MAMIA YA WATU WAMUAGA KOMBA SONGEA

Mwili wa marehemu kapt.John Komba, wakati ukishushwa kwenye ndege katika uwanja wa ndege wa Songea mkoani Ruvuma tayari kwa kusafirishwa kijijini kwake Lituhi Wilayani Mbinga kwa mazishi.
Mwili wa marehemu kapt.John komba, ukiwasili katika uwanja wa michezo wa majimaji mjini Songea tayari kwa ajili ya kuagwa na Wananchi mbalimbali mjini humo.
MAMIA ya wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, jana walijitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga-Magharibi, Kapteni John Komba ambao uliwasili majira ya saa 10.25 katika Uwanja wa Ndege wa Ruhuwiko, mjini hapa.
Baada ya mwili huo kuwasili kwa ndege ya kukodi mkoani hapa, ulipokelewa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mark Mwandosya pamoja na baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Ruvuma huku baadhi yao wakiangua vilio kiwanjani hapo.
Baadaye mwili huo lipelekwa katika uwanja wa michezo wa Majimaji ambapo wananchi walipata fursa ya kuuaga na kisha kuelekea kijijini kwake Lituhi kwa ajili ya mazishi ambayo yamefanyika leo.

Msafara huo kutokea uwanja wa ndege uliongozwa na pikipiki magari ya watu binafsi sambamba na vikosi vya ulinzi na usalama huku wananchi wakiwa wamejipanga barabarani kushuhudia mwili huo.

Awali, kabla ya mwili wa Komba haujaingia uwanjani, waliupitisha katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Songea kwa lengo la kutoa nafasi kwa wananchi ambao hawataweza kufika uwanjani, wapate fursa ya kuaga.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema hadi mwili unawasili, bado wananchi hakuwa wakiamini kilichotokea kwa kumpoteza mtu muhimu, makini na mbunifu na mwenye vionjo vya muziki.
Alisema, Komba alikuwa mtu wa watu wote mwenye upendo na mpenda maendeleo na kwamba kifo chake kilikuwa ni cha kushtukiza.
Aliwataka wananchi mkoani Ruvuma kuwa watulivu na watakaobahatika kwenda kuzika kijijini, walitakiwa kuwahi kabla ya Rais Jakaya Kikwete hajawasili Lituhi.
Rais Kikwete, leo alitarajiwa kuongoza mamia ya wananchi kwenye mazishi ya Kepteni Komba ambapo ilitangulia  ibada ya Misa Takatifu iliyotarajiwa kuongozwa na Askofu wa Jimbo la Mbinga, John Ndimbo.

Comments

Popular posts from this blog