Hali tete Bunda, viongozi Chadema wajiuzulu


13.Ester Bulaya(aliyeko juu ya garu kulia akiwa kwenye msafara huo.
Esther Bulaya akiwa na wanachama wa Chadema.
SIKU chache baada ya mgombea ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Esther Bulaya kuteuliwa na chama hicho na kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, hali ndani ya chama hicho wilayani  Bunda imekuwa tete.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa aliyekuwa mpinzani wa Bulaya katika kura za maoni ndani ya chama hicho, Pius Masururi, kujitoa katika chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tayari Masururi ametangaza kumuunga mkono Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira katika mbio za ubunge huku viongozi 11 wa Chadema katika jimbo hilo wakisimamishwa uongozi.
Inaelezwa kuwa sababu ya kusimamishwa kwa viongozi hao kunatokana na kile kilichodaiwa kuwa kusimamisha wagombea mamluki katika nafasi ya ubunge na udiwani.
Akizungumza jana mjini hapa kupitia Redio ya Kijamii ya Mazingira FM,  Masururi alitangaza kujiunga na CCM jana muda mfupi kabla ya kuondoka na kurejea jijini Nairobi nchini Kenya.
Alisema Kamati Kuu haikutenda haki kwa kumteua  Esther Bulaya na kumwacha yeye ameshinda katika kura za maoni licha ya kushiriki kwake kukijenga chama hicho kwa kipindi cha miaka minne.
Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Chadema Wilaya ya Bunda, Rita Ikandire kwa niaba ya viongozi wanzake wanaotuhumiwa kukihujumu chama hicho wametangaza kujiuzulu nafasi zao za uongozi huku wakidai ofisi ya katibu wa Mkoa wa Mara na Taifa wamevunja katiba ya chama hicho.
“Mimi pamoja na viongozi wa jimbo na kamati  ya utendaji Jimbo la Bunda tumejiuzulu baada ya kutoridhika na  uamuzi wa Kamati Kuu lakini pia baadhi ya makatibu na wenyeviti katika  kata 20 za jimbo hili wamejiuzulu na watabaki kuwa wanachama wa kawaida wa Chadema,” alisema Rita.
Waliotangaza kujiuzulu mbele ya waandishi wa habari ni pamoja na Alfred Imanani(Mwenyekiti wa Jimbo), Emmnuel Malibwa(Katibu Mwenezi),  Dickson Kujerwa(Mwenyekiti BAVICHA), David Abogast (Mjumbe Kamati  ya Utendaji), Mwenge Webiro (Katibu BAWACHA jimbo) na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa,  Juma Omari.
Wengine ni Ng’wena Mwita (Mwenyekiti Baraza la Wazee jimbo), Damas Kunju, Kibago Kibago(Red Brigedia Mkuu) ambao wote wamedai kujiuzulu na kubaki wanachama wa kawaida.
Wakati viongozi hao wakidai kujiuzulu, mmoja wa kiongozi wa Chadema, Kaunya Yohana, alisema viongozi 11 tu ndio wamesimishwa uongozi na chama baada ya kupandikiza wagombea wasiokuwa na sifa.
“Viongozi hao hawakujiuzulu kama wanavyodai isipokuwa wamesimamishwa uongozi mpaka mambo yatakapokuwa sawa tangu tarehe 15/8/2015,” alisema Yohana.
Alisema viongozi hao wamesimamishwa kwa barua yenye kumb. Na.C/HQ/ADM/KK/08 ya tarehe 19/08/2015 iliyosainiwa na Julius Mwita Katibu wa Vijana Taifa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Chadema Taifa.
Aliwataja  baadhi ya waliosimamishwa kuwa ni pamoja na Alfred Imanani, Rita Ikandiro, Emanuel Malibwa, Damas Kunju, Dickson Kujerwa, David Abogast, Matara Athumani na Noa Laurent.
Alisema wakati viongozi hao wakitumikia adhabu hiyo chama kimeunda nguvu kazi itakayosimamia shughuli zote za chama na kuratibu mchakato mzima wa uchaguzi katika majimbo matatu ya Bunda Vijijini, Bunda Mjini na Mwibara.
CREDIT: MTANZANIA

Comments

Popular posts from this blog