BREAKING NEWS: MASIKINI WALE WATOTO MAPACHA WA KIKE WALIOZALIWA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA MARA WALIOUNGANA KIFUA WAMEFARIKI DUNIA,MWANZA
Watoto mapacha wa kike waliozaliwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa
wa Mara iliyopo mjini Musoma wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo
wamefariki dunia jana majira ya saa 9.10 alasiri wakiwa katika hospitali
ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Watoto hao pacha walizaliwa januari 4 mwaka huu na mama mmoja mkazi
wa manispaa ya Musoma Helena Paulo wakiwa na uzito wa kilo 4.6 na kisha
kusafirishwa hadi katika hospitali ya rufaa Bugando kwa ajili ya
uchunguzi zaidi ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kufanyiwa
upasuaji wa kuwatenganisha.
Dk. Shukuru Kibwana ambaye ni daktari katika wodi ya watoto ya
hospitali ya rufaa Bugando, amesema timu ya madaktari wa upasuaji na
wataalamu wengine wamefanya kila lililowezekana kuokoa maisha ya pacha
hao walioungana lakini haikuwezekana na kuongeza kuwa kabla ya upasuaji,
mapacha hao walitakiwa kupitia tomografia ( CT ) na kufanya kipimo cha
ultra sound ili kujua kama watoto hao wameungana baadhi ya maeneo na
viungo muhimu.
Dk. Kibwana amesema watoto hao licha ya kuungana, madaktari bingwa wa
hospitali hiyo wamegundua kuwa viungo vyao vingi vya mwili vilikuwa
vikijitegemea, kila mmoja alikuwa na figo yake, ini na moyo wake huku
muuguzi wa zamu katika wodi ya watoto Sembosah Hiza akieleza kuwa hali
ya pacha hao ilianza kubadilika jana mchana jambo lililokwamisha rufaa
yao ya kwenda hospitali ya taifa Muhimbili kwa ajili ya vipimo zaidi na
uchunguzi.
Agosti 6 mwaka jana mkazi wa katoro wilayani Geita Neema Luswetura
alijifungua watoto wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo wakiwa na
uzito wa kilo 5.1 hata hivyo walifariki muda mfupi baadaye na mwishoni
mwa mwaka jana hospitali ya Apollo nchini India ilitangaza kufanikiwa
kutenganisha mapacha waliokuwa wameungana kutoka Tanzania katika
upasuaji uliochukua saa 11 na wataalamu 50.
Comments
Post a Comment