Gwajima asomewa mashitaka ya kumtukana Askofu Pengo.
NA HELLEN MWANGO
Askofu Gwajima alikanusha tuhuma hizo wakati akisomewa maelezo ya awali
mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, alidai kuwa kati ya Machi
16 na 25, mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyopo
Kawe jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi kwamba ‘mimi
Askofu Gwajima nasema askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule, mjinga mmoja,
amekula nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana akili yule’
alinukuu maneno hayo.
Alidai kuwa Askofu Gwajima alitoa maneno hayo yakufadhaisha dhidi ya
Askofu Pengo na kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa Machi 27, mwaka huu mshtakiwa
alifikishwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya
kuhojiwa.
Ilidaiwa kuwa alifunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma hizo.
Hata hivyo, Askofu Gwajima alikana mashitaka hayo lakini alikiri majina
yake, wadhifa wake, kuhojiwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, kweli kanisa lake liko Kawe na kushitakiwa mahakamani hapo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unatarajia kuita mashahidi saba na watawasilisha vielelezo vitano.
Wakati huo huo, mahakama hiyo imepiga kalenda kusoma maelezo ya awali ya
kesi inayomkabili askofu huyo na wenzake watatu, baada ya mshtakiwa wa
nne kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Dyansobela Agosti 10, mwaka huu.
Mbali na Gwajima wengine ni anayedaiwa kuwa mlinzi wake George Mzava,Yekonia Bihagaze na Georgey Milulu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Machi
29, 2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, jijini Dar es
Salaam,washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakimiliki bastola aina ya
Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa
mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha
32 (1) na cha 34 (1)(2) na(3) cha sheria ya Silaha na Milipuko sura ya
223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Upande wa Jamhuri, uliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio Mzava akiwa
na wenzake hao walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola
pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun. Washtakiwa walikana
mashitaka yao kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.
CHANZO: NIPASHE
Comments
Post a Comment