Unamuwaza kila wakati, hakuwazi kabisa, wa nini?
NAMSHUKURU Mungu kwa kunikutanisha na wewe msomaji wangu katika safu hii, hakika yeye ni mwema na ametujalia uzima ili na wewe uweze kupata kusoma kile ambacho nimekuandalia siku ya leo.
Mapenzi ni dawa. Mapenzi yanatupa
furaha, yanatingisha dunia. Hakuna kitu kizuri kama kupendwa. Umpate mtu
akupende na wewe umpende. Dunia yote mnaiona ni ya kwenu.
Pamoja na kuwa matamu, wakati mwingine
hugeuka shubiri. Yanakuwa machungu pale mmoja wenu anapokuwa hampendi
mwenzake sawasawa na anavyopendwa.
Mmoja anapokuwa anampenda mwenzake
wakati anayependwa harudishi upendo, penzi haliwezi kuwa na uhai mrefu.
Linaweza kulazimishwa kwa sababu fulani lakini mwisho wa siku ukweli
unabaki palepale. Naam! Hapo ndipo kwenye kiini cha mada yangu ya leo.
Ambaye anapendwa ataleta visa ili mradi
tu muachane, atafanya hivyo kwa sababu hakupendi. Yupo ampendaye. Si
wewe. Wewe anakufanya wa akiba au maslahi fulani.
Unayempenda anaweza kukudanganya.
Akajifanya anakupenda kumbe hakupendi. Moyo wake haupo kwako. Anakuwa na
wewe kwa sababu unamuwezesha kiuchumi. Vinginevyo asingethubutu kuwa na
wewe.
Anajibaraguza kama anakupenda,
atakuigizia kama michezo ya runingani. Atakwambia ‘baby i love you so
much’ kumbe anaye ‘sweet heart’ wake tofauti na wewe. Huyo ndiye
anayempenda. Ndiye anayemkosha nafsi yake. Anayemfurahisha. Hisia zake
ndiyo zimefika kwake, ndiyo ini mkalia nyonga wake.
Kwa hali hiyo, kuna wakati unafika penzi
huwa linageuka adhabu. Yule anayependwa kwa kuwa anakuwa na mtu
mwingine anayempenda, anafanya visa ili mradi ujue tu hakuhitaji.
Anaonyesha viashiria mbalimbali ambavyo
vinadhihirisha hakuhitaji. Wewe unakuwa umependa, huwezi kuviona
viashiria hivyo. Vituko vyote anavyokufanyia, unajifanya kipofu huvioni.
Unaona ni changamoto tu za mapenzi. Husikilizi la mtu hapo. Unachoangalia ni uhai wa penzi lako. Hauko tayari kuvunja uhusiano.
Unapambana kutetea uhai wa penzi lako.
Unafanya kila linalowezekana kuhakikisha unamweka kwenye mstari mpenzi
wako. Unakuwa mtumwa wa mapenzi bila wewe mwenyewe kujitambua.
Kwenye kipindi hicho hata mtu
akikushauri uachane naye kutokana na visa anavyokufanyia mpenzi wako,
unamuona mchawi. Asiyependa maendeleo yako. Utahisi anakuonea wivu. Tena
mnaweza mkagombana kama ataendelea kukushauri uachane naye.
Yote hayo unayafanya kwa sababu moyo
unakuwa umependa. Moyo unakuwa ‘umekufa’, umeoza kabisa! Kutetea penzi
hilo kunakuwa na nguvu kwa sababu akili yako inamuwaza kila wakati. Hapo
hutaki kusikia wala kuona penzi lenu limeisha. Eti unafikia hatua ya
kusema; ‘bora nife kuliko kumpoteza.’ Kweli kabisa?
Hukubaliani na ukweli kwamba unakopenda
hupendwi. Hufikirii kabisa kwamba kuna suala linaitwa uongo kwenye
mapenzi. Pengine alikudanganya.
Huoni sababu ya kuwaza kwamba ‘kila ndege hutua kwenye mti aupendao.’ Hutaki kuamini kwamba yeye si mti uupendao.
Unapelekwa na hisia zako. Unaamini yeye
ndiye mtu sahihi kwako duniani. Kwa kuwa unakuwa umeshaonjeshwa penzi,
mawazo yako yote unayaelekeza kwake.
Uvumilivu huwa unafikia mwisho. Baada ya kukuonesha vitimbi kwa muda mrefu, ukawa huelewi somo, anaweza kukuchana ukweli.
Anakuambia kabisa hawezi kuendeleza
safari ya mapenzi na wewe. Moyo wake haupo kwako. Haoni sababu ya
kuendelea na wewe. Alichokuwa anakihitaji kwako kimeshafika ukingoni.
Pengine alishamtimizia shida yake kwa
wakati huo, haoni sababu ya kuendelea kuishi kwenye penzi ambalo halina
faida siku za usoni.
Itaendelea wiki ijayo.
Comments
Post a Comment