TAARIFA ZAIDI TUKUO LA KUKAMATWA KWA MAGAIDI MOROGORO
HII ndiyo
A-Z ya wale watu tisa wanaoshikiliwa na polisi jijini Dar baada ya
kukamatwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera
nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab. Mmoja
kati ya watu hao (wa kumi), Hamad Makweka aliuawa.Watu
hao walikamatwa Aprili 14, mwaka huu saa 3:30 usiku katika Kitongoji
cha Nyandero Tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero, Morogoro wakiwa na
silaha hizo ambapo ilidaiwa kuwa, walikuwa wakijiandaa kwenda kufanya
uhalifu wa ‘kigaidi’ mahali.
Ilidaiwa watu hao walilala kwenye Msikiti wa Answar Sunna uliopo Kidatu ambao unamilikiwa na Islamic Foundation.
Baada ya
kukamatwa, awali walishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Morogoro
na baadaye kupelekwa jijini Dar kwa siri ambako mahojiano makali
yanaendelea.
Habari
kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema kuwa, watu hao wanahojiwa ili kujua
ukubwa wa mtandao wao, walikuwa wakafanye tukio wapi na nani mdhafili
wao mkubwa.“Unajua kwa sasa tatizo ni kwamba, inaonekana wahalifu
wakubwa tunaishi nao, zamani tuliamini wanaweza kuingia kutoka nje ya
nchi.
“Wale
jamaa walikuwa wakijiandaa kwenda kufanya uhalifu mahali, hilo ni moja
lazima waseme. Pia lazima mtandao wao ujulikane. Jeshi la polisi
lilifanya kazi yake kwa usahihi ndiyo maana walinaswa kabla ya muda wa
kwenda kufanya tukio,” alisema askari mmoja kwa kuomba jina lake
lisitumike kwa kuwa si msemaji wa jeshi hilo. Gazeti la Uwazi lilifika
kwenye Msikiti wa Suni na kuzungumza na baadhi ya watu. Mtu wa kwanza
kuongea naye alikuwa muumini wa msikiti huo, Shani Kinyimbi ambaye
alisema:
“Kwa hili
lililotokea, mimi nawaomba viongozi wetu wa msikiti huu kuanzia leo mtu
asilale ndani na baada ya swala msikiti ufungwe. Hii ni hatari sana,
magaidi kugeuza msikiti sehemu ya maficho imeniuma sana msikiti wetu
kuchafuliwa.”
Naye
kiongozi mmoja wa msikiti huo, Mohamed Menze ambaye ni mweka hazina mkuu
alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema:“Tukio hili la kigaidi
limeuchafua sana msikiti wetu na dini yetu kwa ujumla. Kiukweli hawa
jamaa sisi kama viongozi wa msikiti hatuwajui na wamefika usiku na
kukamatwa usiku huohuo.
“Hapa
msikitini kuna vijana watatu wanalala ambao ni Hafidh Kondo, Rajabu
Shomari, Singo na Mustapha Kivale. Kwa mujibu wa vijana hao, juzi
(Aprili 14) usiku walifika watu hao wakiwa na mabegi ya kitalii na
kuswali ambapo baada ya kuswali waliomba kulala msikitini
“Wakati
wakiendelea kuongea na vijana wetu polisi walifika na kuwakamata na
baadaye kwenda kwa imamu wetu ambao walimuuliza kama ana taarifa za
ugeni huo imamu alikana kuwa na taarifa, polisi waliwakamata watuhumiwa
hao na walipopekuliwa kwenye mabegi yao walikutwa na sare za jeshi,
bendera, baruti na vitu vingine mbalimbali. Wakati huo mwenzao mmoja
alishauawa.”
Diwani wa Kata ya Kidatu, Bryson Mwanzenye alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema:
“Hili ni
tukio la kigaidi na kwa sasa kwenye kata yangu hali ni tete, mtu mwenye
ndevu nyingi na kipara (Hamad Makweka) ambaye hafahamiki alivamiwa na
kupigwa na wananchi wenye hasira hadi kufa.”
Alipotakiwa
kueleza alivyomfahamu marehemu Hamad Makweka alisema: “Huyo mtu si
mkazi wa kata yangu, anatoka Ruaha lakini mtu anapokufa ndipo mengi
yanapoibuka. Inadaiwa huyo marehemu alikuwa ni mwalimu wa kareti ambaye
majirani zake wanasema hawakujua kazi yake lakini alikuwa ni mtu wa
kusafirisafiri sana.”
Maulidi Aliphonce ambaye ni dereva wa Bajaj ya pili iliyowachukua baadhi ya watu hao kwenda nao msikitini, alisema:
“Mimi
niliwachukua watano kati ya wale watu kutoka kituo cha Ruaha. Mwenzangu
(Bajaj ya kwanza) aliwachukua watano. Tukiwa tunaenda msikitini, kwa
nyuma tulifuatwa na pikipiki mpaka tunafika msikitini.
“Nilipowashusha,
ile pikipiki iligeuza na sisi wa Bajaj tukageuza kurudi kituoni kwetu.
Lakini mtu mmoja Hamad Makweka aligeuza na mimi licha ya kwamba wakati
wa kuwabeba wenzake na yeye alikuwemo lakini alisema anarudi Kidato kwa
sababu wenzake watalala msikitini.
“Njiani
tukakutana na polisi, wakatusimamisha. Wakaanza kumuuliza maswali Hamad,
ghafla naye akatoka mbio, polisi mmoja akamkimbiza, Hamad akatoa sime
na kumkata shingoni yule askari na kutaka kuendelea kukimbia, lakini
polisi mwingine alimpiga risasi ya mguu, akaanguka na kukamtwa.
“Ndipo
wananchi wenye hasira kali walipotokea na kumpiga mpaka wakamuua kwa
kumchoma moto. Walimpiga kwa sababu alimkata shingo askari kwa kuulizwa
maswali kadhaa.” Naye Koplo Nassoro Dabi ambaye ni mchezaji wa zamani
wa Timu ya Polisi, Morogoro aliyekatwa shingo kwa sime na marehemu Hamad
ambaye kwa sasa amelazwa Zahanati ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia,
Morogoro alikuwa na haya ya kusema:
“Namshukuru
Mungu hadi leo hii napumua. Kwa kweli nilinusa kifo, sikujua kama jamaa
alikuwa na sime kiunoni. Wakati namfukuza aliingia kwenye shimo na
kuangua, nilipojiandaa kumkamata alitoa sime na kunikata shingoni
nikapoteza fahamu baada ya kutoka damu nyingi.
“Kama
ningejua ana sime ningejua namna ya kumwingia. Lakini kwa kweli ilikuwa
hali tete pale. Ila wananchi wa kule wana umoja sana.”Siku za hivi
karibuni kumeibuka uhalifu wenye kutia shaka hasa kutokana na silaha
wanazokuwa nazo wahalifu hao kiasi kwamba, wapo waliobainika kuwa na
ushirika na Kundi la Kigaidi la Al Shabaab la nchini Somalia. Mfano ni
kijana Rashid Charles Mberesero (21) ambaye alihusishwa na mauaji ya
wanafunzi 148 kwenye Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya mapema mwezi
huu.
Comments
Post a Comment