TAARIFA KUTOKA JIMBO LA LUDEWA MAPYA KUHUSU MRIDHI WA DEO FILIKUNJOMBE




Marehemu Deo Filikunjombe
Makada 10 wa CCM waliochukua na kurejesha fomu wanatarajiwa kupigiwa kura na wanachama wa CCM ili kumpata mgombea atakayepambana na wagombea wa vyama vya upinzani.




By Joyce Joliga, Mwananchi

Ludewa. Wanachama wa CCM katika Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, leo wanapiga kura za maoni ili kumpata mgombea ubunge kupitia chama hicho atakayeziba pengo lililoachwa na Deo Filikunjombe aliyefariki dunia Oktoba 15, mwaka huu.
Makada 10 wa CCM waliochukua na kurejesha fomu wanatarajiwa kupigiwa kura na wanachama wa CCM ili kumpata mgombea atakayepambana na wagombea wa vyama vya upinzani.
Makada hao ni Philip Filikunjombe (mdogo wa Deo Filikunjombe), Edgar Lugome, Johnson Mgimba, Emmanuel Mgaya, James Mgaya, Jackob Mpangala, Simon Ngatunga, Evaristo Mtitu, Deo Ngalawa na Zephania Chaula.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Ludewa mjini, Tafuteni Mwasonya alisema kuwa tayari Mungu amekwishawapatia wananchi wa Ludewa mbunge na kinachosubiriwa ni taratibu za kidunia zifanyike.
Alisema wananchi wanapaswa kumuomba Mungu badala ya kusikiliza maneno yasiyo na maana, kwa kuwa anayetakiwa ni mtu anayeifahamu vizuri Ludewa na mwenye uchu wa kuwaletea maendeleo. Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wananchi walisema imani na matumaini yao ni kuona wajumbe wa mkutano wa CCM wanamchagua mtu anayekubalika.
Mmoja wa wakazi hao, Bruno Mtega alisema wanaamini kuwa mtu atayechaguliwa na wana CCM atakuwa mshindani mzuri miongoni mwa wagombea ubunge watakaopigiwa kura.
John Haule anayeishi Mavanga mjini hapa, alisema wagombea wote wana nafasi sawa, lakini yupo mmoja ambaye ni zaidi ya wote kwa kila kitu.
Alisema licha ya kumpoteza Filikunjombe, wana nafasi ya kuchagua mtu ambaye atafanya vizuri zaidi miaka mitano ijayo.

Comments

Popular posts from this blog