KOCHA MARSH AFARIKI DUNIA
ALIYEKUWA kocha msaidizi wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Sylvestre Marsh, amefariki dunia asubuhi ya leo.
Marsh alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuungua maradhi ya saratani ya koo kwa muda mrefu, awali alilazwa hapo akapata nafuu na kupelekwa kwao Mwanza, lakini wiki iliyopita alirudishwa tena na ndipo umauti ulipomkuta.
Marsh ambaye aliwahi kuipa mafanikio makubwa klabu ya Kagera Sugar, amewahi kufundisha soka kwa mafanikio makubwa sana hapa nchini kuanzia mwaka 2003, alipokuwa kocha msaidizi wa timu ya vijana, chini ya Abdallah Kibadeni.
Mwaka 2006, alipandishwa timu ya wakubwa na kuwa kocha msaidizi chini ya Mbrazil Marcio Maximo na baadaye akawa chini ya Wadenish, Kim Poulsen na Jan Poulsen.
Hata hivyo, tangu mwaka jana kocha huyo amekuwa hana timu anayofundishwa baada ya kuondolewa kama msaidizi wa Taifa Stars, lakini mara nyingi amekuwa akijihusisha na kituo chake cha soka cha Marsh Academy, kilichopo Mwanza.
Taarifa zinasema kuwa msiba upo nyumbani kwake mtaa wa Usumau, Mirongo jijini Mwanza.
Mafanikio:
Marsh ni moja ya makocha wenye mafanikio makubwa sana kwenye soka la Tanzania, kwani mwaka 2009, akiwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, aliiwezesha timu hiyo kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Mwaka 2003 akiwa kocha msaidizi wa timu ya vijana chini ya miaka 17 aliiwezesha kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Hata hivyo, timu hiyo ilitolewa kutokana na mchezaji Nurdin Bakari kuwa na umri wa zaidi ya miaka 17.
Akiwa na timu ya Kagera Sugar, Marsh aliiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Tusker mwaka 2005.
Pia amewahi kuzifundisha timu za Toto African ya Mwanza na Azam FC ya Dar es Salaam.
Bwana ametoa na bwana ametwaa, jina la bwana lihimidiwe.
Comments
Post a Comment