MREMBO ABABULIWA ‘RECEPTION’ NA MTALAKA WA BOSI WAKE JIJINI DAR


INASIKITISHA sana! Muuza baa mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Halima, anajiuguza vidonda vikubwa mwilini vilivyotokana na kumwagiwa maji ya moto na mwanamke ambaye ni mtalaka wa bosi wake ambaye ndiye mmiliki wa baa anayofanyia kazi, Amani linakupa zaidi.

Halima anayedaiwa kumwagiwa maji ya moto. Kwa mujibu wa chanzo ambacho ni ndugu wa majeruhi huyo, tukio hilo lilijiri mwezi uliopita ndani ya baa moja maarufu iliyopo maeneo ya Ubungo, Dar es Salaam ambapo majeruhi huyo anafanyia kazi baada ya mwanamke huyo kuamini Halima anatembea na mtalaka wake.

Inadaiwa kuwa, mwanamke huyo ambaye ni mtuhumiwa na mwanaume mmiliki wa baa aliyejulikana kwa jina moja la Mushi waliachana miaka mingi iliyopita.“Lakini mwanamke akawa anamfuatilia mumewe kila siku na kwa kila kitu. Ilifika mahali akaambiwa kuwa, mwanaume huyo aliyetengana naye ana uhusiano wa kamapenzi na baamedi wake mmoja.”

“Ndipo siku ya tukio, mwanamke huyo alifika kwenye baa hiyo akitoka kusikojulikana. Wakati huo, Halima alikaa kwenye kiti akiangalia kaunta. Mwanamke huyo alipitiliza jikoni, akachukua sufuria yenye maji ya moto akammwagia Halima bila kujua kuwa, siye aliyemlenga mpaka Halima aliposema ‘siyo mimi’.”

“Kusema kweli baamedi aliungua sana hadi ngozi kuchunika na kuwa nyekundu kama mnyama aliyechunwa. Aliungua sehemu mbalimbali za mwili. Mfano, usoni ndiyo sana! Mgongoni pia, kifuani na mikononi,” kilisema chanzo hicho.
Ilidaiwa kuwa, maumivu ya maji yalimfanya baamedi huyo kulia kwa maumivu makali. Maana wakati anaungua, palepale ngozi ilianza kuchunika na kutoa majimaji ya malengelenge.”


Jeraha alilolipata sehemu ya bega. “Ni ukatili mkubwa sana kutendeka maana hakuna ukweli wowote kwamba, yule baamedi alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na bosi wake na hakulengwa yeye. Halafu hata kama ni kweli alikuwa na uhusiano naye, yeye walishaachana kwa miaka saba nyuma, sasa wivu wa nini?” kilisema na kuhoji chanzo hicho.

“Ishu ilikwenda kisheria kabisa, walikubaliana kuachana. Wakagawana mali na hata watoto waligawana. Wapo watoto wanne, mwanamke akachukua wawili, wengine wakabaki kwa baba yao.Kikaendelea: “Mbaya zaidi, baada ya ukatili huo, yule mtuhumiwa hakuchukuliwa hatua zozote zile! Hii inaonesha ni jinsi gani wanyonge wanaishi kwa hatari ndani ya nchi yao wenyewe. Pale hakuna cha bahati mbaya bwana.

“Halima hakuwa na pesa za kujitibu zaidi ya kutegemea misaada kutoka kwa wasamaria wema ambao walifahamu kisa kizima. Inauma sana kwa kweli.”Baadhi ya vyanzo vilidai kwamba, baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alitumia pesa kumlaghai majeruhi kwa lengo la kutochukua hatua yoyote na kwenda kumficha mahali akiuguza vidonda.

Baada ya madai hayo, Amani lilimsaka mwanamke anayedaiwa kutenda unyama huo ambapo ilidaiwa anaishi maeneo ya River Side, Ubungo jijini Dar.Hata hivyo, nyumbani kwa mwanamke huyo hakuwepo ambapo baadhi ya majirani walisema alitoka kwenda kwenye biashara zake na muda wake wa kurudi hauna ratiba inayosomeka sawasawa.

...Jeraha alilolipata mgongoni. Walipoulizwa kama wanajua lolote kuhusu mwanamke huyo kumuunguza kwa maji ya moto Halima, walisema wanatambua lakini walishaombana radhi.“Tunajua, lakini si waliombana msamaha wenyewe kwa wenyewe? Nadhani walipatana,” alisema mmoja wa majirani.

Nacho chanzo hicho kilipoulizwa kuhusu madai ya wawili hao kupatana na kusameheana, kilisema:
“Hakuna kitu kama hicho. Kwanza unajua kwamba, Halima amelazwa Hospitali ya Mwananyamala? Amelazwa kule kwa sababu hali yake bado si nzuri.”
Jitihada zote za kumpata Halima hospitalini hapo hazikufua dafu baada ya mganga mkuu ambaye ndiye aliyetakiwa kutoa kibali cha Amani kuzungumza na majeruhi huyo kuwa bize kwa muda mrefu.

Comments

Popular posts from this blog