MANISPAA YA KINONDONI YAENDELEA KUTEKELEZA AGIZO LA RAIS LA KUONDOA MAJI KWENYE MAKAZI YA WATU TEGETA, BUNJU NA KUNDUCHI NA KUJENGA MFEREJI WA KUDUMU KUPITISHA MAJI KUELEKEA BAHARINI.

AT1
Mkuu wa mkoa wa Dar es slaam,Saidi Meck Sadiki(katikati) akiangalia athari ya maji yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni jijini Dar es slaam akiwa ameambatana na wakazi wa eneo hilo la Kunduchi Ununio.Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na DAWASA inaendelea na zoezi la kuyaondoa maji hayo pamoja na ujenzi wa mfereji mkubwa kuelekea baharini utakaokusanya maji kutoka Bunju na Kunduchi na kuyapeleka bahari ya Hindi.

AT2
Kazi ya ujenzi wa mfereji huo mkubwa wenye urefu wa kilometa 2.1 ikiendelea katika eneo la Kunduchi Ununio.
AT3
Maji yaliyotuama yakiwa bado yamezingira nyumba na makazi ya watu eneo la Boko jijini Dar es salaam ambayo harakati za kuyaoondoa zinaendelea kufanywa na manispaa ya Kinondoni.
AT4
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Said Meck Sadiki ( katikati ) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni Musa Nati wakati akikagua utekelezaji wa zoezi la kuondoa maji katika makazi ya watu eneo la Basihayo Tegeta.
………………………………………………………………….
Na.Aron Msigwa- MAELEZO
.Dar es Salaam.
Manispaa ya Kinondoni inaendelelea kujenga mfereji wa kudumu wenye urefu wa Kilometa 2.1 ili kuondoa maji yaliyojaa kwenye makazi ya watu, eneo la Basihayo -Tegeta,Bunju na Kunduchi na kuyapeleka bahari ya Hindi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais alilolitoa hivi karibuni mara baada ya kuwatembelea wananchi katika maeneo hayo walioathiriwa na mafuriko.
Akitembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo kujionea utekelezaji wa agizo hilo leo, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecki Sadiki amesema kazi ya ujenzi wa mfereji huo utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 900 inafanyika kwa kasi inayoridhisha licha ya ugumu uliopo wa kutafuta uelekeo wa maji hayo kutoakana na uwepo wa makazi ya watu.
Amesema ujenzi wa mfereji huo mkubwa unakwenda sambamba na kazi ya uondoaji wa maji ya mvua yaliyojaa katika makazi ya watu katika eneo la Basihaya inayofanywa na Shirika la maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam huku Manispaa ya Kinondoni chini ya usimamizi wa Muhandisi wake Baraka Mkuya ikiendelea na uchimbaji wa mfereji wa juu na ule utakaopita chini ardhi kuelekea baharini.
Amesema kuwa katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi mkubwa bila kuathiri makazi ya watu na kulazimika kulipa fidia kwa wananchi Manispaa hiyo inaendelea kuzungumza na baadhi ya wananchi ambao maeneo yao yatatumika kupitisha mfereji huo waruhusu kazi hiyo iendelee huku taratibu nyingine zikiendelea kufanyika.
Aidha amesema kwa baadhi ya wananchi waliojenga kuta na nyumba kwenye mkondo wa maji hususani eneo la Kunduchi Ununio na kuzuia maji kuelekea baharini maeneo yao yatabomolewa na baadhi ya hati za viwanja kufutwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Mussa Nati akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo kushuhudia zoezi la uondoaji wa maji na ujenzi wa mfereji huo amesema kuwa fedha zinazotumika katika kazi hiyo zinatolewa na manispaa ya Kinondoni, na kazi hiyo itafanywa na wataalam wa Manispaa hiyo na kufafanua kuwa kukamilika kwake kutaondoa adha ya muda mrefu ya mafuriko waliyokuwa wanaipata wakazi hao kipindi cha mvua.
“Manispaa ya Kinondoni tumetenga kiasi cha shilingi 900 kwa ajili ya kufungua maji na kujenga mifereji ya kudumu inayoelekea baharini katika ili wananchi waweze kuishi bila usumbufu wowote,na kazi hii tutaimaliza ndani ya mwezi mmoja” Amesisitiza.
Naye Muhandisi wa Manispaa hiyo Baraka Mkuya amesema kuwa kazi ya uondoaji wa maji na ujenzi wa mifereji ya wazi na ile inayopita chini ya ardhi kutokea eneo la Basihayo Tegeta na kukatisha barabara ya Bagamoyo kuelekea bahari ya Hindi urefu wa kilometa 2.1 itakamilika ndani ya mwezi mmoja.
Kwa upande wao madiwani wa eneo hilo Bw.Majisafi Sharifu,Diwani wa Kata ya Bunju (CHADEMA) na Bi.Janet Lite kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) wamesema kazi ya utekelezaji wa agizo la Rais la ujenzi wa mfereji huo inakwenda na kueleza kuwa itakuwa faraja kwa wakazi wa kata hizo kutokana na adha kubwa ya mafuriko ya maji waliyokua wanaipata wakati wa msimu wa mvua.

Comments

Popular posts from this blog