ni lazima ziidhinishwe na yeye (Rais) au Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu. Rais Magufuli aliagiza kuwa anachotaka ni kuona viongozi wakifanya ziara nyingi kwa wananchi vijijini na kuwatatulia kero zao.
Hii ni dalili nyingine ya wazi kuwa Waziri Mkuu ajaye hatakuwa mtu wa kusafiri nje mara kwa mara na badala yake, atakuwa ni mtu wa kuwa karibu na wananchi huku akisimamia shughuli za serikali kwa umakini zaidi.
Agizo jingine muhimu alilotoa Magufuli ni kutaka kuona viongozi hao wakiweka mikakati mbalimbali itakayoanza kutekelezwa mara moja ifikapo Januari 2016, na mojawapo ya mikakati hiyo iwe ni ahadi yake ya kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.
Aliagiza pia kuwapo kwa mikakati ya kuhakikisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu inatolewa bila shida.
Hii maana yake ni kuwa sifa mojawapo ya Waziri Mkuu itakuwa ni kuwa mzuri katika kuandaa mikakati na kusimamia utekelezaji kwa umakini ili kuleta matokeo chanya, tena kwa wakati.
Kadhalika, katika kikao hicho, Dk. Magufuli alisisitiza kuwa ni lazima kila mtendaji wa serikali kuzingatia, kufuata sheria na taratibu ili taifa lisonge mbele kimaendeleo na kwa ufanisi zaidi. Hii ni dalili kuwa Waziri Mkuu wake na pia mawaziri wengine ni lazima wawe waumini wazuri wa sheria na taratibu, na siyo watu wa kufanya kazi kwa mazoea.
Rais Magufuli alimuagiza Kamishna wa TRA kusimamia kwa umakini ukusanyaji wa mapato nchini na kuhakikisha kuwa kero ndogo ndogo kwa wananchi zinatatuliwa kama alivyoahidi.
Aliitaka TRA kuhakikisha inakusanya mapato hayo kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa zaidi na wale wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote.
Hii ni ishara kuwa sifa nyingine muhimu kwa Waziri Mkuu wa Magufuli ni kufanya kazi kwa kujiamini, lengo likiwa ni kuongeza mapato ya serikali na katika kutekeleza hili, anatakiwa kujiamini muda wote kwani Rais atakuwa akimuunga mkono katika kila hatua na hakuna atakayefanya ujanja ujanja kwa kutumia jina la ‘Rais Magufuli’.
Alisisitiza vilevile kuwa katika serikali yake, mtu wa kutoa maamuzi vinginevyo zaidi ya hayo aliyowapa ni yeye (Rais), au Makamu wa Rais.
Umakini katika kuhakikisha kuwa serikali haipati hasara kutokana na manunuzi yasiyozingatia sheria, au yenye harufu ya rushwa, ni eneo jingine atakalopaswa kuwa nalo Waziri Mkuu mpya wa serikali ya awamu ya tano.
Katika kikao hicho, Magufuli alisema suala la manunuzi limekuwa likitumika vibaya na kuwa mwanya wa kuiibia serikali kwa watu kuongeza bei ya vitu hata kama ni vya bei ndogo katika jamii.
“Ikitokea suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa mara moja,”alisema.
Katika hili, ipo sifa nyingine anayotarajiwa kuwa nayo Waziri Mkuu mpya, ambayo ni kuwa na jicho la ziada kuhakikisha kuwa serikali haipati hasara kwa kuuziwa vitu kwa bei ya juu kuliko iliyopo sokoni.
UHODARI BUNGENI
Sifa nyingine muhimu kwa Waziri Mkuu ni kuwa mzoefu wa kukabili changamoto za hoja moto za wapinzani bunegni kwani katika Bunge lijalo, kambi ya upinzani itakuwa na wabunge 121. Kwa sababu hiyo, ni wazi kwamba mtu atakayeteuliwa na Rais Magufuli kwa nafasi ya Waziri Mkuu ni lazima atakuwa na sifa ya kukabiliana na maswali ya wabunge machachari wa upinzani pale inapobidi, ikiwamo wakati wa maswali ya papo kwa papo.
Kwa ujumla, kama ilivyowahi kuripotiwa katika gazeti hili wiki iliyopita, sifa muhimu za ujumla kwa Waziri Mkuu wa Magufuli zatarajiwa kuwa uadilifu, kwa maana ni lazima awe mtu asiyekuwa na chembe ya kashfa, hasa zinazohusiana na rushwa kama ilivyo kwa mwenyewe (Rais Magufuli); Kujiamini kiasi cha kutoa maamuzi magumu na kwa wakati kwa ajili ya maslahi ya taifa; kufanya kazi kwa pamoja na siyo kusaka umaarufu binafsi kiasi cha kumpiku Rais; Uwezo wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya serikali; Kukubalika ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
NIPASHE

Comments

Popular posts from this blog