Mfanyabiashara Afia Hotelini na Kete 30 za Heroin
Mfanyabiashara
wa dawa za kulevya, Kervin Mafita (40),mkazi wa Kinondoni, Dar es
Salaam, amekutwa amekufa kwenye Hoteli iliyopo jijini Arusha akiwa na
shehena ya dawa hizo aina ya heroin tumboni mwake.
Meneja
wa hoteli hiyo, Bw. Douglas Minja, alisema marehemu alifika hotelini
hapo Aprili 12, mwaka huu, akiwa ameongozana na mama yake mzazi, mdogo
wake na mtoto wake mwenye umri wa miaka 11 na kukodi vyumba viwili.
Alisema
Aprili 15, mwaka huu, saa nne asubuhi, mhudumu wa hoteli alienda
kugonga chumbani kwa marehemu ili aweze kufanya usafi na baada ya
kufunguliwa mlango, ndani kulikuwa na marehemu, mama yake na mgodo wake
marehemu.
Aliongeza
kuwa, ndugu hao walidai muda huo walikuwa na mazungumzo hivyo
hawakutaka usumbufu ambapo kutokana na majibu hayo, muhudumu huyo
alilazimika kuwapisha ili waendelee na mazungumzo yao.
"Baada
ya saa moja, ndugu wawili (mama na mdogo wa marehemu), walitoka na
kutokomea kusikojulikana ila mtoto wake ambaye muda mwingi nilikuwa
naye, aliniomba akamsalimie baba yake chumbani.
"Alipofika
chumbani, alimkuta baba yake akiwa amelala hivyo alijaribu kumwamsha
lakini hakuamka ndipo akamfuata mhudumu na kumweleza kuwa baba yake
anamwamsha lakini haamki,"alisema Bw. Minja.
Mhudumu
alifika katika chumba hicho akiwa ameambatana na Bw. Minja na kumkuta
marehemu katika hali mbaya akitokwa mapovu mdomoni wakaamua kutoa
taarifa polisi.
"Wakati
akitolewa hotelini alikuwa hajafariki ila alikuwa kwenye hali mbaya,
baada ya kufikishwa Hospitali ya Mount Meru, alifariki wakati akipatiwa
matibabu," alisema.
Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuiana Kupambana na Dawa za
Kulevya nchini, Godfrey Nzowa,alithibitisha kutokea kwa tukio hilo
akisema marehemu alifikia katika hoteli hiyo akitokea Dar es Salaam na
alikuwa safarini kwenda nchini China ili kusafirisha dawa hizo.
Alisema
polisi kwa kushirikiana na daktari wa hospitali hiyo, waliufanyia
upasuaji mwili wa marehemu Aprili 18, mwaka huu na kukuta dawa hizo
tumboni kete 30 za heroin.
"Tayari mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya maziko," alisema Kamanda Nzowa.
Kamanda
wa Polisi mkoani humo, Liberatus Sabas, alikiri kutokea na kusema
polisi wanafanya uchunguzi wa tukio hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi
zaidi.
Comments
Post a Comment