TCRA YATOA ADHABU KALI KWA TELEVISION YA ITV KWA HABARI ZA UONGO
1.0 Utangulizi:
Mnamo
tarehe 10/08/2015, kituo cha ITV kilikiuka Kanuni za Huduma ya
Utangazaji (Maudhui), 2005 kupitia kipindi cha Habari Zilizotufikia Hivi
Punde kilichorushwa hewani kati ya saa 2.30 asubuhi hadi saa 5.30
asubuhi. Kipindi hiki kilikiuka Kanuni za Utangazaji kwa kutoa taarifa
zisizo za kweli na za kichochezi zilizotangaza kwamba Jeshi la Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano ya mgombea wa
CHADEMA Mheshimiwa Edward Lowassa. Taarifa hiyo ilikuwa na maandishi
yaliyosomeka kama ifuatavyo:-
1. “
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lapiga marufuku maandamano
ya kumsindikiza kuchukua fomu mgombea Urais kupitia CHADEMA”.
2. “
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lakanusha kupiga marufuku
maandamano kutokea ofisi za CUF kuchukua fomu Mgombea Urais kupitia
CHADEMA.
Katika
kuhitimisha taarifa hiyo mtangazaji alisikika akisisitiza kwamba
Kamishina Suleiman Kova alisema ni marufuku maandamano ya mgombea wa
CHADEMA kupitia UKAWA kwenda kuchukua fomu katika Tume ya Taifa ya
Uchaguzi. Mtangazaji alisikika akizungumza maneno yafuatayo:-
“….ni
Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova akizungumza na
ITV, Radio One pamoja na Capital Radio amesema ya kwamba ni marufuku
maandamano ya Mgombea wa CHADEMA kupitia UKAWA Mheshimiwa Edward Lowassa
kwenda kuchukua fomu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi… hizo
ndizo taarifa ambazo zimetufikia hivi punde”
2.0 Kanuni zilizokiukwa
Kituo cha ITV kimekiuka Kanuni zifuatazo za Huduma ya Utangazaji (Maudhui) 2005
Na. 5(h), 6(2)(b) na 6(2)(c) ambazo zinazosomeka hivi:-
5 Every licensee shall ensure that the programme and its presentation-
(h) does not incite or perpetuate hatred against or vilify, any
group or persons on the basis of ethnicity, race, gender,
Religion or disability.
6(2) The licensee shall-
(b) report accurately and fairly;
6(2)(c) report news in an objective and balanced manner, without
intentional or negligent departure from the facts, whether by
distortion, exaggeration, misrepresentation or material omission;
Tafsiri ya Kanuni hizi kwa mujibu wa Kamati katika shauri hili ni kama ifuatavyo:-
5. Kila mwenye leseni ya utoaji huduma za utangazaji lazima ahakikishe kuwa vipindi vyake vinazingatia:-
(h) havileti uchochezi wala kujenga chuki kwa mtu au kundi la watu kwa kigezo cha kabila, rangi, jinsia, dini au ulemavu.
6(2) Kila mwenye leseni ni lazima ahakikishe-
(b) anatoa taarifa kwa usahihi na uhakika;
6 (2) (c) anaripoti habari bila upendeleo na kizingatia mizani, bila
kukusudia au kuondoka katika ukweli, ama kwa
kuvuruga au kutoa taarifa zisizo sahihi.
3.0 Ushahidi wa Makosa
3.1 Kuangalia DVD ya kipindi cha “Habari Zilizotufikia Hivi Punde”
Ili
kujiridhisha kama maudhui ya kipindi cha Habari Zilizotufikia Hivi Punde
na uwasilishaji wake ulikiuka Kanuni za Utangazaji, Kamati na uongozi
wa ITV waliangalia sehemu ya kipindi hicho. Maudhui ya kipindi hicho
yalionyesha ukiukwaji wa Kanuni za Utangazaji.
4.0 Maelezo ya utetezi
4.1 Maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa ITV
Mkurugenzi
wa ITV aliwasilisha utetezi wa maandishi wakikana kuhusu tuhuma zote za
ukiukwaji wa Kanuni uliofanywa na kituo chao. Alisema msingi wa habari
ulikuwa si wa kichochezi na ilikuwa ombi la Kamishna wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kutoa ufafanuzi wa taarifa za
upotoshaji zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
Aliendelea
kusisitiza kwamba taarifa haikuwa ya kichochezi kutokana na ukweli
kwamba watu walikuwa wamekusanyika Buguruni Ofisi ya CUF kwa lengo la
kuandamana kumsindikiza Mgombea Urais wa CHADEMA jambo ambalo Kamishna
Kova alipiga marufuku. Mkurugenzi pia aliendelea kusema kuwa wakati
wakirusha hewani taarifa ya Kamishna Kova walikuwa wanabadilisha
maandishi kwenye runinga kulingana na taarifa zilizokuwa zinatolewa na
Kamishna Kova.
Aliendelea
kusema kwamba pamoja na kutoa taarifa iliyolalamikiwa Kamishna Kova
alirudi tena kwenye kituo cha ITV na alitoa taarifa kwa umma kwamba
Jeshi la Polisi liliafikiana na viongozi wa vyama hivyo kwamba
maandamano yaanzie ofisi za CUF zilizoko Buguruni hadi ofisi ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi na baadae kuishia Kinondoni katika ofisi za CHADEMA.
4.2 Maelezo ya Mhariri Wa Habari
Mhariri
wa Habari wa ITV alitoa utetezi wake kwa kusema kwamba nia ya ITV
haikuwa kuleta uchochezi kwa kuwa habari ilikusudia kuondoa upotoshaji
wa taarifa kwamba watu waache kwenda mjini kutokana na kuwepo kwa
maandamano ya CHADEMA. Alisisitiza kwamba Mtangazaji wa taarifa hiyo
hakuwa na nia mbaya wala kusudio la kuchochea uvunjifu wa amani na
dhamira yake haikuwa kumfanya Kamishna Kova kuongea anachokitaka yeye
kama mwandishi wa habari ila kuondoa hofu kuhusiana na suala zima la
maandamano.
4.3 Maelezo
Mwanasheria/Mwakilishi
wa ITV alitoa utetezi wake kwa kusema maneno yaliyoandikwa kwenye
taarifa hiyo yalikuwa ni vionjo tu vya kumwezesha mtazamaji kuvutiwa na
taarifa kisha asikilize na kupata ukweli. Bwana Semvua alitoa mfano wa
magazeti yanavyotoa vionjo vya taarifa mbalimbali ambazo humvutia mtu
kuisoma habari katika tukio husika.
5.0 Kukiri Kosa
Katika
majumuisho yao wawakilishi waliotoa utetezi wa ITV moja baada ya
mwingine walikiri kosa na kudai kuwa kituo chao hakina kawaida ya kuitwa
mbele ya Kamati kwa makosa na wao kama binadamu hawakuwa na dhamira ya
kusababisha vurugu nchini kwa kuwa binadamu hukosea.
Mhariri
wa Habari ITV alisisitiza kwamba haikuwa nia yao kuleta uchochezi na
wala mtangazaji wa taarifa hiyo hakuwa na nia mbaya. Mhariri wa habari
alizungumza maneno yafuatayo:-
“Mwenyekiti
tunakushukuru, tunaomba mtuelewe kwamba muktadha wa tukio lote hili
haukuwa na nia mbaya, kwa maana ya kwamba nia mbaya
haikukusudiwa…hakukuwepo na kusudio , hakukuepo na nia mbaya na ovu
yoyote kupeleka lile tukio liwe na tafsiri ya watu kwa jinsi walivyo
lipokea…”
Mwanasheria/Mwakilishi
alisema lengo halikuwa kufanya kosa hilo kwa makusudi na naomba
mtuchukulie hivyo tulifanya kosa kwa bahati mbaya, makosa yapo kwa
binadamu na tafsiri ya kimtazamo ni kawaida kukosea na ilikuwa ni bahati
mbaya watajirekebisha. Alisema maneno yafuatayo:-
“Makosa
yapo ya kila mwanadamu, tulifanya hivyo tudhani tumefanya vizuri na ndio
maana tulidhani tutapongezwa, lakini mtizamo wa wenzetu kwa kweli
imeonekana na tulivyosikia…si kweli kwamba tunaonewa asilimia mia moja..
ukiangalia ITV na Redio One siyo vituo vinanyoletwa letwa huku mara
nyingi na ikitokea mtuchukulie kwamba imetokea kwa bahati mbaya kama
wanadamu na sisi tutajirekebisha kwa haya mliyotuadvise…..”
Aidha
Mkurugenzi wa Radio One alikiri kwamba lengo lilikuwa zuri na kusudio
lilikuwa kuondoa uvumi uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii. Bwana Deo
Rweyunga alisema yafuatayo:-
“…wito
wenu ni wa nia ya kutaka kujirekebisha ili tuende vizuri pamoja,
mmetuandikia tumejieleza, tumekaa pamoja na tumezungunza pamoja, lengo
lilikuwa ni zuri tujaribu kuondoa uvumi ambao ulikuwa tayari kwenye
mitandao….tukiri katika hili ambalo limeonekana kidogo ni tofauti,
tutachukua hatua kama inavyofahamika vyombo vyetu tumekuwa tunajitahidi
sana na tumeteleza kidogo tunaomba mtuwie radhi kwa hilo”
Mkurugenzi
Mtendaji alisema Breaking News ya Tanzania inavyoendeshwa ni vigumu
kuipata, tunaomba radhi kwa hilo lililotokea haikuwa dhamira yetu,
tutahakikisha tunaedelea na dhamira yetu ya kutoa matangazo kwa ubora.
Kubwa lilituleta ni mwanzo na mwisho wa taarifa yenyewe na waliomba
radhi na kuhakikisha watafanya kazi kwa umakini. Alisema maneno
yafuatayo:-
“…pamoja
na hayo kubwa ambalo limetuleta ambalo tumeliona ni mwanzo na mwisho…na
marekebisho ambayo tuliona tukarekebishe tukiwa hewani ni kwamba
tunaomba radhi kwa hilo kwa sababu sisi tulikuwa tunaongea kwa upande
wetu jinsi tunavyofanya kazi…..tunaomba radhi kwamba limetokea hivyo
liliyotokea na hivyo lilivyopokelewa huko nje…na haijawa dhamira yetu
wala nia yetu ya kuvuruga hii nchi…”
6.0 Tathmini ya Kamati
Kamati
iliridhika kwamba, kituo cha ITV katika kipindi cha Habari Zilizotufikia
Hivi Punde kilikiuka Kanuni za Utangazaji kwa kutoa taarifa zisizo za
kweli na za kichochezi zilizotangaza kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalum
ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano ya mgombea wa CHADEMA
Mheshimiwa Edward Lowassa.
Kamati
iliona upungufu katika maneno yaliyoandikwa kwenye runinga (subtitling)
wakati Kamisha Kova akihojiwa. Katika utangulizi wa Habari Zilizotufikia
Hivi Punde mtangazaji alisikika akisema kwamba Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam lapiga marufuku maandamano ya kumsindikiza
kuchukua fomu mgombea Urais kupitia CHADEMA. Mtangazaji alisikika
akimhoji Kamishna Kova kutoa ufafanuzi kuhusu kupiga marufuku
maandamano. Kamishna Kova alisikika akisema alichukua nafasi hiyo
kuwapigia ITV na Radio One kuondoa uvumi uliokuwa umeenea kwenye
mitandao ya kijamii kuwa Polisi wamepiga marufuku maandamano ya
Kumsindikiza Mheshimiwa Lowassa kuchukua fomu za kugombea Urais katika
Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kamishna Kova alisema Polisi ilikuwa
imepanga kuwapa ulinzi wasindikizaji wa Mgombea Urais Mheshimiwa
Lowassa kupitia CHADEMA kutoka ofisi za CHADEMA Kinondoni mpaka ofisi za
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama Jeshi la Polisi lilivyotoa ulinzi kwa
wasindikizaji wa mgombea Urais Kupitia Chama Cha Mapinduzi DKt John
Magufuli. Kamisna Kova alisisitiza kuwa haikuwa jambo jema kwa
maandamano kutokea kila sehemu ya jiji kwa vile kungeweza kuleta
uvunjifu wa amani na kuathiri shughuli zingine za wananchi. Kamisna Kova
alisisitiza kuwa:-
“………ukiwazuia
watu kwa kwenda tu kuchukua fomu hapo unaweza kusababisha uvunjifu wa
amani na njia tunayoisema ambayo tunaitambua ni hiyo ambayo mimekueleza
na ninachukua fursa hii kukanusha kabisa maelezo hayo siyo ya kwetu na
hata jinsi ilivyoandikwa hili tangazo siyo model yetu na namna yetu ya
kuandika taarifa…kwahiyo tunaomba pia watu wasipotoshe watu na masuala
ya Kipolisi ni nyeti mno na mtu asijaribu kutengeneza taarifa za
kupotosha watu kupitia Kiongozi wowote wa Jeshi la Polisi….”
Mwandishi
katika kuhitimisha Habari Zilizotufikia Hivi Punde alirudia na
kusisitiza kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lapiga
marufuku maandamano ya kumsindikiza kuchukua fomu mgombea Urais kupitia
CHADEMA. Hii ni kinyume na utetezi uliotolewa na uongozi wa ITV na Radio
One kwamba walikuwa na nia ya kusaidia kutoa ufafanuzi juu ya uvumi
ulioneea kwenye Mitandao kuwa Polisi walipiga marufuku maandamano.
7.0 Uamuzi wa Kamati
Kamati
iliridhika kuwa kipindi cha Habari Zilizotufikia Hivi Punde
kilichorushwa hewani na kituo cha ITV tarehe 10/08/2015 kilikiuka Kanuni
za Utangazaji.
Baada ya
kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi kutoka viongozi wa
ITV na Radio One, Kamati ya Maudhui inaamua yafuatayo:-
1.1 ITV inapewa onyo kali; na,
1.2 ITV
inatakiwa kukanusha na kuomba radhi katika taarifa yake ya Habari ya saa
mbili usiku na asubuhi kwa siku mbili mfululizo baada ya kusomwa kwa
uamuzi huu.
Endapo ITV itakiuka tena Kanuni za Utangazaji, hatua kali zaidi za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Uamuzi huu umetolewa na kusomwa Dar es Salaam siku hii ya tarehe13 Mwezi wa Agosti Mwaka 2015.
Haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu iko wazi ndani ya siku 30 tangu uamuzi unapotolewa.
Uamuzi umetolewa na:
Mhandisi Margaret T. Munyagi
Mwenyekiti
Na:
WAJUMBE WA KAMATI YA MAUDHUI
1. Bwana Walter Bgoya
2. Bwana Joseph Method Mapunda
3. Bwana Abdul Ramadhani Ngarawa
13 AUGUST 2015
Comments
Post a Comment