Kiongozi Wa Vijana wa JKT Waliopanga Kuandamana Atekwa na Kuokotwa Akiwa Mahututi..... Walitaka awaambie aliyemtuma kati ya Lowassa na Ukawa
KIONGOZI wa vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), waliokuwa wakiishinikiza Serikali kuwapatia ajira, George Mgoba, amelazwa katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na kisha kuteswa na watu wasiojulikana.
Mgoba ni miongoni mwa vijana waliowawakilisha wenzao zaidi ya 300
kukutana na viongozi wa juu wa Serikali hivi karibuni, akiwemo Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuzungumzia kilio chao na kupinga
upendeleo wa ajira ndani ya Jeshi.
Tukio hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linafanana na kile alichofanyiwa
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka au Mhariri
Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda,
lilimfika Mgoba Jumatatu wiki hii saa 11:00 jioni.
Mgoba, ambaye analindwa na vijana wenzake waliomaliza mafunzo ya JKT
katika wodi namba saba aliyolazwa, anadai kufanyiwa vitendo vya kinyama
ikiwa pamoja na kuchomwa sindano ambayo haijulikani aina ya dawa
iliyokuwa nayo.
Mpekuzi lilifika katika Hospitali ya Amana ambako pamoja
na mambo mengine, lilifanikiwa kuzungumza na Msemaji wa vijana hao,
Omary Bakari, ambaye alisema alipokea simu saa nne siku ya Jumatatu hiyo
hiyo ikimtaarifu kuwa Mwenyekiti wao, Mgoba, amelazwa katika Hospitali
ya Tumbi, iliyoko Kibaha, mkoani Pwani.
Alisema simu hiyo aliyopigiwa na mtu aliyejitambulisha kama askari polisi pia ilimtaarifu kuwa mwenzao huyo alikuwa mahututi.
Baada ya kupata taarifa hizo, Bakari alisema alichukua jukumu la kutoa
taarifa kwa baadhi ya vijana wenzao ambao walikutana katika Hospitali ya
Tumbi usiku huo huo.
Alisema akiwa Tumbi alipata nafasi ya kuzungumza na mgonjwa ili kufahamu kilichompata hadi kufikia hatua hiyo.
Bakari alisema mgonjwa, huku akizungumza kwa shida, alieleza
kilichomkuta ambapo alidai kuwa siku hiyo ya Jumatatu saa 11:00 jioni,
akiwa nyumbani kwake maeneo ya Mabibo Loyola, alipigiwa simu na watu
waliojitambulisha kuwa ni vijana wenzake wa JKT.
Alisema vijana hao walimtaka waonane eneo la Mabibo Mwisho ili
wazungumze kuhusu mipango ya maandamano ya kudai ajira yaliyokuwa
yamepangwa kufanyika tena keshokutwa, baada ya yale ya awali ya kuelekea
Ikulu kumuona Rais Jakaya Kikwete kugonga mwamba.
“Nusu saa baada ya kupigiwa simu alifika eneo walilopanga na kukutana na
watu hao ambao walikuwa ni wanawake wawili na mwanaume mmoja, waliokuwa
na gari aina ya Noah,” alisema.
Akinukuu maelezo ya mgonjwa, Bakari alisema baada ya kusalimiana kwa
kupeana mikono na wanawake hao, mmoja wao alimwambia ajitoe kitu katika
sikio na mara baada ya kufanya kitendo hicho alihisi mwili kupata ganzi
na hivyo kupoteza fahamu papo hapo.
Alisema baada ya kuhakikisha amezimia inavyoonekana watu hao walimfunga
kamba mikononi na miguuni na kisha kitambaa usoni na kwenda naye
kusikojulikana.
“Baada ya muda mchache kupita Mgoba alipata fahamu na kujikuta akiwa
amefungwa kamba pamoja na kitambaa usoni na hakujua anakopelekwa, ila
alisema wakati huo alihisi wanaingia kwenye bonde ambako walimshusha,”
alisema.
Alisema walipomshusha walianza kwa kumpiga, huku wakimtaka ataje ni nani aliyemtuma kuandamana kati ya Ukawa au Lowassa?
“Aliposhindwa kusema aliyemtuma ndipo walipombana sehemu za siri, vidole
na mbavu na kisha kumpiga mateke na baada ya kumuona ameishiwa nguvu
wakamvua nguo na kumlazimisha afanye tendo la ndoa na mmoja wa wanawake
hao,” alisema.
Alisema walipoona ameshindwa kufanya tendo hilo wakamnyoa nywele na
kisha kuanza kutafuta mshipa uliopo pembeni ya paji la uso, lakini
walishindwa kuupata na hivyo kuamua kumchoma sindano mkononi.
“Walihakikisha hana nguvu, ndipo walisikika wakisema wamemaliza kazi,
hivyo wakamchukua na kumtupa msitu wa Mailimoja wilaya ya Kibaha Mkoa wa
Pwani.
“Akiwa msituni alijisikia kupata fahamu, ambapo alianza kutambaa
kuelekea barabarani ambako msamaria mwema mmoja alimuona na kisha
kumpeleka Kituo cha Polisi cha Mailimoja, Kibaha,” alisema.
Alisema Polisi wa Kibaha ndio waliochukua jukumu la kumpeleka katika
Hospitali ya Tumbi saa nne usiku, kabla ya kufanya uamuzi mwingine wa
kuwasiliana na ndugu pamoja na jamaa zake.
Kwa mujibu wa Bakari, polisi hao baada ya kufanya mazungumzo na ndugu wa
Mgoba kwa minajili ya kumhamisha hospitali ili apatiwe matibabu zaidi,
badala yake walimpeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central)
kilichopo jijini Dar es Salaam.
“Cha kushangaza huko Central walimuweka rumande na baadaye walimtaka atoe maelezo pasipo kujali hali aliyokuwa nayo,” alisema.
Alisema baadaye polisi hao walimruhusu Mgoba kuondoka na kumpatia Sh 2,000, ingawa wakati huo alikuwa akijisikia vibaya.
Inaelezwa kuwa baada ya kuruhusiwa hakufika mbali, alidondoka na
alizinduka akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, jijini Dar es
Salaam.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia magari ya polisi (defender) matatu
na basi moja la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yakiwa yameegeshwa
katika viunga vya hospitali hiyo.
Kitendo hicho kililalamikiwa na vijana hao kupitia kwa Katibu wake,
Linus Steven, ambaye alisema kinatia shaka na kuonesha ubabe wakati
awali walionekana kukwepa kumhudumia mwenzao.
Alilishutumu Jeshi la Polisi kutaka kutumia tukio hilo kama la kihalifu au kuna jambo la kuvunja amani.
Mwandishi alizungumza na mke wa Mgoba ambaye hata hivyo
alikataa kutaja jina lake, ambapo alithibitisha kuwa siku ya tukio
alikuwa pamoja na mume wake nyumbani na kwamba ilipofika saa 11:00
alimuaga anakwenda kwa rafiki zake.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, kuzungumzia
tukio hilo, alikiri askari wake kumpokea Mgoba na kisha kumpeleka katika
Hospitali ya Tumbi baada ya kumuona kuwa yupo katika hali mbaya.
Kamanda Matei alisema alipofikishwa katika hospitali ya Tumbi madaktari
walithibitisha kuwa hana matatizo yoyote, na hivyo kuruhusiwa.
“Polisi wangu walimsaidia kutafuta ndugu zake na miongoni mwa waliofika
ni mmoja aliyejitambulisha kama askari polisi na mwingine Usalama wa
Taifa, aliyejitambulisha polisi alidai kuwa ni shemeji wa Mgoba, lakini
yule aliyedai usalama wa Taifa alisema ni ndugu yake kwa hiyo sisi
tuliishia hapo, hayo mengine siyafahamu, waulizwe polisi wa Dar es
Salaam,” alisema Kamanda Matei.
Kwa upande wake, Kamada wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, alisema ofisi yake ipo katika hatua za awali za
upelelezi, ingawa kuna taarifa za kukanganya kuhusu kijana huyo.
Pamoja na hilo, Kova aliahidi kutoa taarifa kamili kuanzia leo baada ya kukamilisha upelelezi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela, alisema hawezi
kuzungumzia taarifa zozote za Mgoba mpaka hapo atakapopata taarifa
kutoka kwa yeye mwenyewe au ndugu zake.
Daktari mmoja wa hospitali ya Amana aliyezungumza na mwandishi kwa
sharti la kutotajwa jina alisema mgonjwa huyo anaweza kuhamishiwa katika
Hospitali ya Muhimbili kwa kuwa hospitali hiyo haina baadhi ya vipimo
ambavyo vinaweza kubaini kitu kilichotokea kwenye damu yake baada ya
kulalamika maumivu sehemu za siri na kudaiwa kuchomwa sindano.
Kwa mujibu wa daktari huyo, Polisi walitaka kuchukua jukumu la
kumhamishia Muhimbili baada kumaliza dripu, lakini kumekuwa na mvutano
mkubwa kati yao na ndugu zake.
Mpaka kufikia jana jioni, daktari huyo alisema kuwa hali ya mgonjwa huyo
ilikuwa inaimarika, huku pia wakiwa wanasubiri kumpeleka Hospitali ya
Muhimbili.
Tukio la kutekwa kwa kijana huyo limejenga hisia kwamba huenda kuna
mpango unaandaliwa wa kummaliza nguvu kwa staili ile ile kama
iliyotumika kwa Dk. Ulimboka.
Dk Ulimboka ambaye alikuwa akiongoza wenzake kudai haki za madaktari,
alitekwa na kufanyiwa vitendo vya kinyama Juni 27, 2012, wakati Kibanda
alifanyiwa vitendo vinavyofanana na hivyo Machi 5, 2013.
Mgoba ndiye kiongozi wa vijana zaidi ya 3,000 ambao wanaishinikiza serikali kuwapatia ajira wale wote waliopatiwa mafunzo JKT.
Comments
Post a Comment