MAOFISA WANANE WA BENKI KUU TANZANIA (BOT) KIZIMBANI KWA MASHITAKA 14 YA KUFOJI VYETI VYA KIDATO CHA NNE

Habari na Mwene Said wa Globu ya Jamii .
 Maofisa wanane wa Benki Kuu Tanzania (BOT) wamekutwa na kesi ya kujibu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salam, dhidi ya mashitaka 14 ya kughushi na kuwasilisha vyeti vya kidato cha nne vilivyoghushiwa. 
 Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao, dhidi ya washtakiwa Justina Mungai, Christina Ntemi, Siamini Kombakono, Janeth Mahengena Beatha Masawe, Jacquiline Juma, Philimina Mutagurwa na Amina Mwinchumu. 

 Hakimu Mwaseba alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri bila kuacha shaka washtakiwa wana kesi ya kujibu na kwamba wanatakiwa kupanda kizimbani kujitetea dhidi ya mashitaka yao.
Hakimu alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa utetezi wao Juni 16 hadi 17, mwaka huu. Watumishi hao wa Benki Kuu wanadaiwa kuwa katika kitengo cha kuhesabu fedha vya BoT. Mapema Septemba 19, mwaka 2008, upande wa Jamhuri uliwasomea washtakiwa hao mashitaka yao . 
Ilidaiwa kuwa siku isiyofahamika mwaka 2001, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Mungai alighushi cheti cha kidato cha nne, chenye namba S.342/43 kilichotolewa Februari 26, 1980. 
Aidha, ilidaiwa kuwa cheti hicho kilitolewa na Baraza la Mitihani la Taifa. 
Katika shtaka la pili, mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa siku isiyofahamika mwaka 2001, jijini, aliwasilisha cheti hicho huku akijua ni cha kughushi.
 
Katika shtaka la tatu na nne, ilidaiwa kuwa siku isiyofahamika mwaka 2002 jijini, mshtakiwa wa pili alighushi cheti cha kidato cha nne chenye namba za usajili S.0222/42 kikionyesha kimetolewa Novemba 26, mwaka 1999 na kwamba aliwasilisha Benki Kuu. 
Katika shtaka la tano na sita, ilidaiwa kuwa siku isiyofahamika mwaka 2001 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Komakono, alighushi cheti cha kidato cha nne chenye namba za usajili S.238-0076 kilichotolewa Machi 14, mwaka 1997 akionyesha kuwa kimetolewa na Baraza la Taifa ambapo walikiwasilisha Benki Kuu. 
Upande huo wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa katika shtaka la saba na nane, mshtakiwa wa Mahenge, anadaiwa kuwa alighushi cheti cha kidao cha nne, chenye namba za usajiliS.311/0071 kikionyesha kimetolewa Machi 14, mwaka 1997, na Baraza la Taifa ambapo aliwasilisha benki kuu. 
Aidha, shtaka la tisa na kumi, ilidaiwa kuwa siku isiyofahamika jijini, mshtakiwa Massawe, anadaiwa kuwa 2001 benki kuu, alighushi cheti cha kidato cha nne, chenye namba za usajili S.331/0071 kikionyesha kimetolewa Aprili 22, mwaka 2000, na Baraza la Taifa ambapo alikiwasilisha Benki Kuu. 
Ilidaiwa kuwa, shtaka la 11 na 12, mshtakiwa Juma, anadaiwa kuwa siku isiyofahamika mwaka 2000 jijini, alighushi cheti cha kidato cha nne chenye namba za usajili S.375/020 kikionyesha kimetolewa Machi 14, mwaka 1999 na Baraza la Taifa ambapo alikisilisha Benki Kuu. 
Pia, shtaka la 13 na 14, mshtakiwa Mutagurwa anadaiwa kuwa siku isiyofahamika mwaka 2002, alighushi cheti cha kidato cha nne, chenye namba za usajili S.0764/0012 kikionyesha kimetolewa Machi 14, mwaka 1997 na Baraza la Taifa ambapo alikiwasilisha Benki Kuu. Katika shtaka la 15 na 16, mshtakiwa Mwanchungu anadaiwa kuwa siku isiyofahamika, 2001 jijini, alighushi cheti cha kidato cha nne, chenye namba za usajili S.0307-004 kikionyesha kimetolewa Machi 28, mwaka 1991 na Baraza na Taifa, ambapo aliwasilisha Benki Kuu. Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na wako nje kwa dhamana. 

Comments

Popular posts from this blog