WATAALAMU WA MAMBO YA SIASA WANAKWAMBIA KUWA ETI SLAA NI SHUJAA WA TAIFA
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dokta Wilbroad Slaa.
HOTUBA ya kwanza tangu ‘atoweke’ kwenye anga za siasa ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dokta Wilbroad Slaa, aliyoitoa juzi Jumanne juu ya kujiweka pembeni, imepokelewa kwa hisia tofauti huku wengi wakimuita kuwa ni shujaa wa taifa kutokana na ujasiri wake, Ijumaa lina kila kitu.
Katika mahojiano yaliyowahusisha wananchi na wachambuzi mbalimbali wa mambo ya kisiasa kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam mara baada ya kiongozi huyo kukutana na waandishi wa habari, waliliambia Ijumaa kuwa, Dokta Slaa ni mtu wa aina yake ambaye taifa halijapata kuwa naye tangu kuondoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai, Mhe. Freeman Mbowe.Ana msimamo
Wengi walionesha kufurahishwa na misimamo ya kiongozi huyo tangu ajiingize kwenye masuala ya siasa, kwani siku zote amekuwa mstari wa mbele kuwatetea wanyonge, kuanika maovu na kukemea kila analoliona lipo tofauti na anavyoamini.
“Kwa kweli mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Dk. Slaa ni kati ya viongozi wenye msimamo asiyekubali kuyumbishwa. Amekuwa hivyo tangu nilivyomjua na hata hotuba yake aliyoitoa juzi, inadhihirisha hilo,” alisema Chande Juma wa Kinondoni jijini Dar.
Alisema kama mtu alifuatilia vizuri mazungumzo yake, ni wazi kuwa viongozi wenzake walikubali kubadili msimamo ili kumwezesha Lowassa aingie Chadema, lakini yeye akakataa licha ya kamati ndogo kuundwa ili imshawishi alegeze msimamo.
Mgombea urais kupitia Chadema(Ukawa) Edward Lowassa.Rushwa ni adui mkubwa kwake
Mchambuzi mmoja wa habari za siasa aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema siku zote anamtambua Dk. Slaa kama mtu mwenye kuichukia rushwa, kwani anaamini hicho ndicho chanzo cha matatizo yote yanayosababisha kero za wananchi kutoisha, licha ya nchi kuwa na rasilimali za kutosha.
“Unampata wapi sasa hivi aina ya kiongozi ambaye anaweza kukataa rushwa ya shilingi milioni 500 akitetea masilahi ya wananchi masikini? Viongozi wetu wa sasa kila mtu anaweka mbele masilahi yake na familia yake, suala la kuwatetea wanyonge wanalifanya kama maigizo tu,” alisema mchambuzi huyo, akikumbushia jinsi mbunge huyo wa zamani wa Karatu alivyokataa kiasi hicho cha fedha ili ashiriki kuzuia ripoti ya Kamati ya Bunge juu ya sakata la Richmond isisomwe bungeni.
Maneno kama hayo yalisemwa pia na mkazi mmoja wa Sinza, Nicholaus John akirejea jinsi alivyokataa rushwa ya uongozi pale alipoahidiwa kazi nje ya nchi, ilimradi tu akubali kuachia ubunge wake katika Jimbo la Karatu.
Kwake ni taifa kwanza
Kitendo chake cha kueleza kuwa alitumia sehemu kubwa ya mshahara wake kumpa mkewe ili afanye ziara ya kuzunguka nchi nzima katika harakati za kukijenga chama, ni kielelezo kuwa kiongozi huyo anajali ustawi wa taifa kwa namna anavyoamini kuliko maisha binafsi ya familia yake.
“Slaa amekuwa akitanguliza masilahi ya taifa kwenye siasa zake, kama mtu anakubali yeye na familia yake wale mihogo na maharage ili kipato chao kitumike kwenye mambo ya siasa, unadhani ana uchungu kiasi gani na taifa hili?” alihoji Mama Saidi wa Mwananyamala jijini Dar.
Kuweka maisha yake rehani
Kitu kingine kinachofanya wananchi wengi kumuona Dk. Slaa kuwa ni shujaa wao ni kitendo chake cha kukubali kuweka maisha yake rehani, ilimradi tu mambo makubwa na muhimu ya nchi yanasemwa hadharani na kila mmoja ayasikie.
“Ni nani atakuwa tayari kufa kwa kuwataja watu majina kwenye uovu, tena watu hao ni vigogo wenye fedha na mamlaka ambao wanaweza kumfanya lolote. Fikiria kitendo chake cha kutaja majina ya mafisadi papa wakati ule. Huu ni ujasiri wa aina yake,” alisema Liffa Jason, mwenyeji wa Shinganya aliye Dar kibiashara.Walisema Dk. Slaa alifanya hivyo akijua yeye binafsi hafaidiki na lolote, lakini aliweza kuwataja ili kuwafunua wananchi wawajue watu wanaoitafuna nchi yao.
Hana tamaa
Kingine kilichoelezwa na watu hao ni kwamba kiongozi huyo hana tamaa ya fedha wala madaraka, kwani alikubali kuacha ubunge, wenye mshahara na marupurupu mengi na kwenda kufanya kazi ya kukijenga chama, kitu ambacho alifanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Lakini kikubwa zaidi, wamedai kwamba Dk. Slaa angeweza kunyamaza kimya na kufanya kazi ya kumnadi Lowassa, kwani kwa vyovyote mwisho wa siku angepata kuteuliwa katika nafasi kubwa na nyeti serikalini.
“Kiukweli hana tamaa, naamini angekaa kimya na ukatibu mkuu wake wa chama, bado maisha yake yangekuwa mazuri, kaamua kujiweka pembeni bila kujali athari atakayoipata ili tu asikumbatie mafisadi ndani ya Chadema,” anasema Elika wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Apewe ulinzi
Kwa kuzingatia mambo yote yanayoendelea katika maisha yake ya kisiasa, wananchi waliozungumza suala hili walitaka kiongozi huyo ambaye sasa yuko nchini Italia kupewa ulinzi, kwani kazi yake kubwa kwa nchi inawakera watu wachache wanaoweza kumdhuru kwa namna yoyote.
“Unajua tangu siku alipoongea na kuwalipua viongozi wa Ukawa, ni lazima kutakuwa na vitisho, wengine wamemtukana na kudai kajidhalilisha, lakini ukweli unabaki palepale kuwa yeye ni shujaa na anastahili ulinzi ili wasitokee wa kumdhuru,” alisema Modesta George wa Oysterbay jijini Dar na kuongeza:
“Lakini pia kwa kila mwenye mapenzi na nchi ya Tanzania, anayechukia ufisadi, rushwa na uonevu ndani ya vyama vya siasa anayeona kuwa alichokifanya Slaa ni kitendo cha kishujaa, tuungane kumuombea ili Mungu amuepeshe na balaa.”
Aibomoa VIBAYA Ukawa, aacha majeraha
Kitendo chake cha kutoa maneno makali kwa viongozi wenzake wa Chadema na Ukawa, kimesababisha majeraha kwa umoja huo, kwani viongozi sasa wamegawanyika juu ya nani ni mkweli kati ya yanayosemwa kuhusiana na sakata zima la Dk. Slaa.
“Dk. Slaa ametuacha njia panda, sasa kama yeye alikataa kumkaribisha fisadi bila kutimiza masharti, lakini wenzake wakafanya ina maana sisi sasa tushike lipi?” alihoji Bruno Kei wa Tegeta Kibaoni.
Slaa vs Chadema, Lowassa
Siku moja baada ya Dk. Slaa kutoa hotuba yake hiyo iliyowasisimua mamilioni ya Watanzania wenye uchungu na nchi yao, baadhi ya viongozi wa chama chake wameibuka na kumtetea mgombea wao, Edward Lowassa wakisema kilichotokea katika kumkaribisha kiliridhiwa na pande zote, akiwemo katibu huyo.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akihojiwa na BBC, alisema Dk. Slaa ni mwongo, kwani kama kulikuwa na masharti yoyote ambayo yeye aliweka kwa ujio wa Lowassa, basi yeye alipaswa kushirikishwa kama mtu wa sheria, kitu ambacho hakikuwahi kufanyika.
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia akijibu madai ya Dk. Slaa, alidai kuwa alichokisema Dokta Slaa ni siasa nyepesi zinazoonyesha kushindwa.
“Tupambane kwa hoja badala ya uchochezi kwa sababu sisi sote tutapita ila nchi yetu itabaki, maneno yote ya Dk. Slaa yalijaa uchochezi ila kwa kifupi ni kwamba, sisi katika Ukawa tupo pamoja na tunamuunga mkono mgombea wetu.”
Comments
Post a Comment