HAKIMU AFIA MAHAKAMANI KIUTATA JIJINI DAR
Tukio hilo la
kusikitisha na lililoibua vilio kwa watumishi wa mahakama hiyo na wale
waliokuwa na kesi, lilijiri Aprili 13, mwaka huu mahakamani hapo wakati
makarani wakiandaa mafaili ya kesi mbalimbali. HAYA ndiyo majanga! Hali ya hewa ilibadilika ghafla
katika Mahakama ya Mwanzo Ukonga, Dar kufuatia Mheshimiwa Hakimu Rogart
Venance Alphonce (54) kuugua ghafla, kudondoka na kutokwa povu mdomoni
na puani, hatimaye kufariki dunia! Inauma sana!
KUMBE ALIKUWA ANARIPOTI KITUO KIPYA CHA KAZI
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari mahakamani hapo, Mheshimiwa Alphonce siku hiyo ndiyo alikuwa akiripoti mahakamani hapo kikazi akitokea Mahakama ya Mwanzo Lugoba, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ndipo akapatwa na matatizo hayo ambapo wengi walidai kifo chake kilitokana na ushirikina.
“Huyu hakimu si mgeni kwangu, namjua kwa utendaji wake wa kazi na ni mtenda haki katika hukumu anazozitoa, amekuwa akifuata sheria bila kumuonea mtu, watu wasiompenda ni wale wahalifu ambao alikuwa akiwahukumu kwa mujibu wa sheria kulingana na makosa yao.
“Siamini kama huu ni ugonjwa wa kawaida, lazima kuna mkono wa mtu! Inawezekana amepigwa ‘manati’ (kurushiwa uchawi) huko alikotoka ili aje kufia hapa.“Nasema hivi kwa sababu hapa ofisini alifika salama akiwa na mkoba wake. Alipofika alituonesha barua iliyotoka Wilaya ya Ilala kwamba anatakiwa kuanza kazi hapa.”
TUKIO LATOKEA WAKATI WA USAFI WA OFISI
“Tulimchukua hadi kwa mkubwa wetu, hakimu mfawidhi mama Komba ambaye aliisoma ile barua na akatuambia tumwandalie ofisi yake kwa kuifanyia usafi kwani ilikuwa haitumiki kwa muda mrefu, hakimu aliyekuwa akiitumia alistaafu.
“Sasa wakati ofisi yake ikiandaliwa huku yeye bado akiwa katika ofisi ya bosi wetu tulipata taarifa kwamba, alishikwa na kukohoa mfululizo kisha akadondoka chini akitokwa na povu kinywani na mdomoni na kufariki dunia. Jamani si maajabu haya?”
WATUMISHI WA MAHAKAMA WACHANGANYIKIWA
“Kila mmoja alichanganyikiwa, tulichukua usafiri na kumkimbiza Hospitali ya Amana ambapo iligundulika kuwa alishafariki dunia.“Hali hii imetutia hofu na majonzi makubwa, ikizingatiwa kwamba katika mahakama hii kuna mahakimu wachache sana,” alisema mtumishi mmoja wa mahakama hiyo ambaye hakupenda kutaja jina lake.
Mfanyakazi mwingine wa mahakama hiyo alisema kuwa, mahakimu wanakumbana sana na mambo ya ushirikina hasa kutoka kwa baadhi ya watu wenye kesi mbaya ambao wanaamini kesi zao zitafutwa kwa imani hiyo.“Utakuta mtu anaona kesi yake ni ngumu na kosa analo kweli, ndipo uchawi huanzia hapo. Atakwenda kwa waganga ili hakimu apate matatizo.
“Sasa huyu unajua siku ileile angeingia ofisini kwake na angepewa mafaili ya kesi, hasa zile za kuahirisha. Au pengine alikotoka nako ndiyo kwenye tatizo,” alisema mfanyakazi huyo akiomba hifadhi ya jina lake.
NYUMBANI KWA MAREHEMU
Uwazi lilifanikiwa kufika nyumbani kwa marehemu maeneo ya Ulongoni A, Ukonga jijini Dar na kuongea na Emmanuel Shabani Kiria (kaka wa marehemu) kuhusiana na kifo hicho cha ghafla ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Marehemu mdogo wangu alikuwa mzima wa afya, nakumbuka zamani ndiyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo lakini alitibiwa hospitalini na kupata nafuu, ndiyo maana alikuwa akiendelea na kazi.
“Juni 13, 2005 ndiyo alimaliza Chuo cha Sheria Lushoto, Tanga akapangiwa kazi mkoani Lindi. Baadaye alihamishiwa Lugoba na mauti yamemkuta siku akiripoti katika Mahakama ya Ukonga. Taarifa niliyopata ni kwamba alizidiwa kazini akakimbizwa Amana lakini kumbe alishafariki dunia.
“Uchawi unatajwa lakini mimi siwezi kuzungumzia kwa sababu nilikuwa siishi naye.”
Hata hivyo, kaka huyo wa marehemu aliongeza kusema kwamba mdogo wake ameacha mke na watoto wanne na amezikwa Kibosho mkoani Kilimanjaro.
UONGOZI WA MAHAKAMA WANENA
Uongozi wa mahakama uliyokuwa msibani hapo ulisema kwamba, marehemu alikuwa mtu wa watu ambaye alipenda kushirikiana na wenzake na alikuwa akifanya kazi kwa kuzingatia sheria, hakumuonea mtu.
Comments
Post a Comment