LOWASSA AAHIDI UTENDAJI SPIDI 120
MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia anaungwa mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, Edward Lowassa amesema endapo atachaguliwa kuwa rais ataunda serikali isiyokuwa ‘nyoronyoro’.
Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) ambaye pia anaungwa mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi,
CUF na NLD, Edward Lowassa.
Akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam katika
viwanja vya Shule ya Msingi Bunju ‘A’, Lowassa alisema muda umefika kwa
wananchi wa Tanzania kufanya mabadiliko. “Naombeni mniteue niwe rais
wenu ili mpate maendeleo ambayo hamkuwahi kuyapata kwa kipindi cha miaka
zaidi ya hamsini.“Mimi nitaunda serikali isiyokuwa nyoronyoro na inayofanya kazi zake kwa ufanisi na kila mtanzania ataweza kunufaika na rasilimali za nchi yake,” alisema Lowassa aliyehutubia kwa takribani dakika kumi. Alisema endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, serikali yake itafanya kazi kwa spidi ya mwendo kasi wa 120 na hivyo lazima kutakuwa na maendeleo makubwa kwa muda mfupi.
“Nitaondoa changamoto zote zinazowakabili wananchi wa Tanzania, ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mengi hapa nchini, nitatatua changamoto ya mazingira ya kufanyia biashara ndogondogo pamoja na kutoa elimu bure,” alisema Lowassa. Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa wasiwe na hofu kuwa kura zao zitaibwa, akisema, “Hakuna atakayeiba kura ng’o. Nimesikia kuwa kuna njama za kuiba kura, hakuna jambo kama hilo, bali kila mtu akipiga kura ahakikishe analinda kura hadi mwisho ili kutoruhusu mwanya wa kuiba na hakuna atakayeiba kura ng’o.”
Awali, akimkaribisha Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema wamezunguka katika baadhi ya maeneo ya nchi na kuona watanzania wamechoka na ugumu wa maisha na hivi sasa wanataka mabadiliko. “Watanzania wanahitaji mabadiliko, tumepata mapokezi makubwa sana kila tulipopita kuomba ridhaa ya wananchi, hii inaonesha ni jinsi gani wananchi hawa wapo tayari kukombolewa,” alisema Mbowe.
Mbowe aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na kuchagua Chadema ili kiwakomboe na kutatua changamoto zinazolikabili taifa. Baada ya kutoka Kawe katika Manispaa ya Kinondoni, jioni Lowassa alikwenda katika jimbo lingine la manispaa hiyo, Kibamba, kuendelea na mkutano wa kampeni. CHANZO: HABARI LEO
Comments
Post a Comment