MIMI SI MENEJA TENA WA ROSE MUHANDO-MSAMA

HATIMAYE Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama, ameibuka na kutamka yeye si Meneja wa malkia wa nyimbo za injili nchini, Rose Muhando akisema amekuwa akishirikiana naye katika mazingira ya kawaida kama ilivyo kwa waimbaji wengine.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msama kwa vyombo vya habari jana, yeye akiwa mlezi wa waimbaji wote wa muziki wa Injili, amekuwa akishirikana nao kwa karibu kutokanana nafasi yake katika huduma hiyo ya uimbaji kwa kipindi cha miaka 15.
Msama, mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya muziki wa injili nchini kutokana na kuandaa matukio ya muziki huo kama Tamasha la Pasaka, uzinduzi wa albamu na Tamasha la Krismas, alisema ameamua kutoa tamko hilo kutokana na malalamiko ya muda mrefu ambayo amekuwa akipata juu ya Rose.

"Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi ikiwemo kutoka kwa viongozi wa kiroho wakiwemo wachungaji, kwamba pengine nimekuwa nikimzua Rose (Muhando) katika mtamasha wanayomualika na kushindwa kutokea.
"Lakini, naomba watumishi wa Mungu wanielewe katika hili, sipokei mialiko wala simzuii Rose. Mimi ninapokuwa na matamasha, nimekuwa nikimualika kama wafanyavyo wengine.
"Nimekuwa nikimlipa kiasi cha fedha anachotaka na hakuna zaidi, hivyo mimi sio Meneja wake," alisema Msama katika taarifa hiyo na kuongeza:
"Agosti mwaka huu, kampuni yangu ilidhamini uzinduzi wa albamu yake ya Kamata Pindo la Yesu, haikuwa na maana kwamba ni Meneja wake.
"Nilimualika uzinduzi wa albamu ya Uko Hapa ya msanii John Lissu Oktoba mwaka huu, nilimlipa fedha, lakini hakutokea kama ambavyo amekuwa akifanya kwa wengine ambao wamekuwa wakilalamikia tabia hiyo," alisema Msama.
"Pia wiki iliyopita nilikuwa na Tamasha la Krismasi tulikubaliana aje katika maonesho hayo, lakini hakutokea na tulishamlipa," alisema Msama kwa masikitiko na kuongeza kuwa amemsamehe na anamuombea kwa Mungu aweze kubadilika.
Alieleza kuwa hana tatizo na mwimbaji huyo, wala hana ugomvi naye, lakini amekuwa akipata taabu kutoka kwa baadhi ya wachungaji pale Rose anapoalikwa halafu hatokei na inaonekana yeye ndiye amemzuia.
"Sijawahi kupokea mialiko kwa niaba ya Rose, kila kitu anafanya mwenyewe, hivyo ni vyema wadau wakafahamu hilo," alisema Msama na kusema angekuwa mwepesi wa kulalamika, angeshafanya hivyo muda mrefu dhidi ya Rose.
Aidha, Msama amekana kuhusiana na madai ya Rose kutumia dawa za kulevya na kusisitiza kuwa hajawahi kumuona akijidunga kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti na kuongeza kama ikiwa ni kweli, hilo pia ni suala binafsi.
"Baadhi ya vyombo vya habari vinaandika ni mjamzito, nafikiri pia hayo ni mambo yake binafsi na hakuna mtu mwenye haki au uhalali wa kuhoji hilo.Yule ni mtu mzima na mwenye kujielewa," alisema Msama.
Rose ni mwimbaji mahiri wa muziki wa injili nchini aliyejipatia sifa ndani na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki ambaye mwishoni mwa mwaka 2013, alisaini mkatabawa kufanya kazi na kampuni ya muziki ya Sony ya Afrika Kusini.
Miongoni mwa albamu zilizompa umaarufu Rose kiasi cha kuwa alama ya mafanikio ya muziki wa injili nchini, ni 'Uwe Macho,' Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi), Jipange Sawasawa, Kitimutimu, 'Mungu Anacheka' na Wololo na Kamata Pindo la Yesu aliyoachia hivyo karibuni.

Comments

Popular posts from this blog