ROSE MUHANDO AMWAGA MACHOZI! ATUMIA DAKIKA 45 KUELEZEA MAMBO MAZITO ANAYAOPITIA!

Mwimbaji Injili Bongo, Rose Muhando. ILIKUAJE?Brighton Masalu ROSE Muhando, aliye mwimbaji Injili Bongo, amejikuta akimwaga machozi yaliyojaa uchungu huku akitumia kama dakika 45 kuelezea wazi mateso na manyanyaso ambayo anayapitia kwa sasa ikiwemo kuhusishwa na tuhuma za utapeli na ‘kubwia unga’, Risasi Jumamosi linakupa stori kamili! Mwandishi wetu alimtafuta mwimbaji huyo juzi kwa njia ya simu kutoka mkoani Dodoma yaliko makazi yake lengo likiwa kujua maendeleo yake kikazi ndipo kukaibuka mapya mengi.Rose alianza kuporomosha lawama dhidi ya watu wanaomzushia mambo yasiyo ya kweli juu yake:

MSIKIE MWENYEWE
“Aah, mimi nipo tu (Dodoma) nimekaa kimya kwa sababu si mtu wa majibizano na malumbano, nimepakwa uchafu wa kila aina na kutukanwa huku wanaonitukana ni Wakristo wenzangu na mbaya zaidi hadi wachungaji wananisakama kwa maneno makali, nikaona kukaa kimya ni hekima.”

TUENDELEE
Rose alisema, alichukua uamuzi wa kuachana na dini yake ya zamani (Uislamu) na kujiunga na Ukristo kutokana na kuguswa na mafundisho yake baada ya kuhubiriwa upendo wa kweli lakini kwa sasa anakutana na maumivu na kusalitiwa huku wakisahau mema anayofanya kwa kutangaza Injili.

HUYU HAPA TENA!
“Wakristo wamenifundisha ugaidi na ukatili, ndugu zangu ni Waislamu, kila siku hawaachi kunisuta kutokana na matusi ninayotukanwa na Wakristo wenzangu, nakuwa sina cha kusema, kubisha nashindwa, kumkufuru Mungu nashindwa, nabaki kuugua moyoni kwa kiwango kisichotamkika.”

MATUSI YANAHUSU NINI HASA?
“Unakuta mtu amekualika kwenye tamasha. Kwa bahati mbaya ama kwa kusahau ratiba au kuingiliana majukumu, unaposhindwa kufika, inasambazwa kuwa umetapeli. Unapelekwa polisi wakati mwingine nakuwa nimewasiliana na mhusika juu ya kutofika, namuuliza nimrudishie pesa yake au kama ataandaa tamasha jingine nihudhurie, unashangaa maneno ya utapeli yanaibuka,” alisema Rose.

KILIO CHAANZA!
Rose alishindwa kuhimili kiwango cha maumivu ya moyo na kujikuta akiangua kilio hali iliyomlazimu mwandishi kupata wakati mgumu kumtuliza.

“Oke, nikatukanwa kuwa natumia unga. Ngoja nikuulize. Ingekuwa natumia unga, hivi kweli ningeweza kutunga nyimbo, kuimba na kujituma kwa namna hiyo? Nakuuliza, ninge.... (kilio kikubwa).

AKAENDELEA
“Niliowaamini ndiyo wamenigeuka, wamenitumia kwa muda mrefu na wakati mwingine kwa kunifanyisha kazi ambazo sikuwa nazitaka lakini wameona haitoshi, ni haohao waliniteka na kunipeleka porini na kunitishia maisha. Mungu atajibu na mbingu zitasimama (safari hii kwa kilio cha juu zaidi).”

ENDELEA NAYE
“Wengine wamekuwa wakinitaka kimapenzi (akataja jina), lakini kwa kutumia pesa zao nikikataa wananitishia maisha, wana wake na watoto, nabaki najiuliza kwani mimi ni kafara ya waume za watu? Eeh? Kweli jamani? Nimepelekwa porini, nikapigwa, nikaoneshwa mambo ya ajabu kweli, ili nitoe penzi kwa nguvu, yote hayo nasingiziwa makubwa na kunenewa mabaya, nina moyo wenye nyama, naumia.

“Nimewakosea nini walimwengu? Tatizo ni kuimba? Hivi hawa Wakristo hawaoni kwamba nimekuwa biashara yao nzuri kwa kuimba nyimbo nyingi zinazopendwa na wengi? Hawalioni hata hilo? Nitende wema gani wa kupitiliza hapa?”

YOTE TISA, KUMI HII HAPA!
“Wameninyang’anya vitu vyangu vingi ikiwemo vya ndani, viwanja, na wote ni waume za watu walionitongoza na kuwakataa, wengine nilifanya nao kazi kwa ukaribu, mfano... (akataja jina) na wametumia nafasi hiyo kunipokonya vitu hivyo na wanajua kwa undani uhalali na umiliki wake. Hii ni haki kweli?

“Watu wanaposikia tu Rose Muhando tapeli sasa waelewe napitia mateso magumu yanayoumiza mno, wasisikie tu naimba hivi na kudhani nina furaha ya maisha, nateseka nafsini! (kilio cha kwikwi).

AWEKA NUKTA
Katika kumalizia mazungumzo na mwandishi wetu, Rose alisema: “Waniache na safari yangu ya kumtumikia Mungu, ninachojua yeye (Mungu) atashughulika na watesi wangu na kila nafsi itayaonja mauti.”
Risasi Jumamosi linafanya juhudi za makusudi kuwasaka watu waliotajwa kwenye sauti ya Rose ili kuwasomea madai yake. Endelea kusoma Magazeti Pendwa ya Global Publishers.

Comments

Popular posts from this blog