BIA YA KILIMANJARO YAZIPAMBA SIMBA, YANGA

 Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
WADHAMINI wakuu wa klabu kongwe nchini, Bia ya Kilimanjaro, leo 'wamezipamba maua' baada ya kuzikabidhi jezi na vifaa vingine vipya vyenye thamani ya Sh. milioni 70 kwa ajili ya msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaoanza Septemba 12.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Meneja wa Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli, amesema wataendelea kuhakikisha mishahara ya wachezaji wa klabu hizo mbili inalipwa huku wakijivunia kuzinunulia klabu hizo mabasi mawili makubwa kwa ajili ya usafiri wa wachezaji.

"Tunaamini timu zote mbili zimesajili vizuri na zitafanya vyema kwenye ligi msimu huu. Yanga imetwaa Ngao ya Jamii na Simba imekuwa ikifanya vizuri katika mechi za kirafiki tangu kuajiriwa kwa kocha mpya," amesema Pamela.
Vifaa vilivyokabidhiwa leo kwa wawakilishi wa klabu hizo; Kaimu Katibu Mkuu wa Simba, Collins Frisch na Meneja Masoko wa Yanga, Omary Kaya ni jezi seti mbili kwa kila klabu, jezi za mazoezi, 'casual wear', mipira, vizuia ugoko (sheen guard), viatu vya kuchezea, viatu vya mazoezi, soksi, glavu za makipa na mavazi ya maofisa wa mabenchi ya ufundi.
Wawakilishi wa klabu hizo mbili wameupongeza uongozi wa Kilimanjaro Premium Lager kwa kuwapatia vifaa hivyo huku wakiomba ufadhili zaidi kutoka kwa wadau wengine wa michezo nchini.

Comments

Popular posts from this blog