KILIO KIKUBWA: CCM YAPATA PIGO ZITO BAADA YA MGOMBEA WAO KUFARIKI DUNIA, HALI NI TETE KWA WAGOMBEA


Mgombea udiwani kata ya Muleba Wilaya ya Muleba Kusini, kwa tiketi ya CCM, Osward Rwakabwa amefariki dunia kwa ajali ya pikipiki.
Osward ni mgombea wa tatu udiwani kwa tiketi ya CCM kata ya Muleba kufa akiwa katika harakati za kampeni za Uchaguzi Mkuu kwani wa kwanza alikufa mwaka 2005, 2010 na mwaka huu 2015.
Osward alifariki katika hospitali ya serikali ya Kaigala alikopelekwa mara baada ya ajali hiyo iliyotokea jana jioni katika maeneo ya Tanesco akaribu na viwanja vya michezo vya Zimbiile Wilaya ya Muleba Kusini.
Walioshuhudia ajali hiyo walisema marehemu ambaye alikuwa akiendesha pikipiki aligongana na pikipiki nyingine ambayo mmiliki wake alikimbia baada ya ajali hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, Osward alikuwa akivuja damu kwenye pua na kwenye masikio mara baada ya ajali hiyo lakini alifariki katika hospitali hiyo.
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa marehemu Muleba kuhani msiba kabla ya kuanza mkutano wake wa kwanza. Akizungumza kwenye mkutano huo, Dk. Magufuli aliwapa pole wanafamilia kuwataka wawe watulivu kwani hiyo ni kazi ya mungu na haina makosa.
Mgombea ubunge wa jimbo la Muleba Kusini kwa tiketi ya CCM, Anna Tibaijuka, alimshukuru Dk. Magufuli kwa kwenda kuhani msiba huo licha ya ratiba yake kuwa ngumu. Alisema licha ya kwamba umati mkubwa umehudhuria msiba huo lakini watu wengi wamejitokeza kumsikiliza katika viwanja vya Zimbiile. “Osward ametutoka ghafla na tulitarajia kuwa naye leo lakini ndiyo hivyo tena tumwombee Osward kwa Mungu ili amweke pahala pema peponi, “ alisema Tibaijuka.
Mkazi wa Muleba Kusini, Alistides Kaigwa alisema hiyo ni mara ya tatu kwa mgombea wa CCM anayewania udiwani kata hiyo kufa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Alisema diwani wa sasa wa kata ya Muleba ni Hassan Milanga wa CUF ambaye amekuwa diwani wa kata hiyo kwa vipindi vinne. Alisema Hassan aliwahi kuwa mwanachama wa CCM na jina lake lilipokatwa ndani ya chama hicho mwaka 1995, alihamia CUF na kushinda udiwani wa kata hiyo.
Wagombea wa udiwani wa CCM kata hiyo mwaka 2005, 2010 na 2015 wote walifariki wakiwa wameshateuliwa na kupitishwa na chama hicho kuwania udiwani.

Hata hivyo, mwandishi hakuweza kuyapata mara moja majina ya wagombea udiwani wa CCM waliofariki kaBLA ya uchaguzi mkuu wa 2005 na 2010.
CHANZO: NIPASHE

Comments

Popular posts from this blog