HAPENDWI MTU INAPENDWA POCHI...JANGA LINALOVUNJA NDOA!

NImatumaini yangu wapenzi wasomaji wa safu hii mko poa na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku. Tumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika siku ya leo na kuweza kuperuzi ukurasa huu muhimu wa kuzungumzia masuala ya uhusiano.


Leo napenda nizungumze nanyi kuhusu mada iliyopo hapo juu. Kwa uchunguzi mdogo nilioufanya, inaonekana ndoa zilizofungwa miaka ya 80 kurudi nyuma zilikuwa na uhai mrefu kuliko miaka ya juu ya hapo.
Ndoa miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikisuasua, hazina umri mrefu. Watu wanaingia kwenye ndoa kwa kufuata kitu flani mbele ya safari kikitoweka, hayupo tayari kuvumilia, unakuwa ugomvi na ndoa kuvunjika.
Wazee wetu walifunga ndoa kwa kufuata misingi ya ndoa. Kigezo cha fedha hakikupewa nafasi kubwa katika mapenzi, walitazama zaidi suala la maisha ya kusaidiana na matakwa ya Mungu katika sheria za ndoa.
Mume alijua wajibu wake kama baba wa familia lakini mke pia alijua wajibu wake ndani ya familia. Kila mmoja alifuata kiapo alichokula siku ya ndoa, kwamba ataishi na mwenzake katika shida na raha.
Kwa kufuata misingi hiyo, katika shida walishikamana pamoja na katika raha walikuwa pamoja. Ndoa zao zilidumu hadi kufikia hatua ya kuona wajukuu na hata vitukuu.
Kadiri miaka ilivyozidi kusogea, ndoa nyingi zimekuwa hazidumu. Falsafa ya shida na raha imezidi kubomoka. Watu wanataka kuishi kwa raha, shida hawataki kuzisikia kabisa.Hapa ndipo nataka kupazungumzia leo hii. Ndoa nyingi za sasa hazidumu kutokana na misingi ambayo wanandoa wanajiwekea. Utasikia mtu akikwambia ‘hapendwi mtu inapendwa pochi au mwanaume pesa sura mtavumiliana.’
Upendo wa dhati hakuna, watu wanaoana kwa kufuata maslahi ya fedha. Wanawake wanaingia kwenye ndoa kwa kuangalia kigezo cha fedha. Akiona mwanaume hana fedha, hamkubalii hata awe na mapenzi ya dhati kiasi gani.
Matokeo yake, mwanamke wa aina hiyo, anapokutana na ugumu wa uchumi wa huyo mwanaume kuyumba, anashindwa kuvumilia na kuanza visa vya hapa na pale, ndoa inavunjika.
Hawezi kuvumilia ugumu wa maisha wakati tayari alizoea kupewa matumizi makubwa, ghafla yamekata. Hapo ndipo anapotaka kulazimisha mambo ili na yeye aendelee kuwa katika hali ileile.
Atasaliti ili aweze kupata fedha, matokeo yake mwanaume akigundua, ni ugomvi ambao kutokana na hulka yake na kwa sababu hakukupenda, ni ngumu kumbadilisha, mnafikia hatua kila mtu anachukua njia yake.
Inakuwa ni vigumu kwa mwanamke huyo kudumu ndani ya ndoa sababu kwanza hakumpenda mwanaume huyo tangu awali. Kilichomsukuma aolewe ni fedha.Tatizo hilo kwa sasa halipo tu kwa wanawake, wapo pia wanaume ambao nao wanaingia kwenye ndoa kwa kufuata fedha za wanawake. Haangalii mwanamke huyo ana nidhamu, ana heshima, mstaarabu wala mvumilivu.
Matokeo yake, anapokutana na changamoto ya mwanamke husika kuyumba kiuchumi, tabia yoyote mbaya, msuguano unaibuka na hadi kufikia hatua ya kuachana.Hayo yote yangeweza kuepukika endapo asingeingia kwenye ndoa kwa tamaa ya fedha. Fedha ndiyo zimemponza, matokeo yake ndani inakuwa kitimtim pale anapokutana na vizingiti vya fedha au tabia yoyote ya tofauti.
NINI CHA KUFANYA?
Tunapaswa kurekebisha tabia. Kubadilika na kuishi katika misingi ile ya ndoa zilizokuwa zinafungwa miaka ya nyuma. Kusimama katika viapo ambavyo mliapa wakati wa kufunga ndoa.
Tusichukulie kiapo kama fasheni, tunapaswa kuviishi katika maisha ya kila siku hadi pale kifo kitakapowakuta.
Tunapaswa kutambua kwamba kuna wakati maisha yanaweza kuwa mazuri lakini kuna wakati mwingine yanaweza kubadilika hivyo uwe tayari kuyakabili.
Mnapaswa kujua kwamba ndoa inahitaji uvumilivu, upendo, heshima na busara.
Ndoa ina uzima na magonjwa, hakikisha yule unayeingia naye kwenye ndoa ana sifa za kuishi maisha yoyote.
Ingia kwenye ndoa na mtu sahihi, mwenye moyo wa upendo na uvumilivu ili baadaye usije kujutia.
Wazazi wanatakiwa kuhakikisha wanawalea watoto wao katika misingi mizuri ya kujua shida na raha ili nao waje kuishi maisha hayo. Tukiwaacha waendelee kuishi katika mfumo huu basi ndoa zitaendelea kushuka thamani, zitatoweka kabisa maana watu watakuwa wanaoana leo, wanaachana kesho.

Comments

Popular posts from this blog