MAMA: Miezi 11 Mwanangu Anaishi Kwa Mateso Bila Upasuaji!
Mtoto Asmina Abdallah.
Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
Mtoto
Asmina Abdallah mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minne, mkazi wa
Kijiji cha Mgambo, Unguja, Zanzibar anaishi kwa mateso bila kufanyiwa
upasuaji kwa madai ya kutokamilika kwa vipimo kufuatia upungufu wa
mashine katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mtoto
Asmina Abdallah akiwa na mama yake, Amina Maburuki Amani.Maisha ya
mtoto huyo kwa sasa yapo hatarini kutokana na uvimbe uliopo machoni
kuongezeka na haujapatiwa ufumbuzi wa matibabu kwa miezi 11 huku ukienda
sambamba na maumivu makali.
Akizungumza
na waandishi wa habari hii wiki iliyopita katika wodi ya watoto ya
Makuti A Muhimbili, mama mzazi wa mtoto huyo, Amina Maburuki Amani
alisema kwamba hali ya mtoto wake inazidi kuwa mbaya na anaelekea kukata
tamaa.
Akifafanua zaidi mama huyo alikuwa na haya ya kusema:
“Hali ya
mtoto wangu imekuwa ikibadilika kila kukicha huku akilia kutokana na
maumivu makali, nimechoka safari ya kila mara ya kuja Muhimbili kwa
nauli ya kuombaomba kwa wasamaria mema.
“Maisha yangu yako duni, najua ipo siku nitashindwa kuja, sina kazi na wala sijui mume wangu aliko.
“Tangu
uvimbe huu umuanze mwanangu ukiwa kama upele Januari mwaka huu, umekuwa
ukiongezeka, nilifika Muhimbili kwa mara ya kwanza Januari mwanzoni
lakini Aprili mwaka huu nikarudishwa nyumbani kutokana na ukosefu wa
mashine ya CT Scan.
“Nililazimika
kuja tena Muhimbili Juni nilikaa kidogo nikaambiwa kipimo hicho kiko
katika hospitali binafsi hivyo zinahitajika fedha, nikalazimika kwenda
nyumbani kutafuta bila mafanikio.
“Hali ya
mtoto ilizidi kuwa mbaya nikaomba nauli kwa majirani nikamleta hapa
Muhimbili, Mama Salma Kikwete yaani mke wa rais mstaafu wa awamu ya nne
alinisaidia shilingi laki nne na nusu na baadhi ya wasamaria wema
walinichangia baada ya kuona habari yangu katika gazeti hili.
“Nikafanyiwa
kipimo cha CT Scan katika Hospitali ya Besta lakini hata hivyo hakupata
matibabu kutokana na kutokamilika kwa vipimo vingine.
“Niliambiwa
na uongozi wa Muhimbili kuwa angeweza kwenda India lakini sioni
matarajio, Agosti 20 nikarudishwa nyumbani, baadaye hali ya mtoto
ikazidi kuwa mbaya akawa anazimia.
“Nililazimika kumleta tena hapa Muhimbili Oktoba 7, amepimwa damu na sasa nasubiri matokeo pia nijue nini kitaendelea.”
Kwa yeyote aliyeguswa na kilio cha mama huyu awasilianenaye kwa namba yake ambayo ni 0658 323590.
Comments
Post a Comment