WATU WANNE MBARONI AKIWEMO M/KITI WA KIJIJI KWA TUHUMA ZA MAUAJI YAKIHUSISHA IMANI ZA KISHIRIKINA MKOANI DODOMA
Watu watatu wameuawa Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma katika matukio mawili tofauti yanayohusisha imani za kishirikina.
Akizungumzia matukio Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema tukio la
kwanza limetokea tarehe 01/03/2015 majira ya saa 01:00hrs katika
kitongoji cha Golani, kijiji cha
Masinyeti, kata ya Iduo, tarafa ya Mlali Wilaya ya Kongwa Mkoani
Dodoma ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la SAIDIA S/O CHAKUTWANGA
mwenye miaka 80, kabila Mkaguru, Mkulima Mganga wa kienyeji aliuawa na
watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kupigwa na kitu kizito kichwani
na kutobolewa macho.
Kamanda MISIME amesema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha
mauaji hayo ni imani za kishirikina wakimtuhumu marehemu kuwa anazuia
mvua kunyesha katika eneo hilo.
Pia Kamanda MISIME amesema katika tukio lingine limetokea tarehe
01/03/2015 majira ya saa 02:00hrs katika kitongoji cha Majengo, kijiji
cha Ihanda, Kata na Tarafa ya Mlali Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma ambapo
mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la PETER S/O KALULI mwenye miaka 85,
kabila Mkaguru akiwa na mkewe aitwaye KAILA W/O KALULI mwenye miaka 80,
Mkaguru wote wakulima na wakazi wa Kitongoji cha Majengo wakiwa wamelala
ndani ya nyumba yao ya tembe, waliuawa na watu wasiofahamika kwa
kuangushiwa ukuta wa nyumba yao kisha kuchoma moto na kubomoa nyumba
mbili za tembe.
Watu hao walifanya uharibifu mwingine kwa kuwaua nguruwe mmoja na ng’ombe mmoja kumkata miguu.
Aidha Kamanda MISIME amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa
chanzo cha mauaji na uharibifu huo ni imani za kishirikina wakiwatuhumu
marehemu kuwa wanazuia mvua kunyesha. Watuhumiwa wanne akiwemo M/Kiti wa
Kijiji cha Ihanda na wazee wawili wa kimila wa kijiji wanashikiliwa na
Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hili kwani taarifa zinaonyesha
waliandaa vikao vya kutekeleza mauaji haya. Upelelezi wa matukio yote
mawili unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine
waliohusika na matukio haya.
Kamanda MISIME ametoa wito kwa wananchi kutochukua sheria mkononi na
kujiepusha na imani za kishirikina zinazopelekea kuleta hofu na mashaka
kwa jamii. Alisema ni jambo la aibu kwa jamii hadi karne hii watu
kuamini kuwa kuna watu wanaoweza kuzuia mvua isinyeshe. Pia amewataka
viongozi wa maeneo mbalimbali kutoa taarifa mapema polisi pale wanapoona
mipango ya kihalifu kama hiyo ikipangwa
Comments
Post a Comment