Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
YANGA
SC imetupwa nje ya kombe la Mapinduzi 2015 kufuatia kutandikwa bao 1-0
dhidi ya JKU katika mechi ya mwisho ya robo fainali iliyomalizika uwanja
wa Amaan usiku huu.
Bao
pekee la Amour Omar ‘Janja’ lililofungwa katika dakika ya 72 limetosha
kuwatumbukiza Wanajeshi hao katika hatua ya nusu fainali.
Kipindi
cha kwanza timu zote ziliuanza mchezo kwa makani na kupata nafasi
kadhaa za kufunga, lakini washambuliaji wa timu zote hawakuwa makini.
Yanga
walianza kwa kutawala mchezo huo wakipigiana pasi za uhakika kuanzia
katikati, lakini hesabu zao hazikuwa nzuri kila walipofika eneo la
hatari la wapinzani wao.
Dakika
ya 24 kipindi cha kwanza, Amiss Tambwe aliendeleza maajabu yake ya
kukosa mabao ya wazi katika michuano ya kombe la mapinduzi kwani alipata
nafasi nzuri ya kufunga kufuatia mabeki wa JKU kuchanganyana na kipa
wao Mohammed Abdallah, lakini Mrundi huyo alipiga mpira nje.
Dakika ya 35 kwa mara nyingine tena Tambwe alishindwa kuifungia goli Yanga kufuatia kupata mpira wa kona, lakini alipaisha juu.
Katika
dakika ya 42, Saimon Msuva aliingiza krosi murua kutoka winga ya
kushoto, Tambwe alipiga kichwa cha kudundisha mpira chini akimchanganya
kipa, lakini gozi hilo la Ng’ombe likapaa juu ya lango.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
Kipindi
cha pili Yanga walianza kwa kasi wakilishambulia lango la JKU na katika
dakika ya 46 Andrey Coutinho alipiga shuti kali, lakini halikulenga
lango. Ndani ya sekunde kadhaa Msuva naye alipata nafasi na kupiga shuti
ambalo halikulenga lango pia.
Dakia
ya 49 Coutinho alipiga mpira wa adhabu ndogo uliobabatiza ukuta wa JKU
na kumkuta Kpah Sherman aliyezamisha mpira nyavuni, lakini kibendera cha
mwamuzi msaidizi, Mbaraka Haule kilikuwa juu kuashiria mfungaji wa goli
pamoja na Msuva waliotea.
Yanga
waliendelea kushambulia kwa dakika zote, lakini kama ilivyokuwa katika
mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Shaba, walikuwa wanakosa nafasi za
wazi.
Licha
ya Yanga kushambulia muda mwingi, JKU walionesha ukomavu hasa katika
ukabaji wa nafasi na mtu kwa mtu, hivyo kuwafanya Yanga washindwe
kuliona lango lao kirahisi.
Wakati
Yanga wakitafuta bao la kuongoza, katika dakika ya 72, Amour Omar
‘Janja’ aliachia shuti kali lililomshinda kipa wa Yanga, Ally Mustafa
‘Barthez’ na kuzama nyavuni akiiandika JKU bao la kuongoza.
Kufungwa
kwa bao hilo kuliwaamsha hasira Yanga na kushambulia kama nyuki, lakini
uwezo wa golikipa wa JKU na nidhamu ya ukabaji ya mabeki iliwasaidia
kuzuia ‘presha’ ya Yanga.
Mpaka dakika 90 zinamalizika Yanga walikuwa nyuma kwa bao 1-0.
Hata hivyo, kamati ya mashindano ya kombe la Mapinduzi wamemtangaza Ismail Khamis wa JKU kuwa mchezaji bora wa mechi.
JKU
ambao ni vinara wa ligi kuu ya Zanzibar wamefuzu kucheza hatua ya nusu
fainali ambapo watachuana na vinara wa ligi kuu Tanzania bara Mtibwa
Sugar.
Hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo itatimua vumbi januari 10 mwaka huu uwanja wa Amaan Zanzibar.
Comments
Post a Comment