ZITTO AFUNGUKA MAZITO BAADA YA KUJIUNGA ACT
Ndugu Waandishi wa habari, wanachama na wapenzi wa ACT-Wazalendo na wote mliohudhuria mkutano huu,
Kama
mnavyojua siku ya Ijumaa tarehe 19 Machi 2015 ilikuwa siku yangu ya
mwisho kuhudhuria bunge la kumi linaloendelea Mjini Dodoma.
Baada ya
kung’atuka ubunge kufuatia kukoma uanachama wangu wa chama nilichotumia
kuingia Bungeni, wengi mliniuliza ‘what is next?’
Sasa
ninapenda kuwataarifu, kama ambavyo baadhi yenu tayari mnajua, kwamba
jana siku ya Jumamosi tarehe 20 Machi 2015 nilijiunga rasmi na Chama cha
ACT - Wazalendo na kukabidhiwa kadi na Mwenyekti wa Tawi la Tegeta. Hii
ilikuwa ni moja kati ya siku muhimu kabisa katika maisha yangu ya
kisiasa. Na kwa leo kwa kweli nisingependa nizungumzie mgogoro
uliokuwepo kati yangu na viongozi wangu wa chama cha zamani wala kile
kilichotokea Bungeni. Hayo yote mnayajua, yameandikwa sana na
yameshapita. Sasa ni wakati wa kusonga mbele. Rais Kwame Nkrumah alipata
kusema "forward ever, backward never". Na kama nilivyosema Bungeni,
yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Kwa hiyo leo nitazungumzia
uanachama wangu katika chama changu kipya cha ACT - Wazalendo.
Tuna
vyama 22 kwa sasa. Na kwa kweli wengi watakuwa wanajiuliza kwa nini
nijiunge na chama kipya ambacho kimeanzishwa juzi tu na ambacho pengine
wanachama wake bado wanajaa katika kiganja cha mkono?
Nimejiunga
na ACT kwa sababu ninaona kwamba huku ndiko kunakoendana na kile
ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa, ambacho ni
kuweka mbele maslahi ya Taifa dhidi ya kitu kingine chochote. Kwa
kifupi nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo msingi mama wa
Chama cha ACT - Wazalendo.
Kama
mnavyojua mimi ni mjamaa na ninaamini katika misingi ambayo Mwalimu
Nyerere aliisimamia. ACT-Wazalendo ni chama pekee nchini
kinachokubaliana na Itikadi ya ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya
Unyerere ikiwa na lengo la kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisi
taifa. Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ni chama kinachoamini
katika msingi wa uadilifu na kimeweka miiko na maadili ya viongozi
katika kuhakikisha kwamba viongozi wote wa ACT-Wazalendo wanakubaliana
nayo kwa kusaini. Naamini kuwa na miiko na maadili kwa viongozi ni
mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu na
kwamba viongozi wanakuwa mfano wa uadilifu katika jamii. Uadilifu ni
nguzo muhimu katika kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Mtakumbuka
kwamba katika miaka yangu yote ya ubunge nimepigania uwajibikaji na
uwazi. Hii ni misingi ambayo ninaamini kwamba ni moyo wa utumishi wa
umma. Nimefurahi kwamba kati ya misingi kumi ya ACT-Wazalendo,
uwajibikaji na uwazi ni sehemu muhimu kabisa ya misingi hiyo. Uwazi ni
sehemu ya jina la chama hiki. Yote haya yamenifanya nione kwamba
sitojiona mgeni katika chama hiki. Huku ndiko nyumbani kwangu kisiasa na
katika utumishi wa umma.
Nimejiunga
na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba
Kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika kazi ndiyo msingi wa
maendeleo. Hakuna namna nchi yetu na wananchi watapiga hatua ya
kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia
umakini na weledi. Ninakubaliana na ACT-Wazalendo kwamba raslimali za
Taifa lazima zitumike kuondosha umaskini wa watu wetu. Ninajiunga na
ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Umoja ni ngao
muhimu katika ujenzi wa taifa letu na Afrika kwa ujumla. Lazima
tuirudishe nchi yetu katika misingi iliyoasisi taifa hili. Lazima
tuirudishe nchi yetu katika heshima na uongozi wa bara hili la Afrika.
Ninaahidi
kufanya kazi na vijana, wanawake, wanaume na watu wote wanaoamini
katika siasa safi na siasa za hoja. Tunataka tufungue ukurasa mpya wa
siasa hapa nchini. Siasa za masuala ya nchi yetu. Siasa za masuala ya
vijana, wanawake, wazee, wakulima, wafanyakazi, wajasirialimali,
wafanyabiashara na wote wanahangaika kuijenga nchi yetu na katika
kuondoa umaskini. Tunataka tuzungumze namna bora ya kuendesha elimu,
afya, hifadhi ya jamii, na ajira. Tunataka tujenga hoja mbadala kuhusu
namna endelevu ya kujenga uchumi shirikishi ambapo kila mwananchi
anajisikia sehemu yake.
Mwezi
Oktoba mwaka 1966 Mwalimu Nyerere alipokea maandamano ya wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ikulu. Maandamano yale yalichochewa na kasi
kubwa ya rushwa na maisha ya kifahari ya viongozi (wabenzi). Mwalimu
alifoka kwa kuuliza “ Tunajenga nchi ya namna gani”? Hatimaye Azimio la
Arusha likatangazwa.
Chama
hiki kipya kimeanzishwa katika mazingira yale yale ya mwaka 1966. Ni
wakati wa kujiuliza na kupata majawabu ya aina ya nchi tunayojenga. Sisi
ACT – Wazalendo tumeona jawabu ni kurudi kwenye misingi. Waingereza
wanasema ‘back to the future’ Let the new beginning begin.
Comments
Post a Comment