Majambazi yafunga mtaa jijini Mwanza na kuua mtu mmoja
Matukio ya ujambazi na mauaji ya kutumia silaha, yameanza kuibuka kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hali
hiyo imekuwa ikihojiwa na wananchi na wapenda amani na zaidi ni kuhusu
intelijensia ya polisi kushindwa kugundua mipango ya uhalifu.
Wachunguzi
wa mambo wanasema kuwa kushamiri kwa matukio hayo kunaleta hofu katika
jamii huku jamii yenyewe ikilaumiwa kwa kukaa kimya kwa watu wanaomiliki
silaha kinyume cha sheria na hutumia isivyo halali.
Hali
hiyo imetokea mjini Magu, mkoani Mwanza kwa watu wanaodhaniwa kuwa
majambazi wakiwa na silaha za moto usiku wa kuamkia jana walifunga Mtaa
wa Kisesa Kata ya Kisesa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza na kumuua
mfanyabiashara Nestory Andrew umbali wa mita 50 kilipo Kituo cha Polisi.
Tukio
hilo lilitokea saa 8:00 usiku, majambazi hayo yalifunga Barabara ya
Mwanza-Musoma kwa muda na kusababisha taharuki kwa wakazi wa Kisesa huku
milio ya bunduki ikitawala anga.
Wakizungumza na
Mwandishi eneo la tukio jana, mashuhuda walisema walianza kusikia milio
mizito ya vitu kama bomu na kwamba baada ya muda wakaona watu wakivamia
duka la mfanyabiashara huyo na kupiga risasi hewani.
Mmoja
ya mashuhuda hao, Daud Mwalimu alisema “Mimi ni fundi baiskeli hapa
stendi jana (juzi) muda kama wa saa mbili usiku nilisikia sauti ya
vishindo kama bomu, lakini baada ya muda nikasikia sauti za bunduki
hewani,”
Aliongeza: “Kwa kweli tulitawanyika watu wote
hapa mtaani na kuacha mali zetu. Baada ya kutulia tulikuja kushuhudia
nini kilitokea, lakini tulikuta mtu mmoja ambaye ni mfanyabiashara hapa
Kisesa anavuja damu tulimuangalia tukamkuta amefariki.”
Shuhuda
mwingine, Emmanuel Juke alisema watu hao walifunga Barabara ya
Mwanza-Musoma na kwamba, walikuwa wakipiga risasi ovyo hewani.
Juke
alisema hali ilikuwa mbaya, kwani hawakuwahi kushuhudia tukio kama hilo
na mtu aliyefariki alikuwa mfanyabiashara maarufu Kisesa.
Mwandishi
wa habari hizi jana alifika Kituo cha Polisi Kisesa ambako askari wa
kituo hicho walikiri kuwapo kwa tukio hilo huku wakitaka atafutwe
Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Magu.
Kamanda w Polisi
Magu, Charles Mkapa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini akadai
msemaji mkuu ni Kamanda wa Polisi Mwanza.
Kaimu Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Robert Mnyandwa alimtaja mfanyabiashara
aliyefariki baada ya kupigwa risasi na majambazi hao kuwa ni Nestory
Andrew mkazi wa Igoma.
Mnyandwa alisema hivi sasa
wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba, hata thamani ya mali
na fedha zilizoporwa haijajulikana kwani mhusika alifariki dunia.
“Ni
kweli tukio limetokea jana saa mbili usiku na mtu mmoja ambaye ni
mfanyabiashara wa Kisesa alipigwa risasi na kupoteza maisha. Bado
hatujamkamata mtu na tunaendelea na uchunguzi,” alisema Mnyandwa.
Kufungwa
kwa mitaa na majambazi, kumesababisha wafanyabiashara hasa
wanaojihusisha na biashara ya fedha kwa mitandao kufunga maduka yao
mapema.
Wafanyabiashara kadhaa wamekwishauawa ama kuporwa fedha zao kutokana na majambazi hayo kuvamia maduka yao.
Comments
Post a Comment