JINSI SITTI MTEMVU ALIVYOYABADILISHA MAUMIVU YA SIKU 30 KUWA BIASHARA

Aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Uingereza kuanzia mwaka 1940 hadi 1945 na kisha kurejea tena mwaka 1951 hadi 1955, Winston Churchill aliwahi kusema, “a pessimist sees the difficulty in every opportunity; an optimist sees the opportunity in every difficulty.”

Alimaanisha kuwa “mtu muoga huona ugumu kwenye kila fursa na mtu jasiri huona fursa kwenye kila ugumu.”
2014 ulikuwa ni mwaka wenye majaribu na mitihani mingi kwa Sitti Mtemvu. Mara tu baada ya kushinda taji la Miss Tanzania 2014, skendo moja baada ya nyingine zikaanza kuibuka. Kubwa lilikuwa ni kitendo chake cha kudaiwa kudanganya umri na kuwasilisha cheti cha kuzaliwa ‘feki.’
Pia watu wakazusha kuwa mrembo huyo ana mtoto, kitu ambacho ni kinyume cha vigezo vya shindano hilo lililofungiwa mwaka jana.
Sitti alijikuta kwenye kitimoto. Jina lake likavuma mitaani, kwenye vyombo vya habari na zaidi kwenye mitandao ya kijamii. Habari yake ya kudanganya umri ikawa kubwa kuliko ushindi wenyewe wa taji hilo.
Watu wakamwita kila majina yakiwemo ‘Bibi Bomba’ na mengine ya dhihaka pamoja na kutukanwa matusi ya kila aina.
Ushindi wake wa taji la Miss Tanzania haukuja na furaha. Ulikuja na dhihaka, matusi na huzuni kubwa si kwake tu bali hata kwa familia yake. Kwakuwa wahenga walisema mchuma janga hula na wa kwao, familia ya Mzee Mtemvu ikawa ni ‘centre’ ya habari mbaya za binti yao Sitti kwa siku 30 mfulululizo.

“Hali ile ilikuwa inani-affect mimi pamoja na familia yangu,” alisema Sitti kwenye mahojiano na kipindi cha Nirvana, EATV hivi karibuni. Hayo yalikuwa mahojiano ya kwanza tangu ajivue taji hilo mwaka jana.
“Sawa nilikuwa na dream ya kuwa miss lakini ikawa inaathiri familia yangu. Ndio maana nikaamua ‘OK acha nirudishe maneno yamekuwa mengi hata nikikaa nayo siwezi kuwa happy.”
Familia nzima iliathirika akiwemo mdogo wake asiye na hatia ambaye alilazimika kuacha kwenda shule kutokana na wanafunzi wenzake kumtania kuwa ni mtoto wa Sitti Mtemvu na sio mdogo wake kama ilivyokuwa ikifahamika shuleni hapo.
“Mdogo wangu aliumia sana,” alisema Sitti kwenye mahojiano hayo.
“Ilifikia hatua alikuwa anaenda shule marafiki zake wanamtania kwa sababu sometimes naendaga kumchukua shule so wananijua. So ikafikia hatua marafiki zake wanamwambia ‘umetudanganya kumbe yule ni mama yako, wewe ni mtoto wa ‘Bibi Bomba.’ Kwahiyo ilimuathiri ikafika wakati akawa hataki kwenda shule analia kwamba ‘sitaki kwenda shule wenzangu wananitania! Kuna siku moja nakumbuka alikuja nyumbani na mimi nilisimuliwa na mama, niliumia sana, kwamba ameona kitu kibaya wameandika kuhusu Sitti, baada ya kumbembeleza ndio akasema ‘nimeona kuna sehemu wameandika Sitti ni girlfriend wa baba!”
Zilikuwa ni siku 30 za majonzi kwa Sitti Mtemvu. Kwa mwingine mwenye roho nyepesi matusi na unyanyasaji kama huo wa mtandaoni ulikuwa na nguvu ya kumkatisha kabisa hamu ya kuishi na pengine kufikiria kujitoa uhai. Ama kwa mwingine uamuzi wa haraka ulikuwa ni kukimbia nchi.
Haikuwa hivyo kwa Sitti. Baada ya kuvua taji lake, alikaa kimya kwa muda kuweza kurudisha tena ujasiri wa maisha. Kwenye kipindi cha 360 cha Clouds TV Ijumaa hii, Sitti alisema haikuwa rahisi kuyafuta majonzi hayo.
Amesema alichofanya, ni kutembelea vituo mbalimbali vya watoto yatima na watu wasiojiweza ili kujionea kwa macho yake kuwa kuna watu katika dunia hii wanaoteseka zaidi. Pamoja na kuishi katika maisha yanayotegemea neema ya Mungu tu, watu hao bado wanaishi kwa matumaini. Hiyo ilimsaidia kuuona mzigo aliubeba kuwa rahisi tu na unaoweza kukabilika.
Siku 30 za manyanyaso mtandaoni zilimpa wazo mrembo huyo la kuanzisha taasisi yake ya ‘Sitti Mtemvu Foundation,’ kitabu chake ‘Chozi la Sitti’ na kipindi cha TV kitakachoanza kkuonekana hivi karibuni.

Kwenye kitabu chake, Sitti amezungumzia maumivu na machozi yaliyomtoka katika kipindi hicho kigumu. Ametumia pia kitabu hicho kuelezea jinsi unyanyasaji mtandaoni ulivyo na athari kubwa kisaikolojia.
Nachelea kusema kuwa Sitti Mtemvu ni msichana jasiri. Na nampongeza sana kwa kuamua kutumia tukio hilo kwa kuanzisha miradi chanya ambayo kwa namna moja inaweza kumuingiza fedha pia.

Comments

Popular posts from this blog