BVR 8,000 kuandikisha D'Salaam.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, ametoa onyo
kali kwa maofisa waandikishaji watakaochelewa kufika na kuondoka kabla
ya muda katika vituo vya uandikishaji.
Sadiki ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
jana, alisema uandikishwaji jijini humu utaanza kesho na kuhitimishwa
Julai 31, mwaka huu.
Alisema takribani wakazi milioni mbili wanatarajiwa kuandikishwa katika
BVR na kwa wakazi wenye sifa takribani milioni mbili wa Jiji la Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa Sadiki, vituo 1,684 vitatumika katika uandikishaji kwa Manispaa za Ilala (396), Temeke (572) na Kinondoni (706).
Alisema Manispaa ya Kinondoni itakuwa na maofisa uandikishaji 1,412 na wa akiba 136, waandishi wasaidizi 706 na wa akiba 136.
Aidha, alisema Manispaa ya Temeke nayo itakuwa na maofisa uandikishaji
1,144, wa akiba 128, waandishi wasaidizi 572 na wa akiba 128.
Alisema Ilala itakuwa na maofisa uandikishaji 792 na wa akiba 144, waandishi wasaidizi 136 na wa akiba 144.
Kwa mujibu wa Sadiki, katika manispaa hizo pia kutakuwapo na ofisa
mwandikishaji wa halmashauri, ofisa uchaguzi, maofisa wasaidizi wa
majimbo na kata na wataalam wa Tehama.
Sadiki alitoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa
wingi na mapema kujiandikisha kwani kinyume chake watapoteza haki yao ya
kupiga kura.
Alisisitiza kuwa wasio raia wa Tanzania hawaruhusiwi katika uandikishwaji huo na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.
Aliwataka maofisa uandikishaji kufika vituoni kwa wakati na kuondoka kwa
muda uliowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili kuwaondolea
usumbufu wananchi.
Sadik alisema maandalizi yakiwamo mafunzo kwa wahudumu, yalishafanyika kwa manispaa zote.
Akizungumza na NIPASHE juzi, Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian
Lubuva, alisema vituo vutafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa
12:00 jioni kila siku.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, kila kituo katika manispaa hizo, kitakuwa na
mashine za BVR mbili kwani mashine 8,000 zilizokuwa zikitumika mikoa
mingine zinatarajia kuletwa jijini Dar es Salaam na hivyo kuwaondolea
hofu ya kukosa kujiandikisha kwa wakazi wake.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, wananchi wenye
sifa ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu ni 24, 252,
927.
Watu wenye sifa ya kupiga kura katika Jiji la Dar es Salaam ni 2,932,930 kati ya watu 4, 713, 213.
Awali, uandikishaji kwa mfumo wa BVR, jijini Dar es Salaam, ulipangwa
kuanza Julai 12, mwaka huu, lakini uliahirishwa kwa ajili ya maandalizi
zaidi.
CHANZO: NIPASHE
Comments
Post a Comment