Mazoezi ya kuondoa kitambi.
Kutokuwa na kitambi ndio ndoto ya
watu wengi kwa sasa wanaojali afya zao. Kutokana na kufumka kwa maradhi
mbalimbali baadhi ya watu wamekuwa wakihangaika kutafuta njia rahisi za
kupunguza ama kuondoa vitambi hivyo na uzito uliopitiliza.
Wapo waliamua kukaa na njaa na
wengine kutumia dawa kali wakilenga kufikia malengo yao ambayo ni kupunguza
uzito.
Lakini kuwa na kitambi ama ongezeko
la uzito linaweza kuondolewa kwa njia rahisi sana tofauti na unavyodhani. Tena
njia isiyohusisha hata chembe ya dawa itakayoweza kukuletea madhara baadaye.
Licha ya wataalamu wengi kusisitiza
kuwa kitambi au ongezeko la uzito ni matokeo ya ulaji mbovu, lakini ukweli
utabaki kuwa mazoezi kwa sehemu kubwa yana nafasi kubwa ya kupunguza uzito na kuondoa
kitambi.
Profesa Christine Rosenbloom,
mtaalamu wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Georgia, Marekani anasema kupunguza
mafuta mwilini kunaendana na ulaji wa chakula bora pamoja na mazoezi ya kila
siku.
“Unatakiwa kufanya mazoezi kwa muda
usiopungua dakika 60. Kwa kufanya hivi utaweza kuondokana na matatizo ya unene
ama mafuta tumbo,” anasisitiza.
Naye Profesa Michael Jensen wa
Kliniki ya Mayo anasema, mazoezi ya viungo yana nafasi kubwa sana ya
kuutengeneza mwili wako katika hali nzuri zaidi na pia kuufanya uwe mwepesi
pia.
Ni muhimu kuelewa kuwa
unapoushughulisha mwili wako, unauweka katika nafasi ya kuunguza mafuta na
hivyo kujiweka kwenye nafasi ya kuondokana na unene. Ikiwa utafanya mfululizo
ni wazi mwili hautakuwa na mlundikano wa mafuta.
Umuhimu wa mazoezi
Wataalamu wanasema watu wengi
huamini kuwa unene ni matokeo ya kula vyakula vyenye kalori nyingi. Hivyo kwa
kupunguza kalori wanaamini kuwa itakuwa ni njia rahisi ya kupunguza uzito wa
mwili.
Licha ya kuamini hivyo lakini
wataalamu wanasisitiza kufanywa kwa mazoezi kwani ndiyo njia pekee
itakayoufanya mwili wako kukubaliana na mpango mzima wa kupunguza hizo kalori
huku ukiipa nafasi misuli yako kuurudisha mwili katika hali inayotakiwa.
Wanasema kupunguza kalori kwa njia
isiyokuwa na mazoezi huwaweka wahusika katika hali ya kunenepa zaidi endapo
ataamua kurudi katika ulaji wake wa kawaida.
Kujenga misuli
Jambo la muhimu unalopaswa kufahamu
unapoamua kuanza mpango wa kupunguza uzito na mafuta mwilini ni kujua ni nini
hasa unatakiwa kufanya. Kuwa na malengo ndiyo jambo la msingi litakalokusaidia
kukutia nguvu na hata kufanikiwa.
Watafiti kutoka maabara ya Chuo
Kikuu cha San Diego Marekani, waliunganisha mazoezi mbalimbali ya tumbo.
Matokeo yake waligundua kuwa mazoezi ya tumbo yana nafasi kubwa sana ya kuikaza
misuli inayozunguka tumbo na hivyo kurahisisha zoezi la kupunguza kitambi na
kulifanya tumbo kuwa bapa.
Yafuatayo ni mazoezi matano muhimu katika kupunguza mafuta
tumboni:
Zoezi la baiskeli –
Hili husaidia kukata tumbo sehemu ya
chini na ya juu. Unachotakiwa kufanya ni kulala chali. Kisha chukua mikono
shika kichwani kwa nyuma upande wa kisogoni. Wakati umelala kunja miguu yako na
kisha jinyanyue hadi kujikunja mfano wa ‘c’ iliyolalia mgongo. Fanya hivyo mara
12 hadi 16.
Zoezi la “Sit ups’
Ukiwa umelala chini. Nyoosha miguu
yako. Kisha nyoosha juu mikono yako. Jinyanyue na kugusa miguu yako. Fanya
hivyo mara 20 hadi 30
Zoezi la kunyoosha tumbo
Kaa chini na nyoosha miguu yako huku
ukiitanua hadi kufikia uwezo wako wa mwisho. Geuza kifua chako hadi uweze kuona
upande wa nyuma yako kwa uzuri zaidi bila kugeuka mwili mzima. Fanya hivyo huku
ukibadilisha upande. Hakikisha unafanya mara 10 kwa kila upande, mkono wako wa
kulia uweze kuzunguka.
Zoezi kunyonga miguu
Hili ni maalumu kwa ajili ya tumbo
la chini. Lala chali na kisha nyanyua miguu yako. Anza kuinyonga kama
unavyofanya unapoendesha baiskeli. Fanya hivyo mara 20. Utasikia maumivu katika
tumbo lako la chini
Zoezi la kuzungusha kiuno
Simama na kisha shika mikono yako
kiunoni. Tanua miguu yako ili kusimama imara. Zungusha mwili wako kuanzia
kwenye kiuno kuja juu huku ukiwa umesimama bila kugeuka.
Fanya hivyo mara 20.
Ukihusisha mara kumi kwa kila upande.
Comments
Post a Comment